Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hatari vifungashio vyenye taarifa za watu vikisambaa

Muktasari:

  • Ni vile vinavyotengenezwa kwa karatasi za mitihani ya wanafunzi, barua za maombi ya kazi, nakala za vyeti vya kuzaliwa na nyaraka nyingine zinazowasilishwa kwenye taasisi mbalimbali.

Dar es Salaam.  Umewahi kukutana na kifungashio kilichotengenezwa kwa karatasi zenye taarifa binafsi za mtu? Kama hujawahi kukutana na hili basi karibu Dar es Salaam Jiji lenye kila aina ya hekaheka, huku unaweza kufungiwa maandazi kwenye nakala ya cheti cha mtu cha kuzaliwa au karatasi ya mtihani.

Awali, ilionekana kawaida lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda tabia hii inaota mizizi na watu wameanzisha biashara ya kutengeneza vifungashio vya karatasi huku malighafi kubwa ikiwa karatasi zenye nyaraka na taarifa za watu.

Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la The Citizen umebaini kuwa, biashara hii imeshika kasi kutokana na karatasi hizo kuuzwa kwa gharama nafuu ikilinganishwa na zisizokuwa na maandishi.

Kando na hilo imebainika kuwa, watumishi katika ofisi na taasisi zinazotoa au kukusanya nyaraka hizo ndiyo wanaohusika kuuza kati ya Sh1,000 hadi Sh3,000 kwa kilo.

Pia, imebainika wale wanaopewa jukumu la kufanya usafi na kupanga mafaili kwenye ofisi hutumia fursa hiyo kuchukua nyaraka na kwenda kuziuza.

 “Nina mtu anafanya kazi kwenye shule moja Ilala. Huniambia kila wanapotaka kutupa nyaraka za zamani. Namlipa kama Sh2,000 au Sh3,000, ananipa gunia zima. Pia, napata karatasi kutoka kwa wasafishaji wa ofisi za Serikali. Hawajali kilichoandikwa kwenye karatasi, wanachojali ni kulipwa,” amesema mfanyabiashara mmoja wa Buguruni aliyekataa kutajwa jina.

Wengine hupendelea kununua kutoka kwa wauzaji wa jumla wanaokusanya karatasi kutoka vituo vya uchapishaji au idara za usajili katika taasisi za umma.

“Wapo madalali wenye makubaliano na walimu au watunza mafaili. Wananunua nyaraka hizo moja kwa moja na kuzileta Kariakoo au Kisutu kutuuza sisi. Karatasi safi ni ghali zaidi. Tunalipa hadi Sh1,800 kwa kilo, wakati chafu tunapata kwa Sh1,000,” amesema Samia Konje, mfanyabiashara wa vifungashio kutoka Tandale-Magharibi.

Akizungumzia hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mawasiliano wa Tume ya Kulinda Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania (PDPC), Innocent Mungy amesema tume hiyo inasisitiza kuwa, taarifa binafsi lazima zihifadhiwe au kuharibiwa ipasavyo.

Hata hivyo, wafanyakazi wasio waaminifu wamekuwa wakiuza nyaraka hizo, ambazo baadaye hutumika kufungia chakula hata dawa katika baadhi ya maduka ya dawa.

“Tume tayari tumetoa mwongozo kwa watu binafsi na taasisi zinazokusanya taarifa kwa kutumia nakala ngumu (hard copies). Zinatakiwa kuwa na mfumo rasmi wa kuziharibu, iwe kwa kuziteketeza au kutumia mashine za kuchana karatasi, mara tu zinapokuwa hazihitajiki tena. Tumewashauri kufanya hivyo mara tu nyaraka hizo zitakapomaliza matumizi yake,” amesema Mungy.

Pia, amesema taasisi zinapaswa kuwa na sera za ndani zinazofafanua jinsi taarifa binafsi zinavyoshughulikiwa na kuharibiwa baada ya matumizi.

“Kwa mfano, mtu anapoombwa kuwasilisha nakala ya cheti cha kuzaliwa, CV au nyaraka za kitaaluma, ana haki ya kufahamu taarifa hizo zitatumika kwa namna gani na zitaondolewa vipi baada ya matumizi. Taasisi zinapaswa kuwafahamisha wahusika sababu ya kukusanya taarifa hizo na kama kuna uwezekano wa kuzirejesha baada ya matumizi,” amefafanua Mungy.

Hata hivyo, amesema  ili hatua za kisheria zichukuliwe, ni lazima mtu aliyeathirika awasilishe malalamiko rasmi kwa tume.

“Kuna utaratibu wa kuwasilisha malalamiko kwenye tovuti yetu, pamoja na namba za simu ambazo watu wanaweza kutumia kuripoti matukio kama haya. Tume itachukua hatua endapo tu itathibitishwa bila shaka kuwa kuna ukiukwaji wa taarifa na kwamba, mtu aliyeripotiwa ndiye aliyesababisha,” amesema Mungy.

 “Mtoa malalamiko pia anawajibika kuonesha namna alivyoathirika na uvujaji huo wa taarifa. Katika hali kama hiyo, tume huunda jopo la kuchunguza, kuamua adhabu stahiki na kupendekeza hatua zaidi. Kama taasisi au mtu aliyekiuka sheria hajajiandikisha kuwa mkusanyaji au mchakataji wa taarifa, hiyo pia huwa ni kosa la ziada,”amesema.


Hali ilivyo mtaani

Licha ya kwamba tatizo hili limeenea, maeneo yaliyoathirika zaidi na biashara hii ya vifungashio visivyo rasmi ni Kariakoo na Kisutu, ambako mahitaji ya vifungashio vya bei nafuu ni makubwa.

Biashara hii imewezesha mtandao mkubwa wa wafanyabiashara wasio rasmi wanaofungia bidhaa za chakula kwa kutumia nyenzo hizi bila kujali umuhimu wa taarifa zilizomo.

Licha ya madhara yanayoweza kutokea, wengi wao hudai hawakuwa na taarifa kuwa wanakiuka sheria.

“Hatuna muda wa kusoma kilichoandikwa. Tunachotaka ni karatasi ya kufungia viazi au mihogo. Kama zingekuwepo safi, tungesitumia hizo, lakini hizi ndizo tunazoweza kumudu,” amesema Fatuma Selemani, muuzaji wa mihogo sokoni Kisutu.

Muuzaji mwingine wa Ilala, Hussein Rashid, amesema, “tunachonunua ni kile kilichopo. Si kama tunamuibia mtu.”

Mashuhuda wasimulia

Kwa wateja, mshangao huja baada ya ununuzi, wengi hugundua kuwa wamefungashiwa kwenye nyaraka zenye  taarifa binafsi za watu.

“Nilinunua karanga kutoka kwa muuzaji wa mtaani Mchikichini. Nilipofungua karatasi, ilikuwa na cheti cha shule kilichoandikwa jina kamili, namba ya mtihani na matokeo. Nilishtuka sana. Vipi kama kingekuwa changu?” amesema Brenda Joseph, mwanafunzi wa chuo kikuu jijini Dar es Salaam.

Hussein Omary ambaye ni mkazi wa Kinondoni, amesema amewahi kukutana na cheti cha mtu cha kuzaliwa aliponunua maandazi.

 “Kilikuwa na kila kitu kuanzia jina, tarehe ya kuzaliwa, majina ya wazazi. Hili suala linapaswa kuangaliwa kwa jicho la kipekee, inakuwaje taasisi za Serikali zinashindwa kutunza nyaraka zenye taarifa muhimu za watu,” amesema Omary.


Sheria Inasemaje?

Wakili Josephat Lusajo amesema chini ya Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi ya Tanzania Na. 11 ya mwaka 2022, iliyoanza kutumika Mei mosi, 2023, matumizi ya nyaraka binafsi kwa namna hiyo yana madhara kisheria.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kutumia  taarifa binafsi za mtu bila idhini ni kosa na adhabu yake ni faini kati ya Sh100,000 hadi Sh20 milioni, kifungo cha hadi miaka 10 au vyote viwili.

Taasisi kama shule, ofisi au vituo vya uchapishaji zinazoruhusu uvujaji wa taarifa zinaweza kutozwa hadi Sh5 bilioni.

Pia, uharibifu usio halali, kuanika  au kubadili taarifa binafsi ni kosa la jinai. Iwapo adhabu maalumu haijaainishwa, adhabu za jumla ni faini kati ya Sh100,000 hadi Sh5 milioni au kifungo cha hadi miaka 5.

Utekelezaji wa sheria hii unasimamiwa na PDPC inayoweza kutoa onyo, notisi ya utekelezaji au adhabu kwa yeyote anayeshindwa kushughulikia ukiukwaji ulioripotiwa.

Kwa mujibu wa wakili huyo, mtu aliyeathirika na uvujishwaji huo wa taarifa zake binafsi ana haki ya kuwasilisha malalamiko rasmi ambayo tume lazima iyachunguze na kuyatatua ndani ya siku 90.

“Matumizi ya nyaraka kama vyeti vya shule, CV au namba za kitambulisho bila idhini ni ukiukwaji wa sheria na unastahili adhabu,” amesema Lusajo.

 “Lakini jambo la msingi zaidi ni kuwa sheria inawawajibisha wa kwanza waliokusanya taarifa yaani taasisi kama shule, hospitali na ofisi. Wao wanapaswa kuhakikisha taarifa hizo zimehifadhiwa au kuharibiwa ipasavyo.”