Hii hapa kauli ya wadau ndege mpya ATCL

Muktasari:

  • ATCL imesema lengo lake ni kuunganisha Tanzania, na kwamba baadhi ya vituo wanavyoenda hivi sasa si kuwa vinawalipa bali kwa siku zijazo vitakuwa na faida kubwa.

Dar es Salaam. Wadau wa sekta za biashara na usafiri wa anga wamechambua hatua ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), kuongeza ndege nyingine wakisema italiwezesha kutoa huduma kwa ufanisi katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Wameeleza hayo leo Jumatano Machi 27, 2024 kwenye mjadala wa Mwananchi X Space uliokuwa na mada isemayo: “Kwa kiasi gani kununuliwa kwa ndege za ATCL kunapunguza changamoto katika usafiri wa anga nchini.”

Jana Jumatano Machi 26, 2024, ATCL iliongeza ndege nyingine mpya ya abiria aina ya Boeing B737-9 Max.

Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude amesema uwepo wa ndege nyingine ya ATCL unaongeza nguvu katika utendaji kazi wa shirika katika soko la ndani na nje ya nchi.

Amesema ingawa kuna watu watahoji inakuwaje kwenye taarifa za Serikali linapata hasara na linaongeza ndege.  

"Ni kweli mashirika mengi ya ndege yanajiendesha kihasara  kwa muda, baadaye yanapata faida. ATCL lipo katika hatua ya mwanzo baada ya kufufuliwa, ni kawaida kuanza kwa mwendo usiokuwa na faida kwa sababu linaingia kwenye soko.”

"Lakini tutarajie muda mfupi litaanza kupata faida, hatua ya kuongeza ndege ni mwanzo mzuri ili kujijenga na kutoa huduma kwa Watanzania," amesema Mkude.

Hata hivyo, Mkude amesema biashara ya usafiri wa ndege ina changamoto nyingi ukilinganisha na nyingine za usafirishaji, hivyo suala la kupata hasara ni kawaida wakati shirika likitafuta njia ya kujiweka vizuri.

Kuhusu changamoto, amesema bei ya mafuta ya ndege ambayo mashirika yanabeba ni mzigo mkubwa pale inapopanda katika gharama ya uendeshaji, pili hofu pale linapotokea tatizo akitoa mfano wa ajali.

Mhariri wa Jarida la Biashara la gazeti la Mwananchi, Ephraim Bahemu, amesema kuongeza ndege ni hatua nzuri kwa sababu hivi sasa shirika hilo ndilo linamiliki soko kwa asilimia kubwa, na kwamba kitendo cha kuongeza ndege linajiimarisha.

Amesema ATCL kwa kuwa na ndege linaweza kupanga safari na miruko mingi zaidi na huenda ikaondoa changamoto za malalamiko ya abiria waliokuwa wakilalamika safari kukatizwa au kuchelewa.

"Mara nyingi ndege zinanuliwa kimkakati, hasa kuunganisha Tanzania na mataifa ya Afrika, kama mipango itakuwa mizuri basi tutaona kila kitu kitabadilika. Kikubwa kuwa na mipango mizuri ya kibiashara ili kuleta tija kwenye sekta hii," amesema Bahemu.

TAZAMA NDEGE MPYA YA BOEING 737 MAX 9 YA ATCL ILIVYOPOKEWA

Mwandishi wa habari za biashara wa gazeti la The Citizen, Josephine Christopher amesema wakati ATCL inafufuliwa mwaka 2016 ilikuwa na abiria 100,000 kwa mujibu wa takwimu za Serikali hivi sasa linahudumia watu milioni moja.

"Maana yake mahitaji ya ndege kwa Tanzania yamezidi kuwa makubwa hasa kwa soko la ndani, hii inaonyesha watu wana mahitaji. Hii ni faida kwetu kwa ATCL kutoa huduma kwa Watanzania," amesema Josephine.

Mtaalamu wa sekta ya usafiri wa anga, Jimray Nangawe amesema ATCL linapaswa kujiimarisha kutokana na ushindani uliopo katika sekta ya usafiri wa anga kwa sasa.

Nangawe amesema shirika hilo linapaswa kusimama kidete na kuwa tayari kwa changamoto yoyote itakayojitokeza.

“Ili shirika liwe na ushindani lazima liwe na ndege nyingi mpya na za kisasa zaidi kama hii iliyokuja jana, na baada ya muda wataanza kutengeneza faida,” amesema Nangawe.


Alichosema Matindi

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema shirika hilo limefikisha vituo 15 vinavyotoa huduma zake katika soko la ndani.

Hatua hiyo amesema inatokana na uwezo wa taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake pasipo kuangalia faida.

Matindi amesema lengo la ATCL ni kuunganisha Tanzania, na kwamba baadhi ya vituo wanavyoenda hivi sasa si kuwa vinawalipa bali kwa siku zijazo vitakuwa na faida kubwa.

Amesema faida katika mashirika mengi ya ndege duniani ni ndogo si tu kwa ATCL.

Matindi amesema mchakato ni mrefu hadi kuanza kupata faida na suala hilo ni la kuangalia kwa umakini zaidi.

Amesema kwa hali ilivyo sasa vituo vingi vilivyopo nchini bado si vya kutengeneza faida na vingi vinaendeshwa kwa matumaini. Hivyo inahitaji muda hadi kuanza kutengeneza faida.

Kwa mujibu wa Matindi, soko la ndani limekua kwa kiasi kikubwa, hivyo suala la kununua ndege linaendana na mpango wa kibiashara.

"Soko la ndani limebadilisha fikra za Watanzania na mwonekano wa soko la anga, natumaini mwakani tutaongeza abiria wengi zaidi. Sikutarajia kama litakuwa hivi, tumejitahidi kuongeza ubunifu kwa kuangalia pato la Mtanzania," amesema.

Matindi amesema ili kupanua fursa zilizopo katika soko la ndani lazima kuwe na ndege, sambamba na kutoa huduma za uhakika, hivyo ununuzi wa ndege unamaliza changamoto ya usafiri.


Kuhusu changamoto

Kuhusu changamoto ya usafiri wa ndege, Matindi amesema ni kweli zipo kama vile bei za nauli, lakini kwa gharama za uendeshaji zinaendana na gharama za tiketi.

Amefafanua kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo wanachofanya ni kuweka mazingira ya Watanzania kupata tiketi kwa njia mbadala kama ‘kibubu’ inayotumiwa na familia mbalimbali katika kufanikisha kutumia usafiri huo nyakati za likizo.

Matindi amegusia hatua ya ndege kuchelewa akisema: "Ni kweli lakini ilitokana na ndege zetu tatu za Air Bus zenye ujazo wa kati kutokuwepo, zilikuwa zikitumika kikanda. Hata hivyo, tunaboresha kwa kuongeza uwezo wa ndege zetu.”