Helikopta mbili zasindikiza mwili wa Membe

Mwili wa marehemu Bernard Membe ukishushwa katika helikopta iliyousafirisha kutoka jijini Dar es Salaam. Leo Jumatatu Mei 15, 2025

Rondo. Helikopta mbili za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ndizo zimetumika kuusafirisha mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe kutoka jijini Dar es Salaam hadi Kijiji cha Rondo kilichopo Kata ya Chiponda.

Moja ya helikopta hizo zilibeba mwili wa marehemu Membe, mkewe, watoto pamoja na askari wa JWTZ.

Helikopta nyingine iliwabeba ndugu wengine na baadhi ya viongozi akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela.

Helikopta hizo zilizotua katika uwanja uliopo pembeni ya nyumba ya Membe zilianza kuonekana katika anga za kijiji hicho saa 6:40 mchana na milio yake ilisababisha baadhi ya watu waanze kuangua kilio kutokana na taarifa walizopata kuwa mwili wa mpendwa wao utawasili kwa helikopta.

Helikopta iliyobeba ndugu ndiyo iliyokuwa ya kwanza kutua katika eneo hilo ambalo tayari watu walijitokeza kuupokea mwili huo.

Hata hivyo ndugu hao hawakushuka mpaka ilipofika helikopta ya pili iliyobeba mwili huo ambayo ilipishana kwa takribani dakika 7

Baada ya kutua kwa helikopta yenye mwili zilipata dakika 3 za kusubiri itulie na izimwe kwa ajili ya watu kushuka na mwili kushushwa.

Mwili wa Membe ulishushwa saa 7:01 mchana baada ya mke wa marehemu kushuka. Vijana kwa kushirikiana na wanajeshi wa JWTZ walianza kushusha mwili huo na kuuingizwa ndani ambako vilio vilianza kusikika baada ya watu kuona sanduku lililokuwa na mwili wa Membe.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ndiye aliwaongoza waombolezaji waliofika kijijini hapo kuupokea mwili huo na kuwataka wananchi wawe watulivu.

Amesema Membe alikuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Jimbo la Mtama ambalo yeye (Nape) ndiye alilirithi mikoba yake.

Amesema baada ya kuwasili mwili kutakuwa na ibada ya kumuombea marehemu na baada ya hapo familia itaendelea na taratibu nyingine.

Waziri Nape amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kesho ndiye ataiwakilisha Serikali kwenye mazishi hayo.

"Nawahakikishia wote watakaokuja kutoa heshima za mwisho kwa mpendwa wao watapata fursa hiyo. Tuwe watulivu wakati huu mgumu unaotukabili," amesema.

Steve Membe ambaye mdogo wa marehemu amesema kuwa taratibu zote zinakwenda vizuri ambapo baadae watakaa kikao cha kifamilia kuweka mikakati ya mwisho ya kumuhifadhi ndugu yao.

Membe alifariki dunia Mei 12, 2023 jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Kairuki alikokuwa akipatiwa matibabu kutokana na kushindwa kupumua.