Ujenzi wa miundombinu fahari ya Zanzibar

Baadhi wa wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi wakiongozwa na Naibu Waziri wa elimu Abdulgulam Hussein, katika ziara kukagua shughuli za maenedeleo Kisiwani Pemba. Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

  • Mwenyekiti Kamati ya Ustawi wa Jamii Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Sabiha Filfil Thani amesema miundombinu mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa shule mpya za kisasa Unguja na Pemba ni kielelezo tosha kwa wananchi kufaidi matunda ya Serikali yao.

Pemba. Mwenyekiti Kamati ya Ustawi wa Jamii Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Sabiha Filfil Thani amesema miundombinu mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa shule mpya za kisasa Unguja na Pemba ni kielelezo tosha kwa wananchi kufaidi matunda ya Serikali yao.

Amesema hayo leo Novemba 8, 2023 wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya Wizara ya elimu kisiwani humo akiambana na wajumbe wa kamati hiyo na baadhi ya maofisa kisiwani humo.

Amesema Serikali ya awamu ya nane inafanya hivyo ili kuhakikisha kila huduma inapatikana maeneo yote ya karibu na wananchi.

Katika hatua nyingine kamati hiyo imeitaka wizara kuhakikisha wanajenga uzio katika eneo la Chuo Kikuu cha Taifa Suza Tawi la Pemba ili kiweze kuwa katika mazingira salama zaidi.


Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Abdulgulam Hussein amesema mradi wa ujenzi wa madarasa 1,000 katika maeneo tofauti umeanza mwezi Juni mwaka huu ambapo ni mategemeo ya wizara kuizindua baadhi ya madarasa hayo Januari mwakani yakiwa yamekamilika.

Pia, amesema kuna uwezekano wa baadhi ya madarasa kuchelewa kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza.

Mkandarasi kutoka Kampuni ya SINIC, Hawa Natepe amesema mradi wa Shule ya Sekondari Kiuyu Maziwang'ombe upo katika asilimia 90 na kutokana na kasi kubwa ya kazi anategemea kuukabidhisha mradi huo Desemba mwaka huu.

Kamati hiyo ya Ustawi wa Jamii Baraza la Wawakilishi Zanzibar imetembelea miradi tofauti inayosimamiwa na Wizara ya Elimu ukiwemo mradi wa ujenzi wa Skuli ya Ghorofa Maziwang'ombe, ukarabati wa Skuli ya Chwaka Tumbe na maendeleo ya Chuo Kikuu cha Taifa (Suza) tawi la Mchangamdogo Mkoa wa Kaskazini Pemba.