Hivi ndivyo Taliban walivyojijenga kutokana na ufadhili wa Marekani

Muktasari:

  • Ulimwengu unawatazama Taliban kama watu hatari na haushangazwi jinsi walivyoichukua Afghanistan na kuiweka kwenye himaya yao, bali unastaajabishwa na namna ilivyokuwa rahisi kuliteka Taifa hilo.

Ulimwengu unawatazama Taliban kama watu hatari na haushangazwi jinsi walivyoichukua Afghanistan na kuiweka kwenye himaya yao, bali unastaajabishwa na namna ilivyokuwa rahisi kuliteka Taifa hilo.

Wengi wanataka kujua Taliban ni akina nani, walikotoka na kiwango cha nguvu zao, lakini swali mama ambalo wengi wanajiuliza, wanaweza vipi kuitesa Marekani?

Historia ya kuanzishwa na kukua kwa Taliban kunahusisha msaada wa mataifa mawili; Marekani na Pakistan. Naam, Marekani wanateswa na kinyago chao wenyewe. Si kwamba Marekani ilisaidia moja kwa moja, bali kwa mlango wa nyuma.

Nguvu kubwa ya Marekani katika kuidhoofisha Dola ya Umoja wa Nchi za Sovieti (USSR) ndiyo sababu ya kuibuka kwa Taliban.


Mwanzo wa Taliban

Mwaka 1978, USSR iliivamia Afghanistan na kuikalia kimabavu. Uhasimu wa jadi kati ya Urusi na Marekani ikawa sababu ya wapiganaji wa Afghanistan, hasa vikundi vya mujahidina, kupokea misaada ya hali na mali kutoka Marekani.

Picha ya mwaka 1983 ya Rais wa 40 wa Marekani, Ronald Regan, akiwa na mujahidina wa Afghanistan Ikulu ya Marekani, ni kielelezo cha namna ambavyo Taifa hilo lilikuwa mstari wa mbele kuhakikisha USSR wanang’oka Uarabuni.

Rais wa zamani wa Pakistan naye, Muhammad Zia-ul-Haq alipoona USSR wameiteka Afghanistan, aliogopa kwamba nchi yake ingevamiwa kupitia Mji wa Balochistan, hivyo akatoa msaada kwa wapiganaji wa Afghanistan waliotaka kuwaondoa Sovieti.

Rais Zia-ul-Haq alimtuma aliyekuwa Mkuu wa Majeshi, Akhtar Abdur Rahman kwenda nchini Saudi Arabia kuomba ushirikiano wa kuwasaidia wapiganaji wa Afghanistan halafu Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) na Kurugenzi Kuu ya Kiintelijensia, Saudi Arabia (GID), waliwezesha fedha na vifaa kwa Shirika la Usalama wa Taifa la Pakistan (ISI) kwa ajili kuendesha mafunzo kwa wapiganaji wa Afghanistan.

Mwanzoni mwa miaka ya 1980, vijana 90,000 wa Afghanistan walipewa mafunzo na ISI nchini Pakistan kwa msaada wa CIA (Marekani) na GID (Saudi Arabia). Katika vijana hao alikuwamo aliyeitesa Marekani baadaye anayejulikana kama Mohammed Omar, lakini dunia ikimtambua kama Mullah Omar.

Muhimu zaidi kufahamu ni kwamba mwanzoni kwenye mapambano ya Waafghani dhidi ya USSR, viongozi wote wa Taliban, ama walikuwa kwenye kundi la Hezb-i Islami Khalis au Harakat-i Inqilab-e Islami, makundi makubwa ya mujahidina yalikuwa yanapigana kuwaondoa USSR nchini Afghanistan.

Kama utataka kufahamu Taliban walitoka wapi, kwa lugha rahisi kabisa ni kuwa kundi hilo lilizaliwa kutoka kwenye makundi mawili ya mujahidina, Hezb-i Islami Khalis au Harakat-i Inqilab-e Islami, ambayo yalijengwa na Pakistan kwa ufadhili wa Marekani na Saudi Arabia.

Aprili 1992, baada ya Sovieti kuangushwa, hivyo kuondolewa madarakani kwa utawala wa Mohammad Najibullah, ambaye alikuwa anaungwa mkono na Urusi, Waafghani kwa wingi wao, walikubaliana kuchangia mamlaka, chini ya mkataba maarufu wa Peshawar Accord.

Ni kupitia Peshawar Accord, ndipo Dola ya Kiislamu ya Afghanistan ikazaliwa kisha Serikali ya mpito ikaundwa. Chama cha siasa Afghanistan, Hezb-e Islami Gulbuddin, kilichoongozwa na Gulbuddin Hekmatyar, vyama vya Hizb-e Wahdat na Ittihad-i Islami, havikushirikishwa katika Serikali hiyo, hivyo kumaanisha Dola ya Kiislamu ya Afghanistan ilifeli ilipozaliwa tu.

Kutokana na kutoshirikishwa, Hekmatyar na chama chake, Hezb-e Islami Gulbuddin, hawakuitambua Serikali ya mpito iliyoundwa.

Itaendelea kesho...