Hesabu za mwisho uchaguzi Kenya

Muktasari:

  • Wakati zikisalia siku tatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, utafiti uliofanywa na kampuni ya Nation Media Group (NMG) unaonyesha kwenye jimbo la Nyanza mgombea urais wa Azimio la Umoja, Raila Odinga ana nafasi kubwa ya kushinda kwenye eneo, lakini bado mgombea huyo anaendelea kujiimarisha kwenye ukanda huo kwa kufanya kampeni za lala salama.


Nairobi. Wakati zikisalia siku tatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, utafiti uliofanywa na kampuni ya Nation Media Group (NMG) unaonyesha kwenye jimbo la Nyanza mgombea urais wa Azimio la Umoja, Raila Odinga ana nafasi kubwa ya kushinda kwenye eneo, lakini bado mgombea huyo anaendelea kujiimarisha kwenye ukanda huo kwa kufanya kampeni za lala salama.

Eneo hilo lenye Kaunti sita za Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii na Nyamira, lina wapiga kura 3.12 milioni ambao ni sawa na asilimia 14 ya wapiga kura wote nchini Kenya.

Hii inaweza kuwa mbinu ambayo Waziri Mkuu huyo mstaafu anaamua kuitumia ili kukusanya kura nyingi zitakazoamua matokeo kwenye uchaguzi huo ambao mshindi ni lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote.

Siku chache nyuma mgombea huyo kwa kushirikiana na mgombea mwenza wake, Martha Karua walifanya kampeni kwenye eneo la Mlima Kenya lenye wapiga kura wengi zaidi (asilimia 26) nchini humo na linakusanya Kaunti 10.

Ruto ajizatiti

Naibu Rais Wiliam Ruto ambaye kwa muda mrefu inaaminika anaungwa mkono kwa wingi na watu kutoka Mlima Kenya, amekuwa akirushiana maneno na vijembe na Rais Uhuru Kenyatta majukwaani.

Mpaka sasa wakati kampeni zikielekea ukingoni Ruto amefanya mambo matatu ambayo yanaweza kumbeba au kumuangusha kwenye uchaguzi huu.

Kwanza aliiburuza mahakamani mamlaka ya michezo nchini humo kwa kumnyima kufanya mkutano wake wa mwisho kwenye uwanja wa Taifa wa Nyayo na alishinda na kupewa kibali cha kufanya kampeni hiyo ya mwisho kwenye uwanja huo unaoingiza watu zaidi ya 45,000 kwa wakati mmoja.

Pili, mgombea huyo wa tiketi ya Kenya Kwanza ambaye pia ni kiongozi wa chama cha UDA, katika wakati huu wa lala salama ameitisha mkutano na waandishi wa habari kwenye makazi yake ya kiserikali huko Kareni na kumshutumu Rais Kenyatta kwa kukaa kikao cha siri kwa ajili ya kusababisha fujo na kumchafua siku ya uchaguzi.

“Muda sio mrefu Rais (Kenyatta) alikutana na watu Nakuru na matokeo ya mkutano huo si mazuri kwa nchi, ukiachana na mipango ya kuwadhuru na kuwatishia watu wa timu yangu, lakini pia wamepanga kusambaza vipeperushi na vijitabu vya kunichafua na kuwaonya wananchi wasinichague kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, kitu ambacho hakikubaliki,” alisema Ruto.

Lakini, mwisho ni kwamba Ruto mara nyingi akisimama kwenye majukwaa anarusha vijembe kwa Rais Uhuru Kenyatta, huku akihakikisha anaweka ushawishi miongoni mwa wananchi ili avune kura nyingi kupitia sababu hiyo.

Hata hivyo, Rais Kenyatta amekuwa akipuuza madai ya Ruto na kumtaka asake kura bila kuwadanganya Wakenya.

Odinga amtetea Kenyatta

Huku Ruto akiendelea kurushiana vijembe na Rais Kenyatta, Mgombea wa tiketi ya Azimio la Umoja, Raila Odinga yeye ameonyesha waziwazi kumkingia kifua Kenyatta na kumtaka mgombea mwenzake asimwongelee mtu anayeenda kupumzika.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Kisumu, kiongozi huyo wa ODM alimuonya mshindani wake na mgombea wa UDA, William Ruto dhidi ya kumshambulia Rais Kenyatta.

“Kwa kuwa Rais Kenyatta anaenda nyumbani (anamaliza muda wake), anapaswa kuachwa astaafu kwa amani. Ikiwa una tatizo basi inatakiwa unikabili mimi na Martha Karua kwa uwazi,” alisema.

Wagombea wenza

Kwenye kumtafuta mshindi wa nafasi ya urais kwenye siasa za Kenya huwezi kuuacha ukabila nyuma, huku kabila maarufu na lenye nguvu na wapiga kura wengi likiwa la Wakikuyu wanaopatikana upande wa Mlima Kenya, kwenye uchaguzi huu limetoa wagombea wenza wawili maarufu (Martha Karua na Rigathi Gachagua). Wote wameteuliwa na wagombea wao kwa lengo la kukusanya kura za upande huo maarufu wenye wapiga kura zaidi ya milioni 5.

Wajackoyah aponda

Wakati matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanywa nchini Kenya yakionyesha kuwa mgombea wa urais kupitia Chama cha Roots, George Wajackoyah akiwa nafasi ya tatu, yeye amepinga tafiti hizo.

Akiwa katika mkutano wake wa kampeni za lala salama kwenye mji wa Nanyuki, alisema kuwa matokeo ya tafiti hizo hayana maana kwa kuwa yeye anakubalika zaidi kuliko hao walioonekana kuongoza.

Alisema ana uungwaji mkubwa kutoka kwa vijana na anaamini atafanya vizuri.