Faida za ndege mpya ya mizigo, wafanyabiashara kicheko

Dar es Salaam. Ndege mpya ya mizigo inayotarajiwa kuwasili kesho, inaelezwa kuwa itawapunguzia wafanyabiashara gharama za usafirishaji, hasa wa bidhaa za maua, mbogamboga, nyama na samaki kwa kuwa sasa hawatalazimika kwenda nje ya nchi kusafirisha mizigo yao.

Ndege hiyo aina ya Boeing 767 - 300F, inatarajiwa kutua nchini na kupokewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), ikiwa ni ndege ya kwanza ya mizigo kununuliwa na Serikali.

Akizungumzia ujio wa ndege hiyo jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema itarahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kwenda nje ya nchi.

"Ujio wa ndege hii utaleta unafuu kwa wafanyabiashara, hasa wa mbogamboga, maua, nyama, samaki na madini na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje na Serikali pamoja na wafanyabiashara, hususani wa dawa," alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Shirika la Ndege nchini (ATCL), Sarah Reuben alisema baada ya kuwasili nchini, ndege hiyo itaanza kutoa huduma Julai 2023 baada ya kukamilisha taratibu za usajili na vibali vingine.

Wakizungumzia ujio wa ndege hiyo, wadau wa sekta hizo wameipongeza Serikali kwa kununua ndege hiyo na kwamba itawasaidia kupata uhakika wa kusafirisha bidhaa zao kwa gharama nafuu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wakulima wa Mbogamboga na Matunda (Taha), Jacqueline Mkindi alisema kama ndege hiyo itakwenda kwenye masoko ya Ulaya wanakopeleka bidhaa za maua na mbogamboga, itakuwa ni nafuu kwa mazao yao yanayotegemea usafiri huo.

"Masoko ya horticulture (maua, mbogamboga na matunda) yanayotumia usafiri wa ndege yako Ulaya, kama ndege itakwenda Ulaya itakuwa na faida kubwa sana kwetu," alisema Mkindi.