Hawa hapa waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano
Muktasari:
- Wanafunzi 131,986 wakiwamo wasichana 66,432 na wavulana 65,554 wenye sifa, wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za kidato cha tano.
Dodoma. Wahitimu 188,787 kati ya 197,426 waliofaulu mitihani ya kidato cha nne, wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na vyuo mbalimbali kwa mwaka 2024.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohamed Mchengerwa amesema hayo leo Alhamisi Mei 30, 2024 wakati akitangaza uchaguzi wa wanafunzi.
“Wanafunzi waliochaguliwa baada ya kukidhi vigezo wapo wenye mahitaji maalumu 812 na kupangiwa kujiunga na kidato cha tano katika shule mbalimbali nchini pamoja na vyuo vya kati katika fani mbalimbali,”amesema Mchengerwa.
Mchengerwa amesema wanafunzi 131,986 wakiwamo wasichana 66,432 na wavulana 65,554 wenye sifa, wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za kidato cha tano 622 zikiwamo shule mpya 82 zinazoanza mwaka huu wa 2024.
“Wanafunzi 1,462 wakiwamo wasichana 669 na wavulana 793 walipangwa katika shule za sekondari nane zinazopokea wanafunzi wenye ufaulu wa juu zaidi ambazo ni Kilakala, Mzumbe, Ilboru, Kisimiri, Msalato, Kibaha, Tabora Boys na Tabora Girls,”amesema Mchengerwa.
Pia, amesema wanafunzi 6,576 wakiwamo wasichana 3,449 na wavulana 3,127 wamepangwa katika shule za sekondari za kutwa za kidato cha tano.
Waziri huyo amesema wanafunzi 123,948 wakiwamo wasichana 62,636 na wavulana 61,312 wamepangiwa katika shule za sekondari za bweni za kitaifa za kidato cha tano.
Mchengerwa amesema wanafunzi 56,801 wakiwamo wasichana 17,332 na wavulana 39,469 wamepangiwa kujiunga kwenye kozi na fani mbalimbali za stashahada katika vyuo vya elimu ya ufundi vinavyosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).
Mchengerwa amesema wanafunzi 52,675 wakiwamo wasichana 15,717 na wavulana 37,158 wamechaguliwa kujiunga kwenye kozi mbalimbali zikiwamo za kilimo, ufugaji, utawala, biashara na zinginezo za stashahada katika vyuo elimu ya ufundi mbalimbali nchini.
Waziri huyo amebainisha kuwa muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa kidato cha tano utaanza Julai mosi mwaka huu na hivyo wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na kidato cha tano kwa mwaka, 2024 wanapaswa kuanza kuripoti shuleni kuanzia Juni 30, 2024.
Amesema mwisho wa kuripoti shuleni kwa wanafunzi hao ni Julai 14 mwaka huu.
Aidha, Mchengerwa amesema kwa wanafunzi waliopangwa kwenye vyuo vya elimu ya ufundi watapokea maelekezo ya namna ya kujiunga kutoka katika vyuo walivyopangwa.
“Uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi zilizopo katika shule, hivyo hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule kutokana na ukosefu wa nafasi,”amesema.
Amesema orodha ya wanafunzi waliochaguliwa na fomu za kujiunga na kidato cha tano, vyuo vya elimu ya ufundi mwaka, 2024 inapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Rais -Tamisemi ya www.tamisemi.go.tz na Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi www.nactvet.go.tz.
Akizungumza na Mwananchi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, (Udom) Paul Loisulie amesema walikuwa wakiingia wachache kidato cha tano kwa kuwa shule zilikuwa ni chache.
Amesema wingi huo wa wanafunzi wanaoenda kidato cha tano, unamaanisha kuwa fursa zimeongezeka kwa sababu huwezi kuongeza idadi ya wanafunzi kama nafasi ni chache.
“Idadi kubwa hiyo ya uchaguzi wa wanafunzi inaonyesha kulegezwa kwa masharti ya ufaulu, kwa kadri nafasi zinapoongeza ndipo na masharti yanapunguzwa,”amesema.
Dk Loisulie amesema pia kuongezeka kwa idadi hiyo kunamanisha kuwa mwamko wa ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne umeongezeka.
Jumla ya watahiniwa walioandikishwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka, 2023 walikuwa ni 572,359 wakiwamo wasichana 310,248 (asilimia 54.21) na wavulana 262,111 (asilimia 45.79).
Kati yao watahiniwa wa shule waliosajiliwa walikuwa 543,332 wakiwamo wasichana 293,122 (asilimia 53.95) na wavulana 250,210 (asilimia 46.05).
Kwa mujibu wa Tamisemi, ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja, unaonesha kuwa watahiniwa 197,426 sawa na asilimia 37.42, walipata ufaulu wa daraja la I – III.
Hali inayoonesha kuwa ufaulu wa watahiniwa wa mwaka 2023 umeongezeka kwa asilimia 0.47 ikilinganishwa na ufaulu wa daraja la I – III wa watahiniwa 192,348 asilimia 36.95 wa mwaka 2022.