Hekta takribani 469,000 ya ardhi huharibiwa kila mwaka

Muktasari:


  • Tanzania inatarajia kurejesha uoto wa asili katika ardhi takribani hekta milioni 5.2 ifikapo 2030

Dar es Salaam. Hekta takribani 469,000 ya ardhi huharibiwa kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo shughuli za binaadamu zinazosababisha uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mhifadhi Mkuu kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Juma Mwangi katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wanaohusika na masuala ya uongoaji (urejeshaji) wa ardhi iliyoharibika nchini ili kujadili ni namna gani Tanzania inaweza kufikia malengo yake ya kuongoa ardhi kwa kurejesha uoto wa asili takribani hekta milioni 5.2 ifikapo 2030.

Mwangi amesema baadhi ya shughuli zinazopelea uharibifu huo ni pamoja na ufugaji wa mifugo mingi katika eneo moja, uharibifu wa vyanzo vya maji pamoja na ukataji wa misitu kwa ajili ya nishati uanzishaji wa mashamba pamoja na makazi.

Amesema maeneo hayo yaliyoaribika yanatoa fursa kwa sekta binafsi kuwekeza na kuweka mkakati mbadala wa wanachi waliopo katika eneo husika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania,  Revocatus Mushumbusi amesema maeneo ambayo yamekuwa yakisumbuliwa sana na changamoto ya ukame haswa mikoa ya kati ndiyo yameathirika zaidi na uharibifu wa mazingira ambao unasababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi pamoja na shughuli za kibinadamu.

Amesema ili kufikia hatua hiyo wamekuwa wakitoa elimu kwa wadau pamoja na wananchi juu ya umuhimu wa urejeshaji wa wa ardhi iliyoharibika pamoja na mbinu za kutumia ili kuhakikisha urejeshwaji wa ardhi unafanikiwa kwa kiwango kinachoridhisha.

“Kurejesha uoto wa asili hauhusishi upandaji wa miti peke yake hata utumiaji wa rasilimali zilizopo kwa njia iliyo endelevu pamoja na kuacha maeneo yaliyoharibika kurejesha yenyewe uoto wake wa asili ni baadhi ya mbinu nyingine zinazoweza kutumika kufanikisha hilo”alisema.

Hata hivyo amesema katika mapambano ya kufikia lengo la urejesha uoto wa asilili katika ardhi iliyoharibika wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo shughuli za kilimo cha kuhamahama ambazo zimekuwa zikifanyika katika baadhi ya maeneo.

“Watu wengi wanaamini kwamba wakilima katika maeneo ya misitu huwa yana rutuba ya kutosha ambayo inaweza kufanya mazao mengi”.

Nae Mkurugenzi wa Miradi kutoka Lead Foundation, Njamasi Chiwanga amesema wao kama sekta binafsi wamekuwa wakishirikiana na serikali katika kuweka mikakati mbalimbali ili kufikia lengo lililowekwa na nchi ifikapo 2030.

Amesema utekelezaji wa miradi inayolenga kurejesha uoto wa asili katika aridhi imekuwa ikifanyika kwa ushirikiano wa karibu na viongozi wa serikali za mitaa.

“Katika kila miradi ambayo tumeanza kutekeleza huwa tunakusanya taarifa na kuzikusanya kwa TFS ili kuziweka katika rekodi zao”aliongeza.