Prime
Hisabati mwiba, robo tatu ya watahimiwa wapata alama F
Muktasari:
- Matokeo yaliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Januari 31, 2026 yanaonesha kuwa kati ya shule 5,843 zilizokuwa na matokeo katika mtihani huo, 2,908 zilipata daraja D na F, huku zinazobakia zikiwa katika daraja A hadi C.
Dar es Salaam. Wakati takribani nusu ya shule za sekondari nchini zimepata wastani dhaifu na sifuri katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2025, mitihani ya somo la hisabati, baiolojia na book keeping bado ni mwiba kwa wanafunzi.
Hii ni kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) Januari 31, 2026, kupitia Katibu Mtendaji wake, Profesa Said Mohammed.
Matokeo hayo yanaonesha kuwa kati ya shule 5,843 zilizokuwa na matokeo katika mtihani huo, 2,908 zilipata daraja D na F, huku zinazobaki zikiwa katika daraja A hadi C.
Shule hizo ni pungufu ikilinganishwa na zile 3,069 zilizokuwa na wastani wa D na F katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka uliotangulia.
Licha ya shule zinazopata wastani dhaifu na mbaya kupungua, wanafunzi wameendelea kusota kupata ufaulu mzuri katika masomo ya hisabati, baiolojia na book keeping.
Hiyo ni baada ya ufaulu katika masomo hayo kuendelea kushuka, huku wadau wakielezea sababu zinazochochea hali hiyo.
Masomo yenye ufaulu dhaifu
Takwimu zinaonesha kuwa katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2025, asilimia 73.55 ya watahiniwa katika somo la hisabati wamepata daraja F, huku waliopata daraja A hadi C wakiwa asilimia 15.86. Idadi ya waliopata F wakijumlishwa na waliopata D wanafikia asilimia 84.17.
Idadi ya waliopata A hadi C katika mtihani wa kidato cha nne kwa somo la hisabati ni ongezeko kutoka asilimia 11.71 mwaka 2024 na asilimia 12.75 iliyokuwapo mwaka 2023.
Kwa upande wa somo la baiolojia, asilimia 34.32 wamepata daraja F, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 25.85 iliyokuwapo mwaka 2024, huku katika somo la book keeping waliopata F wakiongezeka hadi asilimia 25.75 mwaka jana kutoka asilimia 11.73 mwaka uliotangulia.
Mwalimu wa masomo ya hisabati na fizikia katika vituo mbalimbali vya kufundishia mkoani Arusha, Paul Saileku, anasema kutofanya vizuri kwa wanafunzi wengi katika somo la hesabu kunasababishwa na wanafunzi kutoandaliwa msingi mzuri kuanzia ngazi za awali.
Saileku anasema kama msingi wa mwanafunzi kuipenda hesabu na kuiona kama somo la kawaida haujajengwa tangu anapokuwa darasa la awali, ni vigumu kwake kulipenda na hata kufanya vizuri.
“Wanafunzi wawekwe katika mazingira ya kupenda somo la hesabu tangu ngazi za awali. Kama msingi ukiwa mbovu, ni vigumu kwa mwanafunzi kufanya vizuri katika masomo yake,” amesema.
Pia anasisitiza kuwa ni muhimu kwa walimu, wazazi na jamii kwa ujumla kuacha tabia ya kuwajengea watoto dhana kuwa masomo ya hisabati na sayansi ni magumu.
Anasema dhana hiyo inachangia baadhi ya wanafunzi kuyaogopa masomo hayo na hatimaye kushindwa kufanya vizuri.
Akifafanua, mtaalamu wa saikolojia na mdau katika masuala ya malezi, Vanessa Mpagelage, anasema katika malezi ya mtoto, kile anachokuzwa nacho ndicho anachoishi na kukiamini.
“Anapoambiwa jambo hili ni baya au zuri, anaishi na kukua akiamini hivyo. Unapomwambia hesabu ni ngumu tangu mdogo, naye hukua na kuishi akiamini kuwa somo la hesabu ni gumu,” anasema.
Anasema kwa kawaida unapomwambia mtu na kuamini kuwa jambo ni rahisi, ubongo nao hujipanga kulirahisisha, lakini unapomwambia ni gumu na akaamini, ubongo hupokea ujumbe huo na kufanya alione kuwa gumu zaidi.
Anasema ni vyema jamii kufahamu athari ya kile wanachokizungumza kwa watoto, kwa kuwa kile unachomueleza ndicho anachokua nacho na kukiamini.
‘Ufaulu unatofautiana’
Katika hisabati, Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (Chahita), Dk Said Sima, anasema changamoto za ujumla zipo, lakini mara zote ufaulu hutofautiana kati ya mkoa na mkoa na halmashauri, huku akibainisha kuwa tathmini ya kina itawezesha kubaini maeneo yenye changamoto na kuyashughulikia.
“Kila halmashauri ifanye tathmini ili kujua ufaulu wake na iweke juhudi za makusudi kupambana na hali hiyo, iwe ni upungufu wa walimu au tatizo lipo wapi, kwa sababu sasa halmashauri zinaweza kuajiri walimu wa muda,” anasema Dk Sima.
Anaongeza kuwa kama kuna upungufu wa walimu, teknolojia inaweza kutumika, ikiwemo mwalimu mmoja kufundisha kwa masafa ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
“Hii inaweza kufanyika ndani ya halmashauri, walimu waliopo wakajipanga kusaidia shule zote, na hakuna mwanafunzi anayeachwa nyuma. Hili litawezekana kupitia tathmini itakayofanyika,” anasema.
Anatolea mfano shule moja aliyokuwa akiifuatilia bila kuitaja jina, akisema kuwa katika matokeo ya mwaka 2024 ilifaulisha asilimia 55, lakini sasa imeshuka hadi chini ya asilimia 40, hali inayothibitisha umuhimu wa tathmini.
“Halmashauri ndiyo eneo dogo linaloweza kumaliza changamoto zake vizuri, iwe ni semina au jitihada nyinginezo,” anasema.
Anaongeza kuwa wanafunzi wanaweza kutumika kusaidia wenzao, ambapo mwanafunzi wa kidato cha nne akafundisha wa kidato cha tatu, na wa kidato cha sita akafundisha wa kidato cha tano, hali itakayosaidia kuimarisha ujifunzaji.
Pia anasema njia nyingine ni kuwachangamanisha wanafunzi wasiofanya vizuri na wale wanaofanya vizuri ili kuwachochea kufanya vizuri zaidi.
“Kuna shule za kawaida zinafaulisha zaidi ya asilimia 90. Mfano ni Shule ya Pamoja Ngabobo iliyofaulisha kati ya asilimia 94 hadi 97 katika somo la hisabati. Uzoefu waliotumia ni kuwashindanisha wanafunzi wao na wale wa Ilboru, jambo lililowafanya wachangamke na kufaulu,” amesema.
Mdau wa elimu, Dk Muhanyi Muhanyi, anasema zipo sababu mbalimbali zinazosababisha ufaulu hafifu katika masomo ya sayansi, baadhi zikiwa za wanafunzi wenyewe na nyingine zikiwa za kimfumo zinazohusisha shule na walimu.
Anasema bado kuna pengo kubwa linalofanya watu kupendelea masomo ya sanaa na kuacha sayansi, hali inayoweza kutatuliwa na jamii, wazazi na walimu kwa kutoa msisitizo chanya kwa wanafunzi.
“Tunaweza kuinua ufaulu wa masomo haya kama tutaachana na dhana na misemo iliyopo katika jamii kwamba hisabati ni ugonjwa wa taifa,” anasema.
Pia anasisitiza umuhimu wa kuwawezesha walimu kwa kuwapatia semina endelevu na kuwajengea uwezo wa kufundisha kwa weledi, akisema mwalimu bora huzalisha mwanafunzi bora.
Dk Nkoronko anaweka bayana pia haja ya kutatua changamoto zinazofanya ufundishaji wa masomo ya sayansi kuwa mgumu, ikiwemo kuongeza maabara katika shule za sekondari, vitabu vya kiada na ziada.
“Pia vyumba vya madarasa viwepo vya kutosha, kwani kuna baadhi ya wanafunzi wanafeli kwa sababu wanashindwa kufikiwa na walimu,” anasema.