Hatua kwa hatua kinachoendelea mgomo wa Kariakoo
Muktasari:
- Licha ya kuwapo katika maeneo yao ya biashara, wafanyabiashara hawajafungua maduka jambo linaloibua changamoto kwa wananchi wanaokwenda kununua bidhaa
Dar es Salaam. Wafanyabiashara katika soko la Kariakoo, jijini Dar es Salaam wamegoma kufungua maduka yao leo Jumatatu, Juni 24, 2024 ikiwa ni mgomo uliotangazwa kufanyika.
Taarifa ya mgomo huo usio na kikomo zilianza kujulikana kupitia mitandao ya kijamii, baada ya kusambaa kwa vipeperushi vilivyowataka wafanyabiashara kutofungua maduka hayo kuanzia leo.
Licha ya viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kitaifa na wale wa Soko la Kariakoo kukana kuhusika katika mgomo huo, wafanyabiashara wameitikia wito, huku wakiwa hawajui ni saa ngapi watafungua maduka.
Mgomo huo unatajwa kuchochewa na kamatakamata inayofanywa na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na utitiri wa kodi wanazotozwa.
Akizungumza na Mwananchi Digital mmoja wa wafanyabiashara katika soko hili, Martha Masanja amesema tangu afike saa moja ameshindwa kufungua duka lake, baada ya kukuta wenzake wote wamefunga.
“Kero kubwa ni TRA. Mimi niko hapa kusaidia sauti isikike, hatujajua watatuambia tufungue saa ngapi ila tunasubiri,” amesema Martha.
Kuwepo kwa mgomo huu ni maumivu kwa wafanyabiashara wa mikoani ambao walifika kufunga mzigo bila ya kujua kilichokuwa kikipangwa awali.
“Unajua kabla sijatoka jana nyumbani (Mbeya) kuja huku nilikuwa nimeona hicho kipeperushi nikajaribu kuuliza kuhusu huo mgomo baadhi wakaniambia haujatangazwa na mwenyekiti, basi wakanipa moyo kuwa hautakuwepo matokeo yake nimekwama,” amesema Silvester Mwaipopo.
Mwaipopo alipanga kuondoka na gari la leo usiku kurudi jijini Mbeya, lakini mpaka sasa hajui kama ratiba yake itaenda kama alivyopanga.
Wakati maduka yakiwa yamefungwa, imekuwa ni kicheko kwa wafanyabiashara ndogondogo ‘machinga’ ambao wanaendelea na shughuli zao kama kawaida katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo.
Kelele zao za kutangaza bei ndizo zinasikika zikiita wateja huku na kule, huku wengine wakiwaambia wateja kuwa wao ndiyo wanaweza kuwahudumia na hakuna duka liko wazi.
Mbali na waliotoka mikoani, wapo waliotoka nchi jirani kwao ni maumivu pia, baada ya kufika asubuhi kukuta maduka yamefungwa.
“Sikujua kama kuna mgomo, nia yangu ni kufunga mzigo leo na nilipofika hapa nimekuta maduka yote yamefungwa, nilipouliza nikaambiwa leo hawafungui. Nilitarajia kuondoka kesho, sasa hapa gharama itaongezeka,” amesema Grace mfanyabiashara kutoka Zambia.
Mbali na wafanyabiashara hao kulalamika, wale wanaofanya shughuli zao sokoni hapa wanasema mpaka sasa hawajapata majibu ya yaliyokuwa yamelalamikiwa mwaka jana.
“Viongozi hawapo upande wetu, tangu mwaka jana tulipogoma malalamiko yetu hayajapewa majibu, tungekuwa tumepewa tusingegoma, ile tume iliyoundwa haikuja na majibu ya yale yaliyofikiwa,” amesema Lazaro Michael.
Happiness Tesha, amesema mbali na kutokuwapo kwa majibu yanayoeleweka juu ya malalamiko yao waliyotoa mwaka uliopita, bado kodi zimezidi kuongezwa jambo linalowaumiza.
“Wengine kodi mpya inakuja umeshanunua mzigo upo ndani, unataka tuuzeje? Tutapata wapi faida mnatuumiza,” amesema Tesha.
Mwananchi bado imepiga kambi katika soko hili na itaendelea kukujuza yale yatakayoendea.