Halmashauri zatakiwa kusajili vikundi maalum vya zabuni kufikia Septemba

Muktasari:
- Serikali imesema vikundi hivyo ambavyo ni wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu vinapaswa kupewa fursa za kiuchumi kupitia zabuni zinazotolewa na taasisi za umma, ambazo kwa mujibu wa sheria zinapaswa kutenga asilimia 30 ya thamani ya bajeti ya ununuzi wa mwaka kwa ajili ya makundi hayo.
Mwanza. Serikali imezielekeza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaanzisha na kusajili angalau vikundi maalum 20 katika Mfumo wa Manunuzi ya Umma (NeST) ndani ya miezi mitatu kuanzia Julai 3 hadi Septemba 3, 2025, kupitia Maofisa Maendeleo ya Jamii katika maeneo yao.
Agizo hilo limetolewa leo Alhamisi, Julai 3, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk John Jingu, wakati wa mafunzo kwa Maofisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Mwanza kuhusu ushiriki wa makundi maalum katika utekelezaji wa agizo la serikali la kutenga asilimia 30 ya zabuni za umma kwa makundi hayo.
Dk Jingu amesema vikundi hivyo ambavyo ni wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu vinapaswa kupewa fursa za kiuchumi kupitia zabuni zinazotolewa na taasisi za umma, ambazo kwa mujibu wa sheria zinapaswa kutenga asilimia 30 ya thamani ya bajeti ya ununuzi wa mwaka kwa ajili ya makundi hayo.
Tangu kuanza kwa mfumo wa NeST Julai, 2023 hadi Mei, 2025 vikundi 85 vya vijana vimepata zabuni zenye thamani ya Sh3.1 bilioni, vikundi 95 vya wanawake vimepata zabuni za Sh5.6 bilioni, vikundi vitatu vya watu wenye ulemavu zabuni 12 zenye thamani ya Sh138.5 milioni na vikundi vitano vya wazee zabuni 17 za Sh800.6 milioni.
“Kupitia kwenu Maofisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri zote nchini, tuhakikishe kila halmashauri inakuwa na vikundi visivyopungua 20 vilivyosajiliwa kwenye mfumo wa manunuzi, na vyenye sifa za kushiriki katika michakato ya zabuni,” amesema Dk Jingu.
Ameongeza kuwa baada ya usajili, vikundi hivyo viunganishwe na fursa zilizopo katika maeneo yao, zikiwemo taasisi za serikali na mashirika binafsi, huku akisisitiza kuwa elimu iendelee kutolewa kwa jamii kuhusu uwepo wa fursa ya asilimia 30 ya zabuni za umma kwa makundi maalum.
Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Ziwa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Juma Mkoja amesema zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya Serikali huelekezwa kwenye manunuzi ya umma, hivyo makundi ya wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu yanapaswa kuchangamkia fursa hiyo ili kujiongezea kipato.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma namba 10 ya Mwaka 2023, kifungu cha 64, taasisi zote nunuzi zinalazimika kutenga asilimia 30 ya bajeti ya mwaka ya ununuzi kwa ajili ya makundi maalum ili yaweze kunufaika na zabuni hizo.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Juliana Kibonde amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo Maafisa hao ili waweze kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuanzisha na kurasimisha vikundi maalum, na kuhakikisha vinashiriki kikamilifu katika mchakato wa manunuzi ya umma.
“Lengo lingine ni kuyaongoza makundi maalum katika kupanga, kuandaa na kuwasilisha zabuni zinazokidhi vigezo vya kisheria,” amesema Kibonde.
Ameongeza kuwa washiriki wa mafunzo hayo watafundishwa pia namna ya kuainisha taratibu za msingi za usajili wa vikundi maalum, unaofanywa na taasisi husika, na namna ya kushiriki katika zabuni zinazotolewa na taasisi za umma.
Zakia Mohamed, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, amesema elimu hiyo itawawezesha kuhamasisha jamii na kuwajengea wananchi uelewa juu ya fursa ya kupata fedha kupitia zabuni za umma badala ya kutegemea mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri pekee.