Hii hapa mikakati kuongeza tija uzalishaji wa tumbaku

Dodoma. Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) imesema ili kufikia utekelezaji wa ajenda 10/30 inayolenga kukuza sekta ya kilimo kwa asilimia 10 hadi kufikia mwaka 2030 ni lazima wabadili fikra za wafanyakazi wao.

Hayo yamesemwa leo Novemba 13, 2023 mkoani Morogoro ambapo menejimenti na watumishi wa TTB wamejifungia kujadili njia za kuongeza tija.

Akizungumza kwenye mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Stanley Mnozya amewataka watumishi wa bodi hiyo kubadili fikra na kuwa na fikra za kufanyakazi kwa kuzingatia weledi na uadilifu ili kuendana na mwelekeo wa Wizara katika kukuza sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na zao la tumbaku.

“Tuache kufanya kazi kwa mazoea, na tuongeza ubunifu na uwajibikaji ili kuhakikisha zao linatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi,”amesema.

Aidha Mnozya amewahakikishia watumishi wa TTB kufanya kazi kwa kujiamini bila  woga kwani Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe yupo pamoja na watumishi wote watakaofanya kazi kwa kuzingatia miongozo na malengo ya Wizara ya Kilimo ili malengo yaweze kufikiwa.

Uzalishaji wa tumbaku katika msimu wa 2022/2023 umefikia tani 123,000 ikilinganishwa na tani 60,000 zilizozalishwa kwenye msimu wa 2021/22, kuongezeka kwa uzalishaji huo kumepelekea wakulima kulipwa zaidi ya Sh700 bilioni.

Mnozya  amesema iwapo matumizi bora ya pembejeo na uzingatiaji wa kanuni bora za kilimo cha tumbaku,  nchi inaweza kuzalisha zaidi ya tani 350,000 kwa mwaka  na kuongoza katika uzalishaji  Afrika, kuongeza kipato kwa wakulima na mapato ya fedha za kigeni na mapato ya ndani kupitia kodi  kwa nchi.