Helikopta kusaka simba waliovamia vijiji

Iringa.  Helikopta imeanza kutumika katika kutafuta simba waliovamia vijiji mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.

Hatua hiyo imekuja baada ya jitihada za awali za kuwasaka wanyama hao kugonga mwamba huku mifugo ikiendelea kuteketea.

Mpaka sasa zaidi ya ng'ombe 16, nguruwe na kuku wameuwawa huku hofu ikisambaa miongoni mwa wananchi hasa katika maeneo ya Kiponzelo, Maboga na Tanangozi.

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Veronika Kessy amesema wameanza kutumia helkopta kuwatafuta wanyama hao.

Amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ili kukabiliana na simba ambao bado wanasakwa.

Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Godwell Ole Meing'ataki, amesema matumizi ya helkopta yanaweza kuwa njia muhimu ya kuboresha uwezo wa kufuatilia na kudhibiti mienendo ya Simba.

Amesema helikopta itawasaidia maafisa wa uhifadhi kufika kwenye maeneo ambayo hayafikiki.

"Tunatarajia kutumia helkopta na tumehamishia kambi ya askari wa Wanyama pori tupo hapa katika kijiji cha Tanangozi hivyo tutaanzia hapa," amesema Ole Meing'ataki.

Baadhi ya wananchi wa vijiji walikovamiwa na simba wamesema hali ya hofu imetanda kwenye maeneo yao huku maombi ikiwa ni kuhakikisha wanapatikana.