Hii ndiyo tofauti ya uchaguzi wa Uganda na wa Tanzania

Hii ndiyo tofauti ya uchaguzi wa Uganda na wa Tanzania

Muktasari:

Madai ya Tume huru ya uchaguzi, Katiba mpya, tuhuma za wapinzani kunyanyaswa na vyombo vya dola na idara za Serikali, umekuwa kama wimbo katika chaguzi za nchi za Kiafrika.

  

Madai ya Tume huru ya uchaguzi, Katiba mpya, tuhuma za wapinzani kunyanyaswa na vyombo vya dola na idara za Serikali, umekuwa kama wimbo katika chaguzi za nchi za Kiafrika.

Wachambuzi wa siasa nchini, wamegusia mifumo ya uchaguzi ya Afrika wakiutaja uchaguzi mkuu wa Uganda uliofanyika Januari 14 na wa Tanzania uliofanyika Oktoba 28.

“Chaguzi za Uganda na Tanzania hazina tofauti, labda tofauti pekee kwa Uganda, Rais Museveni ameendelea kuwa madarakani kwa muda mrefu, lakini Tanzania chama cha CCM ndiyo kimekaa madarakani kwa muda mrefu na wanaobadilika ni watu tu, lakini mbinu wanazotumia ni zilezile,” amesema Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO) Iringa alipozungumza na Mwananchi juu ya uchaguzi huo.

Uchaguzi wa Uganda

Kama ilivyotarajiwa na wengi katika uchaguzi mkuu wa nchi hii kuwa Yoweri Museveni ataibuka na ushindi, ndivyo ilivyotokea.

Museveni ameshinda uchaguzi huo baada ya kumshinda kwa mara nyingine mpinzani wake wa karibu, Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu ‘Bobi Wine.’

Matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Uganda, yameonyesha Museveni aliyegombea kupitia chama cha NRM, ndiye mshindi. Museven ameongoza nchi hiyo tangu mwaka 1986.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, alipata kura zaidi ya milioni 5.85 sawa na asilimia 58.64 kati ya kura milioni 10,359,479 zilizopigwa, huku Bobi Wine akipata kura milioni 3.47 sawa na asilimia 34.83.

Wananchi waliojitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Mpiga kura ni milioni 18,103,603.

Mbali na wagombea hao, kulikuwa na wagombea wengine nao ni Patrick Oboi Amuriat wa Chama cha Forum for Democratic Change.

Amuriat alipata asilimia 3.24 ya kura, Mugisha Muntu wa Alliance for National Transformation alipata asilimia 0.65, Nobert Mao wa Democratic Party alipata asilimia 0.56.

Tofauti na Tanzania, Katiba ya Uganda inaruhusu kuwa na wagombea huru na waliogombea safari kwa nafasi ya Urais ni pamoja na Henry Tumukunde, Joseph Kabuleta, Nancy Kalembe, John Katumba, Willy Mayambala na Fred Mwesigye.

Lakini pia Katiba ya nchi hiyo inaruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani jambo ambalo haliruhusiwi na Katiba ya Tanzania.


Mpambano wa kuwania nafsi ya Rais

Inaelezwa kuwa mchuano mkali ulikuwa kati ya Museveni na Bobi Wine ambaye aligombea nafasi ya Urais kwa mara ya kwanza.

Bobi Wine aliyegombea kwa tiketi ya Chama cha National Unity Platform, aliwahi kuwa mbunge huru. Pamoja na kugonga mwamba kwenye urais, lakini chama hicho kimepata zaidi ya wawakilishi 50 bungeni na hivyo kuwa chama kikuu cha upinzani dhidi ya NRM.

Hiyo ni tofauti na Tanzania, ambapo wapinzani wameambulia majimbo mawili tu ya ubunge licha ya kuwa walisimamisha wagombea kwenye majimbo yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.


Mlinganyo na Tanzania

Itakumbukwa kuwa uchaguzi wa Uganda umefanyika ikiwa ni miezi michache tangu Tanzania ilipofanya uchaguzi wake mkuu ambao, Rais John Magufuli wa CCM alishinda kwa kujizolea zaidi ya asilimia 84 ya kura zote zilizopigwa.

Mgombea aliyefuatia katika kinyang’anyiro hicho, alikuwa Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyepata zaidi ya asilimia 19.

Hivyo, chaguzi hizo mbili katika eneo la Afrika Mashariki, zimeibua kilio cha demokrasia kutoka kwa wapinzani wanaosema kuna haja ya kuwa na Tume huru za uchaguzi ambazo zitasaidia kumaliza makandokando wanaydai yanawanyima uongozi.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya vyama vya upinzani vya Tanzania, ndiyo hayo yametolewa na wapinzani wa Uganda.

Malalamiko hayo ni pamoja na matumizi ya vyombo vya dola hususan Jeshi la Polisi lililodaiwa kuwadhibiti wapinzani walipokuwa wakitaka kufanya kampeni zao.

Katika uchaguzi wa Uganda, tangu wakati wa kampeni, lawama za uwapo wa vurugu kubwa inadaiwa zilisababishwa na Jeshi la Polisi kutaka kuwadhibiti wapinzani wasifanye mikutano ya kampeni.

Hali hiyo inadaiwa kuwa ilichangia kwa kiwango kikubwa uwapo wa mauaji na kukamatwa kwa makada na viongozi wa upinzani waliodaiwa kukiuka masharti ya nch hiyo juu ya kujikinga na maambukizo ya Virusi vya corona kwa kuanzisa mikusanyiko.

Inaelezwa kuwa mikusanyiko nchini humo iliyokuwa imeruhusiwa kipindi chote cha kampeni, ni ile ambayo ilikuwa haizidi watu 200.

Kipindi chote cha kampeni, wagombea wa upinzani na wafuasi wao waliandamwa na maofisa usalama waliojihami kwa silaha. Mamia ya askari polisi na wanajeshi walikuwa wakiwafuatilia kila mahala walikokuwa wakifana mikutano yao na kuisambaratisha.

Lakini kwa Tanzania, malalamiko ya wapinzani kunyanyaswa na Polisi pia yalikuwepo.


Mtandao wa intaneti

Katika hali iliyoonyesha kukosekana kwa uwazi katika uchaguzi huo nchini Uganda, agizo la kuzimwa kwa mtandao wa intaneti lilitolewa na usiku wa kuamkia siku ya kupiga kura, ukazimwa.

Hali ya kukosekana kwa intaneti ilikuwapo pia nchini Tanzania siku ya uchaguzi mkuu. Lakini tofauti ya Tanzaia na Uganda ni kuwa, Tanzania hakuna kiongozi aliyesimama hadharani na kutoa agizo hilo.

Lakini kwa Uganda, agizo la kuzima intaneti lilitolewa na Rais Museveni baada ya mtandao wa Facebook kufunga akaunti za maofisa wa Serikali kwa madai ya kuchochea mjadala kuelekea uchaguzi mkuu.

Mchakato mzima wa uchaguzi huo wa Uganda pia ulilalamikiwa kuwa uliendeshwa kwa kificho bila kuwapo macho ya waangalizi wa kimataifa.

Kwa mfano, Umoja wa Ulaya ulikataa kupeleka waangalizi wake katika uchaguzi huo kwa sababu mapendekezo waliyotoa hayakutekelezwa.

Januari 13, Marekani ilizuia waangalizi wake ikisema umekosa uwazi na uwajibikaji.

Akizungumzia uchaguzi huo, mwanasheria mkongwe Profesa Abdallah Safari amesema chaguzi hizo hazikuwa tofauti kutokana na mfanano wa historia na matukio yaliyojitokeza. “Hakuna utofauti wowote, kwa sababu modus operand (njia za utekelezaji) ilikuwa ni ile ile. Pamoja na kuwepo kwa sheria ya kupinga matokeo ya urais bado inategemea kama mfumo wa mahakama una msimamo kiasi gani kama ule wa Kenya na Malawi.

Akizungumzia wagombea huru, Profesa Safari amesema ni suala lililojadiliwa tangu mwaka 1992 baada ya kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila.

“Hata Mwalimu (Julius) Nyerere aliunga mkono hukumu ya Jaji (Kahwa) Lugakingira iliyoelekeza kuwe na mgombea huru. Lakini baadaye jopo la majaji saba liliipinga,” amesema.

Maoni hayo yameungwa mkono na Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha Iringa (Ruco), akisema mfumo mzima wa uchaguzi wa Uganda una mambo yanayolalamikiwa kama ya Tanzania. “Mbinu wanazotumia ni zilezile; kwanza hawataki madai ya kuwa na tume huru, hawataki mabadiliko ya Katiba wala kuwa na mfumo huru wa mahakama,” anasema Profesa Mpangala.

Ameendelea kusema siyo kosa kwa chama kukaa madarakani kwa muda mrefu wala Rais kukaa madarakani kwa muda mrefu, bali ni kutokuruhusu utekelezwaji wa demokrasia ya kweli.

“Kinachotakiwa ni kuruhusu wananchi waamue, lakini kinachofanyika sasa ni kupunguza nguvu ya wapinzani kwa kulitumia Jeshi la Polisi na kukosekana kwa tume huru ya uchaguzi,” anasema.

Anasema ili kuzifanya nchi hizi ziwe huru na kusiwe na manung’uniko toka kwa wau au wafuasi wa vyama vya upinzani na viongozi wao, ni kuruhusu demokrasia ya kweli ifanyike, badla ya ‘funika kombe mwanaharamu apite’.