Hifadhi milima Mahale kuongeza watalii
Kigoma. Kukamilika kwa ujenzi wa kiwango cha changarawe barabara Buhingu – Mahale yenye urefu wa kilometa 22, kuna tarajiwa kuwa chachu ya kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi ya Taifa ya Milima Mahale kuongeza.
Hayo yameelezwa na mkuu wa hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Susuma Kusekwa wakati wa makabidhiano ya kuanza ujenzi huo baina ya serikali na mkandarasi, ambapo Sh850 milioni zitatumika.
“Ujenzi wa barabara ya Buhingu kuelekea hifadhi ya taifa ya Milima Mahale itachangia ongezeko la watalii wanaotumia barabara kwa kuwa awali hawakuwepo kutokana na ukosekanaji wa miundombinu ya barabara inayofika katika hifadhi,” amesema Kasekwa.
Kusekwa amesema awali watalii walikua wanatumia usafiri wa anga na maji kupitia meli ya MV Liemba ambayo kwa sasa ipo katika matengenezo jambo ambalo linawafanya watalii wa njia ya barabara kushindwa kufika Mahale na kupunguza idadi ya watalii katika hifadhi hiyo.
Sambamba na hilo ujenzi wa barabara hiyo utasaidia jamii kupata barabara bora itakayorahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa ndani na nje ya hifadhi, hivyo kuimarika kichumi.
Akizingumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo meneja Tarura Mkoa Muhandisi Godwin Mpinzile amesema, serikali imetoa fedha hizo kwa lengo la kurahisisha miundomindu hiyo ili kurahisisha shughuli za kimaendeleo.
Mpinzile ametoa wito kwa viongozi wa vijiji vya Mugambo, Buhingu, Nkonkwa, Katumbi na Kalilani kutoa elimu kwa wananchi kutoa ushirikiano wakati wa utelekelezaji wa mradi huo kwa kuwa kuna upanuzi pande zote mita 40.
"Kutakua na upanuzi wa kushoto na kulia mita 20 kwa 20, kutakua na kuchimba chini na juu hasa katika huduma za jamii kama kupitisha mabomba ya maji na nguzo za umeme, wananchi watumie wataalam katika shughuli hizo ili kulinda barabara hii," alieleza Mpizile.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi mtendaji wa kijiji cha Buhingu Saidi Mkallah amesema, wamekuwa wakitumia masaa takribani nane kufika Kigoma mjini kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao jambo ambalo linawagharimu kwani msafiri atatakiwa kuwa na zaidi Sh50, 000 kwa safari moja.