Hatua kwa hatua mafuriko Arusha

Muktasari:

  •  Mvua hiyo iliyoanza kunyesha jana Aprili 10, 2024 kuanzia saa 2 usiku, imesababisha makazi ya baadhi ya wananchi kuharibiwa na wengine kunusurika baada ya kuokolewa na majirani. Hata hivyo, hakuna vifo vilivyoripotiwa hadi sasa.

Arusha. Mvua kubwa iliyonyesha takribani saa 12 zilizopita katika maeneo mbalimbali mkoani  Arusha, imesababisha athari kwa wananchi ikiwemo mazao kusombwa na maji, nyumba na maduka na stoo za kuhifadhia mazao na bidhaa kujaa maji katika eneo la Kisongo.

Baadhi ya madaraja yaliyopo katika eneo hilo yamejaa miti na mawe yaliyotoka milimani huku baadhi ya magari yaliyokuwa yameegeshwa  yakiwa yamesombwa na maji na mengine yakiharibiwa vibaya.

Simulizi waliokumbwa na mafuriko Arusha wakielezea hali ilivyokuwa usiku

Vijiji kadhaa vilivyopo katika eneo la Kisongo, kata ya Mateves, wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, vimeathiriwa na mvua hiyo ambapo baadhi ya makazi ya watu, maduka yenye bidhaa na stoo za mazao mbalimbali kujaa matope.

Mvua hiyo iliyoanza kunyesha jana Aprili 10, 2024 kuanzia saa 2 usiku, imesababisha makazi ya baadhi ya wananchi kuharibiwa na wengine kunusurika baada ya kuokolewa na majirani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Aprili 11, 2025, mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo, Tatu Kisaburi, mkazi wa Kisongo, amesema wamepoteza kila kitu kilichokuwamo kwenye nyumba yao.

Tatu ambaye alikuwa ndani ya nyumba pamoja na mume wake na mtoto, amesema wakati mvua inaendelea kunyesha walishtuka maji yanaingia ndani kwa nguvu.

“Tulichoshangaa ni maji yanaingia ndani kwa nguvu kwa sababu mvua iliyonyesha haikuwa kubwa, hatukujua itakua na madhara kiasi hicho, kwa hiyo baada ya kuona hali hiyo,  tukaanza kutoa vitu baadhi ila tukaona yana kasi kubwa sana. Tulichofanya, tulijitahidi kufungua mlango kutoka ndani lakini ikashindikana, maji yalishafika katikati ya mlango.”

“Ikabidi turudi ndani tukapanda juu ya dari, nilikuwa mimi, mume wangu pamoja na mtoto na wifi yangu. Kila kitu ndani ya nyumba kilikuwa kinaelea huko nje, ilikuwa ni yowe tu, sisi tuliokolewa usiku, walikuja wakavunja bati tukatoka baada ya maji kupungua na tulipata hifadhi sehemu na ndiyo tumerudi sasa hivi, tumekuta hakuna kitu," ameongeza Tatu.

Kwa upande, Lydia Mollel, mkazi kijiji cha Ngorbob, amesema mtoto wake mwenye umri wa mwezi mmoja na nusu aliokolewa baada ya kurushwa juu ya bati ambapo ambapo aliokolewa baada ya mvua hiyo kukatika.

“Nilikuwa nimelala na mwanangu kidogo nikaona maji yameingia ndani nikaanza kupiga kelele watu wakaja, nikapiga yowe uwii mtoto wangu jamani anaelea na maji  na vitu vinaelea vyote kuanzia godoro kila kitu, nikaanza kupiga ukunga nisaidieni na mtoto nakufa."

“Kuna kaka anaitwa Omary, akamchukua mtoto maji yakiwa yamemfika shingoni akambeba kichwani akamrusha juu ya bati, akabebwa huko kisha akaja kunichukua mimi akanirusha ukuta wa pili na ndiyo nimeenda kumchukua mtoto kule ofisini, lakini ameanza kukohoa maana alikunywa maji machafu,"ameeleza

Hata hivyo, licha ya Mwananchi kushuhudia nyumba kadhaa zilizoathiriwa na mvua hiyo, watu wanane wanadaiwa kunusurika kifo baada ya kusombwa na mafuriko katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Arusha.

Mbali na watu hao, magari sita na mali mbalimbali zimeopolewa katika mafuriko hayo.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Arusha, Osward Manjejele amesema mvua hiyo imeleta madhara makubwa ikiwemo kuharibu mali, kubomoa nyumba na maduka sambamba na kuharibu bidhaa zilizokuwemo.

“Bado hatuna taarifa za undani, lakini hadi alfajiri, kikosi changu kimeweza kuokoa watu hao wanane na magari sita, lakini pia bidhaa mbalimbali za madukani hasa yaliyokuwa pembezoni yameharibika na kuta kubomolewa,” amesema Mwanjejele.