Halima Mdee, wenzake 18 wavuliwa uanachama Chadema

Friday November 27 2020
mdeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee
By Bakari Kiango

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Halima Mdee na wenzake 18 wamevuliwa uanachama wa chama hicho kwa sababu wamekiuka katiba na kanuni za chama hicho kwa uamuzi wao wa kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum bila chama hicho kuwapitisha.
Mbowe ametoa tamko hilo leo Ijumaa Novemba 27, 2020 saa 5 usiku wakati akisoma maazimio ya kikao cha kamati kuu kilichoketi kuanzia saa 3 asubuhi kuwajadili wabunge hao.
Waliovuliwa uanachama ni Halima Mdee, Esther Matiko,  Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart,  Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo,  Asia Mohammed,  Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest,  Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.
Kabla ya kutangaza uamuzi huo, Mbowe alitaja hatua nyingine tatu ambazo kamati kuu imezichukua ikiwa ni pamoja na  kuwavua nyadhifa miongoni mwao waliokuwa viongozi wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) na lile la wanawake (Bawacha) na kuagiza mchakato wa kujaza nafasi zao uanze  mara moja.
“Tumeagiza kurugenzi yetu ya kisheria itafute taratibu mbalimbali za kisheria kupinga mchakato wa kuwapata wabunge 19 wa Chadema kwa sababu mchakato huo ni batili kuanzia hatua ya mwanzo maana wameghushi majina na waliopelekewa majina nao wameyapokea,” alisema Mbowe.
Mbowe amesema licha ya kuwaita kuhojiwa hawakutokea huku wakitoa sababu zinazofanana kwamba waongezewe siku saba wajitafakari kwa madai wanahofia usalama wao kwa madai kuwa kuna wanachama walijipanga kuwafanyia vurugu.
Mwenyekiti huyo wa Chadema amesema wana nafasi ya kuomba radhi ili kurejeshewa uanachama wao na kama hawakuridhika na uamuzi huo wana haki ya kukata rufaa.
“Kikao cha kamati kuu hakikufanyika makao makuu ya chama tulikifanya  katika hoteli ya Ledger Plaza (zamani Bahari Beach) Ili kuhakikisha wanakuwa huru zaidi ila wao hawakuja wote na pia tuliwapigia simu kusisitiza waje, hawa dada zetu wamekumbwa na nini,” amesema Mbowe.

Advertisement