Hifadhi za misitu zitakavyochochea sekta ya utalii

Hifadhi za misitu zitakavyochochea sekta ya utalii

Muktasari:

Mpango wa Serikali kufikia watalii zaidi ya milioni nchini kati ya sasa na mwaka 2025, ukilenga kuhakikisha Taifa linaongeza mapato kupitia sekta hiyo ambayo nchi jirani – Kenya, imekuwa ikiingiza katika hifadhi zake Zaidi ya idadi hiyo ya watalii kwa mwaka.

Mpango wa Serikali kufikia watalii zaidi ya milioni nchini kati ya sasa na mwaka 2025, ukilenga kuhakikisha Taifa linaongeza mapato kupitia sekta hiyo ambayo nchi jirani – Kenya, imekuwa ikiingiza katika hifadhi zake Zaidi ya idadi hiyo ya watalii kwa mwaka.

Kenya, tofauti na Tanzania haina vivutio vivutio vingi vya utalii, badala yake imekuwa ikijivunia kutua fukwe zake za Pwani kama chanzo kikubwa cha utalii pamoja na hifadhi chache za wanyama.

Hata hivyo, Tanzania imesheheni ikiwa na hifadhi za wanyama, misitu, mambo ya kale, mila na desturi za makabila na malikale za aina mbalimbali – vivutio vilivyotapakaa katika kila kona ya nchi. Hivi ndivyo Serikali imepanga kuvitumia vichangie pato la Taifa.

Wakati vivutio vikiwa vingi na vya kila aina, upande wa misitu dhamira ya kuongeza pato kupitia utalii imewekewa mikakati kadhaa kuhakikisha inafanikiwa ndani ya kipindi cha mitano ijayo.

Katika hifadhi hizo, shughuli ya utalii inafanyika kwa watalii kuzuru maeneo mbalimbali ambako hukutana na watembeza wageni kuzungukia maeneo husika kama ilivyo katika Hifadhi za Taifa.

Wakati Hifadhi za Taifa zinahusisha uwapo wa wanyama wa aina mbalimbali, misitu na mandhari za kuvutia yakiwa chini ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), hifadhi za misitu zimewekwa chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Pamoja na shughuli za uhifadhi, TFS kwa kutumia misitu hiyo ina jukumu ya kuitumia kuingiza fedha serikalini kupitia shughuli za utalii, na kwa mkakati wa miaka mitano ijayo wakala huo umejikita katika kuhakikisha kuwa utalii unanawiri hifadhini.

Idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za misitu ya mazingira ya msili imeongezeka zaidi ya mara mbili kutoka watalii 2,277 mwaka 2015 hadi kufikia watalii 5,387 mwaka 2019.

Hata hivyo, naibu kamishna wa Mipango na Matumizi ya rasilimali wa TFS, anayeshughulikia Mipango na Matumizi ya Rasilimali, Mohamed Kilongo anasema katika kipindi cha miaka mitano ijayo wamejikita kuboresha vivutio katika baadhi ya misitu na maeneo ambayo wamekabidhiwa na serikali kuratibu uhifadhi wake.

“Katika mwaka ujao wa fedha tumetenga zaidi ya Sh3 bilioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu – kuweka barabara, njia za kupita watalii, nyumba za mapumziko kwa ajili ya watalii pamoja na matangazo,” anasema Kilongo.

Kilongo anasema wanakusudia kuboresha zaidi maeneo hayo kwa ajili ya kuvutia utalii wa ikolojia ambao ni aina ya utalii wa kisasa zaidi unaovutia watalii wa aina tofauti wakiwemo watafiti kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na utalii wa utamaduni.

Katika maeneo 20 tengefu ambayo TFS imekabidhiwa kuhakikisha yanalipa kupitia uhifadhi na utalii, maneoo manane yamo katika bajeti ya uboreshwaji mwaka ujao wa fedha.

Maeneo hayo ni Ziwa Duluti (Arusha), hifadhi za mazingira asili za Magamba (Lushoto) na Amani (Muhezo)-zote mkoani Tanga, Ngome Kongwe na Kaole (Bagamoyo), Pugu/Kazimbuzumbwi (Dar), Ziwa Ngosi (Rungwe), Maporomoko ya Kalambo na Eneo Tengefu la Hanang (Arusha).

Pamoja na uwekezaji unaofanywa na wakala huo, pia unakusudia kukaribisha wawekezaji binafsi ili kusaidiana na serikali kuhakikisha kwamba shughuli za utalii katika maeneo yaliyo chini yake zinakua.

Miongoni mwa maeneo ambayo wageni hupendelea kutembelea ni Hifadhi ya Mazingira ya Amani iliyopo Muheza mkoani Tanga, ambayo ina utajiri mkubwa wa vipepeo na vinyonga, pamoja na wanyama wadogo kama mbega.

Ni katika hifadhi hiyo, pia kuna maporomoko ya maji ambayo ni kivutio kwa wanaotembelea eneo hilo, sambamba na miti mikubwa ikiwamo inayotumiwa na wenyeji kwa shughuli za kimila na matambiko. “Watu wanakuja hapa kwa ajili ya kuangalia vitu vingi ambavyo vipo hapa, mfano mandhari haya ya juu ni kivutio tosha, vilevile kuna yale maporomoko ya maji na hata wanyama wadogo na mimea isiyopatikana kwingine,” anasema Joshua Said maarufu Side, mmoja wa vijana wanaofanya shughuli za kuongoza watalii katika msimu huo.

Hifadhi ya Mazingira Asili ya Magamba iliyopo Lushoto mkoani Tanga ni eneo jingine ambalo lina vivutio vingi ikiwamo miti na mimea isiyopatikana sehemu zingine, lililotumiwa na Wajerumani miaka mingi kujifichia, wanyama aina ya mbega, vinyonga na ndege wa aina mbalimbali na mandhari ya kuvutia.

Watalii wengi katika hifadhi hiyo ni wanafunzi pamoja na watafiti ambapo katika miaka ya karibuni umekuwa ukiwavutia wageni kutoka nchi mbalimbali zikiwamo za Ulaya – wengi wakiwa ni watafiti wa masuala ya mimea na misitu.

Mandhari ya msitu huo nyakati zote za majira ya mwaka, utulivu na mazingira vinavutia mtu kutumia siku nzima akizunguka kuangalia vivutio vilivyomo.

“Kuna vivutio vingi tu hapa, msitu wenyewe ulivyokaa ni kivutio tosha, lakini pia humo ndani ya huu msitu kuna vivutio vya mimea, wanyama na wadudu wa kila aina, mtu akifika atapenda kuangalia vitu vingi vilivyomo ndani,” anasema ofisa Utalii wa Hifadhi ya Mazingira Asili ya Magamba, Samiji Mlemba.

Imeandikwa na Kulwa Magwa,