Hilda avunja rekodi ya kupika kwa saa 100 bila kupumzika


Muktasari:

  • Hilda anakuwa mwanamke wa pili kushika rekodi hiyo ya dunia ya kupika kwa saa nyingi bila ya kupumzika.

Dar es Salaam. Binti wa miaka 27 ambaye ni moja kati ya wapishi mashuhuri nchini Nigeria, Hilda Bassey maarufu kama Hilda Basi amevunja rekodi ya dunia ya ‘Guinness’ kwa kupika kwa saa 100 bila kupumzika.

Rekodi hizo zilizovunjwa na Hilda zilikuwa zikishikiliwa na Lata Tondon kutoka nchini India mwaka 2019 ambaye alitumia saa 87 na dakika 45 kupika na kufanikiwa kuweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika rekodi hiyo ya kupika kwa muda mrefu kupitia shindano la 'Longest Cooking Marathon'.

Guinness Word Record kupitia ukurasa wao wa Twitter wamesema wana taarifa juu ya rekodi hiyo iliyowekwa, hata hivyo wanahitaji kupitia vielelezo vyote ili kujiridhisha.

Safari ya kuvunja rekodi hiyo ya Hilda ilianza Alhamisi ya wiki iliyopita katika mgahawa mmoja uliopo eneo la Lekki jijini Lagos nchini Nigeria na ilipofika jana Mei 15, 2023 saa 1:45 asubuhi alifaniliwa kuvunja rekodi hiyo iliyowekwa na mtangulizi wake kutoka India.

Hata hivyo, Hilda aliendelea kuipalilia rekodi yake kwa kuendelea kupika hadi ilipofika saa 1:45 kwa saa za Afrika Magharibi ambapo alifikisha saa 100 akiwa anapika japokuwa kwa mujibu wa shindano hilo Hilda alitakiwa kupika kwa siku 4 mfululizo (saa 96) bila kupumzika.

Baadhi ya vitu ambavyo alitakiwa kuzingatia kwenye shindano hilo ni kama ni kusimama wakati anapika, kutotumia kahawa au kinywaji chochote cha kumuongezea nguvu kama (energy drinks).

Pia aliruhusiwa kunywa, kula na kutumia glucose, siku nne bila kulala kabisa na kupatiwa dakika 5 za kupumzika kwa kila saa kwa ajili ya kuchuliwa misuli.

Katika kufikia rekodi yake hiyo wakati mwingine alionekana kutaka kukata tamaa lakini mamia ya watu waliokuwa nje ya mgahawa huo wakimshangilia walimpa moyo wa kuendelelea.

Kwa mujibu wa tovuti ya ‘The Guardian Nigeria’ Hilda kupitia rekodi hiyo aliyoweka amepatiwa zawadi ya fedha dola za kimarekani 5,000 (Sh11.5 milioni).