Majina ya wanafunzi waliochaguliwa kidato cha tano 2023 haya hapa

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(Tamisemi) Angelah Kairuki akizungumza na waandishi wa habari, leo Jumapili Juni 11, 2023 jijini Dodoma kuhusu uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano, vyuo vya fani mbalimbali kwa mwaka 2023.

Muktasari:

  • Waziri Kairuki amesema wanafunzi 1,878 wakiwemo wasichana 1,097 na wavulana 781 wamepangiwa katika shule za sekondari maalum nane ambazo ni Kilakala, Mzumbe, Ilboru, Kisimiri, Msalato, Kibaha, Tabora Boys na Tabora Girls.

Dodoma. Wanafunzi 188,128 waliokidhi vigezo wamechaguliwa na kupangiwa kujiunga na kidato cha tano katika shule mbalimbali nchini pamoja na vyuo vya fani mbalimbali.

Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022 yanaonyesha kuwa watahiniwa 192,348 walipata ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu ambapo kati yao Tanzania Bara walikuwa watahiniwa 188,128 wakiwemo wasichana 84,509 na wavulana 103,619.

Akizungumza na Waandishi wa Habari , leo Jumapili Juni 11, 2023 jijini hapa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angelah Kairuki amesema zoezi hilo limezingatia takwimu za matokeo ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022 kutoka Tanzania Bara.

Amesema wanafunzi waliochaguliwa ni kutoka katika shule za serikali, binafsi, watahiniwa wa kujitegemea, waliofanya mtihani chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.

Amesema wanafunzi 129,830 wakiwemo wasichana 66,343 na wavulana 63,487 sawa na asilimia 69 ya wenye sifa wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za kidato cha tano 540 zikiwemo shule mpya 29 zinazotarajiwa kuanza mwaka huu.

Waziri Kairuki amesema wanafunzi 1,878 wakiwemo wasichana 1,097 na wavulana 781 wamepangiwa katika shule za sekondari maalum nane ambazo ni Kilakala, Mzumbe, Ilboru, Kisimiri, Msalato, Kibaha, Tabora Boys na Tabora Girls.

Amesema wanafunzi 122,908 wakiwemo wasichana 62,731 na wavulana 60,177 wamepangiwa katika shule 519 za sekondari za bweni za kidato cha tano.

Waziri Kairuki amesema wanafunzi 5,044 wakiwemo wasichana 2,515 na wavulana 2,529 wamepangwa katika shule 11 za sekondari za kutwa za kidato cha tano.