Utafiti wataja dhana ya ‘kufikiri nje ya boksi; kuboresha elimu
Muktasari:
- Utafiti mpya uliofanywa na Vincent Lema, wenye jina la “Quality Education for Tanzania: ‘Think outside the Box’ in Preparing Teachers,” unakuja na mtazamo mpya kabisa unaotaka nchi itoke kwenye njia za mazoea.
Dar es Salaam. Kwa miaka mingi, mijadala kuhusu kushuka kwa ubora wa elimu nchini Tanzania imekuwa ikijirudia.
Wadau wamekuwa wakinyoshea vidole upungufu wa vitabu, madarasa, na mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala.
Hata hivyo, utafiti mpya uliofanywa na Vincent Lema, wenye jina la “Quality Education for Tanzania: ‘Think outside the Box’ in Preparing Teachers,” unakuja na mtazamo mpya kabisa unaotaka nchi itoke kwenye njia za mazoea.
Lema anabainisha kuwa, ingawa kazi nyingi za kitafiti zimeshaonyesha ukweli usiopingika kuhusu kuporomoka kwa ubora wa elimu na vyanzo vyake, suluhu zilizopo zimekuwa za zimamoto.
Katika andiko lake, anasisitiza kuwa mwalimu ndiye kiungo muhimu zaidi katika mfumo wa elimu rasmi.
Ili kuleta mabadiliko ya dhati, Lema anatoa mwito wa "kufikiri nje ya sanduku" (thinking outside the box) katika maandalizi ya walimu kupitia mambo makubwa matano:
Kujifunza kutoka elimu ya mkoloni
Kwa muda mrefu, mfumo wa elimu wa kikoloni umekuwa ukikosolewa kwa kuandaa watu wa kuwa "matarishi" au wafanyakazi wa ngazi za chini.
Hata hivyo, Lema anasisitiza kuwa kufikiri nje ya sanduku kunatutaka tuache kuangalia mabaya tu.
Badala yake, tuangalie ni kwa nini mfumo ule ulifanikiwa kuzalisha wahitimu wachache lakini waliokuwa na umahiri mkubwa wa lugha, hesabu, nidhamu, na maarifa ya vitendo.
Kuna mambo mazuri ya usimamizi na viwango tunaweza kuyachukua na kuyaboresha sasa.
Tutoke kwenye sera, twende kwenye vitendo
Tanzania haijawahi kuwa na upungufu wa sera nzuri za elimu. Tumekuwa tukibadili sera na miongozo kila muongo unapoisha, lakini mabadiliko hayo yanaishia kwenye makaratasi.
Utafiti huu unasisitiza kuwa suluhu ya ubora wa elimu haitapatikana kwa kutengeneza sera mpya kila siku, bali kwa kuweka nguvu na rasilimali katika utekelezaji wa dhati wa kile kilichopo, hasa katika ngazi ya darasani.
Walimu wote kuwa na shahada
Hili ni moja ya mapendekezo mazito na ya kijasiri katika utafiti huu. Lema anashauri kuwa Tanzania inapaswa kwenda mbali zaidi ya kanuni na miongozo ya sasa ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
Anapendekeza kuwa, ili kuinua ubora wa elimu kutoka kwenye msingi kabisa, walimu wa ngazi zote (kuanzia chekechea, msingi, hadi sekondari) wanapaswa kuwa na kiwango cha elimu cha shahada ya kwanza.
Haikubaliki kuwa na walimu wenye sifa za chini katika ngazi za awali ambapo ndipo msingi wa mtoto unapojengwa.
Kuanzishwa kwa shahada ya uzamivu ya elimu
Ili kuleta hadhi na utaalamu wa hali ya juu katika ufundishaji, mtafiti anashauri kuanzishwa kwa programu maalumu za "Doctor of Education"
Programu hizi zisiwe za kinadharia tu kwa ajili ya kufundisha vyuo vikuu, bali ziwalenge walimu wa vitendo waliopo kwenye shule za chekechea, msingi, na sekondari.
Hii itazalisha mabingwa wa mbinu za kufundishia na viongozi wa shule watakaobadili mifumo ya ufundishaji kwa vitendo.
Wakufunzi wa walimu wawe zaidi ya wahadhiri
Lema anagusa eneo lingine muhimu: nani anayeandaa walimu wetu? Anajenga hoja kuwa kuwa "mwalimu wa wakufunzi wa walimu" (Teacher of Teacher Educators) ni zaidi ya kuwa tu mhadhiri wa chuo kikuu mwenye shahada kubwa.
Mtu anayeandaa walimu anahitaji kuwa na ujuzi wa ziada wa jinsi ya kuhamisha mbinu za ufundishaji, uzoefu wa darasani, na malezi ya kiualimu, na si tu kutoa mihadhara ya kinadharia vyuoni.
Mtazamo mpya
Utafiti wa Lema unadhihirisha kuwa hatuwezi kupata matokeo tofauti kama tutaendelea kutumia mbinu zile zile za miaka ya nyuma.
Ili Tanzania ifikie elimu bora inayozalisha wabunifu na watatuzi wa matatizo, ni lazima iwekeze kwa dhati katika mapinduzi ya elimu ya walimu.
Ni wakati sasa kwa wizara husika, vyuo vikuu, na mamlaka zinazohusika kukubali changamoto hii na kuanza "kufikiri nje ya sanduku" kabla hatujachelewa.