Serikali kununua ndege tano mpya ATCL

Muktasari:

  • Serikali imetaja miradi 15 ya maendeleo itakayoendelea nao mwaka ujao wa fedha ikiwemo ununuzi wa ndege, ununuzi wa meli za wavuvi, uendelezaji wa sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia.

Dar es Salaam. Serikali imetaja miradi 15 ya maendeleo itakayoendelea nayo mwaka 2023/2024 ikiwemo kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kukamilisha manunuzi ya ndege tano mpya.

 Baadhi ya miradi mingine inayotekelezwa ni Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere – MW 2,115, Daraja la JPM - Kigongo – Busisi (Mwanza), ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania), Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi.

Hayo yameelezwa kupitia taarifa ya Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2023/2024 iliyotolewa na Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ndege moja ni aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, ndege mbili ni aina ya Boeing 737-9, ndege moja ya mizigo aina ya Boeing 767-300F na ndege moja (1) aina ya De Havilland Dash 8 Q400.

“Ndege moja aina ya Boeing 767-300F ya mizigo inatarajiwa kuwasili Machi 2023, ndege mbili aina ya Boeing 737-9 zitakawasili Julai 2023 na Oktoba 2023,” amesema.

“Pia ndege moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner itawasili Novemba, 2023 na ndege moja aina ya De Havilland Dash 8-Q400 inatarajiwa kuwasili Juni 2023,” inaeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeelezwa kuwa ukarabati na ununuzi wa vifaa vya karakana za matengenezo ya ndege (Hangar) za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) utafanyika.

“Pia tutakamilisha ujenzi wa hanga jipya la kisasa katika kiwanja cha JNIA, kugharamia mahitaji ya awali ya uendeshaji wa ndege tano ambazo ni boeing 787 – 8, Boeing 737- 9 mbili, Boeing 767 - 300F na Dash 8 Q400 moja, ununuzi wa vifaa vya kuhudumia ndege na abiria viwanjani,” imeeleza taarifa hiyo.

Pia imeelezwa kuwa ukarabati wa majengo ya ofisi ya ATCL makao makuu na lililopo Kiwanja cha Ndege cha JNIA Terminal I utafanyika.

Hilo litaenda sambamba na ukarabati wa nyumba 38 zilizopo KIA pamoja na ujenzi wa eneo la mafunzo ya awali kwa wanaanga, ununuzi wa ndege aina ya Boeing Business Jet 737 – 7, ujenzi na ukarabati wa majengo kwa ajili ya kuhifadhi mizigo katika viwanja vya ndege vya JNIA, KIA na Songwe.

Miradi mingine iliyotajwa katika mpango huo ni ule wa Kufua Umeme wa Maji wa Ruhudji (MW 358) na Rumakali (MW 222), Makaa ya mawe Mchuchuma yote iliyopo Njombe, Uendelezaji wa Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia,  Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi – Kilwa Masoko,  Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi na ununuzi wa meli za uvuvi.