HELSB yahitaji bilioni 800 kukopesha wanafunzi wote

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda akijibu hoja za wabunge kuhusu wanafunzi waliofaulu vizuri kukosa mikopo ya elimu ya juu wakati wa mkutano wa tisa, bungeni jijini Dodoma, Novemba 1, 2022. Kushoto ni naibu wake, Omary Kipanga

Muktasari:

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo amesema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, (HESLB), inahitaji Sh800 bilioni ili iweze kutoa mikopo kwa wanafunzi wote waliodahiliwa kujiunga na vyuo vikuu.

Dodoma. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo amesema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, (HESLB), inahitaji Sh800 bilioni ili iweze kutoa mikopo kwa wanafunzi wote waliodahiliwa kujiunga na vyuo vikuu.

 Nyongo ametoa kauli hiyo leo Jumanne Novemba Mosi, 2022 wakati akichangia hoja ya wanafunzi wa elimu ya juu kukosa mikopo iliyotolewa na Mbunge wa Biharamulo (CCM) Ezra Chiwelesa.

Amesema vigezo vinavyotumika kutoa mikopo vinavyoelezwa na HESLB, vinachanganya kwamba wanatoa mikopo kwa wanafunzi wasio na uwezo na yatima.

Amesema asilimia 62 ya mikopo inayotolewa na HESLB imekuwa ikitoa kwa wanafunzi waliosoma masomo ya sanaa (arts) ambao wakimaliza wanakwenda mtaani kwa sababu ya ukosefu wa ajira na hivyo kutorudisha mikopo.

Amesema asilimia 20 ya wadahiliwa wanaokwenda kusoma masomo ya sayansi na ndio waliopatiwa mikopo na asilimia tano japo hawakuomba.

Ametaka elimu itolewe kwa wazazi, kuwa mikopo hiyo inartolewa kwa wanafunzi, lakini watalazimika kuilipa watakapomaliza masomo yao.