Prime
Hatari ya kubeba vifurushi usivyovifahamu
Muktasari:
- Uchunguzi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) umeonyesha kuwa mitandao ya usafirishaji wa dawa za kulevya imekuwa ikibadilika mara kwa mara na kutumia mbinu mpya, ikiwemo kuficha dawa hizo kwenye mizigo na vifurushi vinavyoonekana vya kawaida ndani ya vyombo vya usafiri wa umma.
Dar es Salaam. Kitendo cha kumsaidia mtu kubeba kifurushi au mzigo wake kinaweza kuonekana kuwa ishara ya utu na msaada wa kawaida, hasa katika safari za mabasi ya mikoani, lakini nyuma yake kuna hatari kubwa.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeonya kuhusu tabia hiyo, ikisema huo unaweza kuwa mwanzo wa matatizo makubwa ya kisheria ikiwa mzigo husika utabainika ni dawa za kulevya.
Tahadhari hiyo imetolewa baada ya matukio mengi ya wahalifu kuwatumia abiria, wahudumu wa mabasi na wananchi wengine kusafirisha dawa za kulevya bila wao kutambua walichobeba.
Ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu tatizo hilo, DCEA imezindua mfango wa kutoa elimu kwa umma kupitia filamu.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema wameamua kufanya hivyo, kwa kuwa wahalifu wengi hutumia mwanya wa huruma na kuaminiana kwa wananchi kufanikisha usafirishaji wa dawa za kulevya.
“Usikubali kubeba mzigo, kifurushi au bidhaa yoyote usiyoifahamu. Hakikisha unatambua unachobeba, kinatoka kwa nani na kinaelekea kwa nani. Kifurushi unachodhani ni cha kawaida kinaweza kubeba dawa za kulevya na kubadili maisha yako kwa matokeo hasi,” ameonya Lyimo.
Kwa mujibu wa DCEA, baadhi ya watu wamejikuta wakikamatwa na kuhojiwa na vyombo vya dola baada ya kubeba mizigo waliyopewa na watu wasiowafahamu vizuri, wakiamini kuwa walikuwa wanasaidia tu.
Kwa mfano, abiria anaweza kuombwa na mtu aliyekutana naye stendi kupeleka kifurushi kwa ndugu anayekisubiri mkoa mwingine. Bila kufungua au kujua kilichomo ndani, anaweza kukubali kwa nia njema.
Hata hivyo, kifurushi hicho kikikamatwa na kubainika kuwa ni dawa za kulevya, abiria huyo ndiye anayebeba jukumu la kwanza la kueleza kilichomo na namna alivyokipata.
Mmoja wa wasafiri wa mara kwa mara kati ya Dar es Salaam na Mwanza, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema tahadhari hiyo ni muhimu kutokana na tabia iliyozoeleka ya watu kubebeshana mizigo safarini.
“Mara nyingi watu huomba msaada wa kubebewa mizigo bila kuulizwa maswali mengi. Baada ya kusikia matukio ya watu kukamatwa kwa sababu ya vifurushi wasivyovijua, sasa nimeamua kutokubali kubeba mzigo wowote ambao siujui chanzo chake,” amesema.
Kwa mujibu wa Lyimo, uchunguzi wa hivi karibuni umeonyesha kuwa mitandao ya usafirishaji wa dawa za kulevya ambayo imekuwa ikibadilika mara kwa mara na kutumia mbinu mpya, ikiwemo kuficha dawa hizo kwenye mizigo na vifurushi vinavyoonekana kuwa vya kawaida ndani ya vyombo vya usafiri wa umma.
Takwimu za karibuni kutoka DCEA zinaonyesha kuanzia Juni 2025 hadi Juni 2026, mabasi 15 yamekamatwa na watumishi 41 wa mabasi hayo wamekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sharia kutokana na mizigo wanayobebeshwa.
Mbali na mabasi hayo, bodaboda 171 nazo zimekamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja zikiwa zimetumika kusafirisha aina mbalimbali za dawa za kulevya.
Amesema baadhi ya wananchi wakiwemo makondakta na madereva wa mabasi wamejikuta wakikabiliwa na matatizo makubwa ya kisheria, baada ya kukubali kubeba mizigo ya watu wasiowafahamu au bila kujiridhisha kuhusu kilichomo ndani vifurushi husika.
“Hapo ndipo wahalifu wanapotumia mwanya huo. Wanatumia mwonekano wa kawaida wa kifurushi au mzigo, kuwafanya watu waamini hakuna tatizo, kumbe ndani kuna dawa za kulevya,” amesema.
Filamu ya Kifurushi
Kutokana na hali hiyo, DCEA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Bodi ya Filamu Tanzania imeandaa filamu iitwayo “Kifurushi”, ambayo itaonyeshwa kwenye mabasi nchini ikilenga kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kufahamu kilichomo kwenye mzigo wanaoubeba au kuusafirisha.
Kampeni hiyo yenye kaulimbiu ya ‘Usafiri Salama Bila Dawa za Kulevya’ inalenga kutoa elimu hiyo kwa madereva, makondakta, wahudumu wa mabasi, wasafirishaji wa mizigo, abiria na wananchi kwa ujumla.
Filamu hiyo inaonesha simulizi za maisha halisi kuhusu namna mtu anavyoweza kuingia kwenye mtego wa wahalifu bila kutambua na madhara yanayoweza kufuata baada ya kukamatwa akiwa na mzigo usio wake.
Lyimo amesema mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayawezi kuachiwa vyombo vya dola pekee, bali yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi kwa kuwa makini na kutoa taarifa za vitendo vinavyohusiana na usafirishaji wa dawa hizo.
Amewataka wamiliki wa mabasi na makampuni ya usafirishaji kuipa kipaumbele filamu hiyo kwa kuhakikisha inaonyeshwa kwa wasafiri wote ili kila safari iwe darasa la elimu dhidi ya dawa za kulevya.
“Kwa pamoja tunaweza kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya, kulinda vijana wetu, kuimarisha usalama wa jamii na kujenga taifa lenye afya, nguvu kazi salama na maendeleo endelevu,” amesema Lyimo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti wa Latra, Halima Lutavi amesema filamu ni njia yenye nguvu ya kufikisha ujumbe kwa wananchi, ikibadilisha mtazamo na tabia ya jamii.
Amesema mamlaka hiyo kwa kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya usafiri na vyombo vya dola, inaendelea kusimamia uzingatiaji wa sheria na kanuni za kuzuia matumizi mabaya ya vyombo vya usafiri.
“Wahalifu, wabebaji, na wasambazaji wamekuwa wakitumia vyombo vya usafiri vibaya, jambo linalohatarisha usalama wa wasafiri wengine na kudhoofisha taswira ya sekta ya usafirishaji. Niwasihi wamiliki wa mabasi, madereva, na wahudumu, pamoja na wananchi wote, kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu ili tuweze kushirikiana katika kudhibiti tatizo hili.
“Ninaamini filamu hii itasaidia kuongeza uelewa wa jamii, hivyo kuimarisha mapambano dhidi ya usafirishaji wa madawa ya kulevya nchini,” amesema Halima.
Akizungumza hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mohamed Abdallah amesema janga la dawa za kulevya, lina madhara makubwa kwa afya, usalama, na uchumi wa Taifa.
“Tunatambua kuwa tatizo la dawa za kulevya lina athari kubwa kwa afya za wananchi, usalama wa jamii, na uchumi wa taifa letu. Hivyo, matumizi ya filamu kama chombo cha kuimarisha na kuhamasisha jamii ni hatua muhimu katika kuimarisha mapambano dhidi ya janga hili,” amesema Abdallah.
Amesema sekta ya usafirishaji wa abiria ni kiungo muhimu katika kuhakikisha mifumo ya usafiri haihusiki au kutumiwa vibaya kwa namna yoyote kusafirisha madawa ya kulevya.
“Kwa hiyo, Taboa inaendelea kushirikiana na Serikali na taasisi zake katika kuimarisha ulinzi, utoaji wa taarifa, na elimu kwa wadau wetu. Tumeipokea filamu hii na tunaahidi kutoa ushirikiano wa hali ya juu, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wanachama wetu na jamii, ili kuongeza uelewa kuhusu madhara ya dawa za kulevya na umuhimu wa kushiriki katika mapambano dhidi yake,” amesema.