Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haya ndiyo matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar

Muktasari:

  • Wadau wa siasa wanabainisha maendeleo kutoka visiwani humo wakati wakichambua maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi na namna mapinduzi hayo yalivyoleta matunda kwa wananchi

Uhuru wa kufanya wanachokitaka ili mradi hawavunji sheria ni moja ya matunda wanayojivunia Wazanzibari katika kipindi cha miaka 60 tangu kufanyika kwa Mapinduzi yaliyoung’oa utawala Sultani ulihudumu kwa miaka zaidi ya 100.

Pia, wanasema kuwepo kwa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa baina yao kunaendelea kuchochea ujenzi wa sera na dira ya maendeleo katika kuleta huduma muhimu za kustawisha afya za wananchi wa visiwa hivyo.

Wadau wa siasa wanabainisha na maendeleo kutoka visiwani humo wakati wakichambua maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi na namna mapinduzi hayo yalivyoleta matunda kwa wananchi.

“Kwa sasa tuna uhuru, hata kama una uwezo wa kujenga ghorofa au kufanya biashara ya aina yoyote utaifanya, huko nyuma maendeleo ya ujenzi wa nyumba yalikuwa yanabanwa kwa sheria lakini Mapinduzi yametoa uhuru kwa wananchi kujiendeleza kwa kadri wanavyojiweza,” anasema Ali Makame, mchambuzi wa siasa za Zanzibar.

Makame anasema mfumo wa elimu wa Zanzibar umewezesha kuwa na wasomi wengi wa elimu ya juu kama maprofesa na madaktari ukilinganisha na idadi ya watu waliopo huku akieleza kwamba wanaweza kupishana kidogo na Tanzania Bara.

“Zamani hakukuwa na Chuo Kikuu Zanzibar, lakini leo tuna vyuo vikuu zaidi ya vitano, tunashukuru kumekuwa kukijengewa vyuo, jambo ninaloweza kusema kwenye elimu tumefanikiwa kiasi,” anasema.

Kwenye sekta ya afya, Makame anasema zamani walikuwa nyuma na walikuwa wanatembea hadi vijiji vinne lakini hakuna zahanati lakini sasa mfumo wa afya unazidi kuboreshwa na kuimarishwa kwa kuwekwa vifaa na wataalamu wanazidi kuongezeka kulinda afya za raia.

“Huduma za kijamii masuala ya barabara, umeme, maji, zamani watu wakiona mfereji wanafurahi na kuona bomba ilikuwa ajabu lakini kwa sasa asilimia kubwa wanatumia maji ya bomba ambayo ni safi na salama,” anasema.

Mchambuzi huyo anasema hata wakulima kwa sasa katika visiwa hivyo wanapelekewa huduma za umeme na jambo lingine anasema ni ustawi wa amani kisiasa ni ishara kwamba kadiri muda unavyokwenda Wazanzibar watazidi kuelewana.

Anasema katika kila wilaya kumejengwa hospitali kubwa na zina uwezo wa kulaza wagonjwa 200 kwa wakati mmoja lakini zina vifaa vyote vya kisasa, X-Ray, CT Scans na katika hospitali hizo daktari yeyote bingwa duniani anaweza kufanya shughuli ya opereshini yeyote.

“Kumeimarishwa vituo vya afya maeneo mbalimbali hakuna raia anayetembea kilomita tatu bila kukuta kituo cha kutoa huduma za kiafya,” anasema.


CCM yajivunia mafanikio

Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Idara ya Itikadi na Uenezi  Zanzibar, Khamis Mbeto anasema Serikali imejitahidi kuleta maendeleo katika kipindi cha miaka 60 baada ya Mapinduzi.  

“Zimepita awamu saba, kila awamu ilifanya maendeleo kulingana na wakati wake. Sekta za kijamii zimeendelezwa vya kutosha ikiwamo sekta ya elimu kwa kujenga miundombinu ya majengo, vifaa vya kufundishia na ajira nyingi za walimu zimetolewa,” anasema.

Anatolea mfano ndani ya kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nane, zimejenga shule za maghorofa 21 lakini hawajamalizia ujenzi wa maghorofa tisa, kwa hiyo zaidi ya maghorofa 30 yamejengwa katika kuboresha sekta ya elimu.

“Serikali imeboresha vitendea kazi shuleni kwa maana ya maabara, maktaba na kuna madarasa ya Tehama kwa shule za msingi na sekondari, shule za bweni zimejengwa mikoa mbalimbali ikiwamo Mkoa wa Kazikazini Unguja na Pemba na kumejengwa vituo vya walimu kila wilaya,” anasema.

Mbeto anasema barabara zimekuwa zikiboreshwa kwa awamu zote hususani Serikali ya awamu ya nane, jumla ya kilomita 480 katika hizo, kilomita 275 inajumuisha barabara za ndani lakini kilomita 279 zinaunganisha barabara kubwa.

“Kuna barabara kubwa nne, kati yake kuna moja inaelekea Makunduchi na Kizimkazi lakini pia bado tuna mpango wa kujenga barabara zote za mrisho na kubwa, lengo likiwa ni kurahishisha shughuli za uzalishaji,” anasema.

Mbeto anasema wanajenga uwanja wa ndege wa Pemba utakaokuwa urefu wa mita 250 utakaokuwa na uwezo wa kutua ndege kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 350.

“Tunajenga Bandari ya Wete na tutajenga nyingine ya makontena lakini tutajenga bandari kubwa maeneo ya Mangapwani,”anasema

Kiongozi huyo wa CCM anasema wazee wanaofikisha kuanzia umri wa miaka 70 bila kujali hakuitumikia Serikali katika ngazi yoyote wote wanapokea Sh50,000 kila mwezi.

“Wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70, wanapokea Sh50,000 kila mwezi na hii inaonesha Serikali zote zinawajali wazee waliolitumikia Taifa lao kwa muda mrefu,” anasema.

Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid anasema watu waliunganishwa kwa kutumia  Kiswahili na kuna vijana wengi walisomeshwa kuja kuongoza nchi yao.

“Vilevile, elimu imekuwa ikitolewa bure, haya ndiyo matunda ya Mapinduzi” anasema Mbeto.


Matarajio yao

Makame anaiomba CCM, chama kinachoongoza Serikali zote mbili, kuangalia sera yake na kuifanya Zanzibar kuwa kitovu kikuu cha utalii huku akieleza raia wake hawafiki milioni tatu ikiwa watakuja na mkakati mzuri inaweza kujiingizia kipata kikubwa.

“Zanzibar imekuwa ikikusanya mapato mengi lakini mifumo yake haijaimarishwa kuna mianya mingi kiasi kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inashindwa kukusanya kiwango kikubwa zaidi,” anasema.

Anasema bajeti inayoweza kutumika kuimarisha mkoa mmoja Tanzania Bara ikielekezwa Zanzibar wanaweza kuvuna mapato makubwa zaidi lakini sura ya nchi kwa jumla itaonekana kwa kulifanya eneo hilo kuwa kubwa kwa maendeleo ya uchumi.

Anaeleza kuwa bado hali ya maisha kwa Wazanzibar wengi hairidhishi ni jambo linalopaswa kuwekewa msukumo mkubwa gharama ya maisha imekuwa ikipanda kutokana na mfumuko wa bei ya vyakula madukuni.

“Jingine ninalolipigia kelele mara kwa mara mfumo wetu wa elimu haujakaa sawa tume inapaswa kuundwa kupitia upya tumekubali hata kukatwa kwa tozo ila taratibu ziwe wazi mwanafunzi anakwenda shule bure si bure kwa kutukata kupitia tozo watengeneze mpango kuimarisha elimu,” anasema.

Makame anaiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufikiria kuunda tume itakayofanya shughuli zake kwa kupitia kipindi chote tangu mapinduzi yamefanyika kimekosekana kitu gani na mambo yanayopaswa kuboreshwa.

“Jambo hilo likifanyika litawaleta pamoja wananchi kwa sababu hadi sasa kuna baadhi ya watu wanayazungumza vibaya Mapinduzi hayo tunapaswa kujiuliza na kuweka mkakati wakulimaza kwa kuwasikiliza Wazanzibar wenyewe wanachohitaji,” anasema.