Hizo ndizo fadhila za siku kumi za Dhul Hijja kwa Waislamu
Picha na Mtandao.
Muktasari:
- Katika kipindi hiki waumini wanapaswa kuongeza ibada za saumu, kusoma Qur’an, kutoa sadaka na kufanya dua nyingi.
Dar es Salaam. Waislamu duniani wameingia katika moja ya vipindi vitukufu zaidi katika kalenda ya Kiislamu, huku viongozi wa dini wakiwahimiza waumini kutumia vizuri masiku kumi ya mwanzo ya mwezi wa Dhul Hijja kwa kuongeza ibada, kufanya toba, kusaidia wahitaji na kurekebisha mwenendo wa maisha yao.
Masiku hayo ambayo ndani yake ipo ibada ya Hijja pamoja na Sikukuu ya Eid Al-Adha, yamekuwa yakitajwa kuwa miongoni mwa siku zenye fadhila kubwa zaidi katika Uislamu, kutokana na wingi wa rehema, msamaha na malipo ya matendo mema yanayofanywa ndani yake.
Wanazuoni wa Kiislamu wanaeleza kuwa hizi ni siku ambazo Allah huzipenda zaidi amali njema zinazofanywa na waumini wake kuliko kipindi kingine chochote katika mwaka.
Katika Qur’an Tukufu, Allah Mtukuka amesema:“Naapa kwa alfajiri. Na kwa masiku kumi.” (Surat Al-Fajr: 1–2)
Kwa mujibu wa wafasiri wengi wa Qur’an, “masiku kumi” yaliyotajwa katika aya hiyo ni masiku kumi ya mwanzo ya Dhul Hijja.
Aya nyingine inayotajwa kuhusu ubora wa siku hizi ni ile ya Surat Al-Hajj inayosema:
“Ili washuhudie manufaa yao na kulitaja Jina la Allah katika masiku maalumu.” (Surat Al-Hajj: 28)
Wanazuoni wanasema aya hizo zinaonyesha namna Allah alivyozipa hadhi kubwa siku hizi na kuwataka waumini kuzitumia katika ibada na utiifu.
Mtume Muhammad naye amenukuliwa katika hadithi sahihi akisema:“Hakuna masiku ambayo amali njema inapendwa zaidi mbele ya Allah kuliko masiku haya kumi.”
Maswahaba waliuliza: “Hata jihadi katika njia ya Allah?”
Mtume akajibu:“Hata jihadi, isipokuwa mtu aliyetoka na nafsi yake na mali yake kisha hakurudi na chochote.”
Hadithi hiyo iliyopokewa na Sahih al-Bukhari imeendelea kuwa msingi wa wanazuoni kuwahimiza Waislamu kuongeza ibada katika kipindi hiki.
Akizungumza na Mwananchi, Sheikh Mussa Salum amesema masiku haya ni fursa adhimu kwa kila Muislamu kurekebisha uhusiano wake na Mwenyezi Mungu na kujitathmini kiimani.
Amesema katika kipindi hiki waumini wanapaswa kuongeza ibada za saumu, kusoma Qur’an, kutoa sadaka na kufanya dua nyingi.
“Hizi ni siku ambazo rehema za Allah hushuka kwa wingi. Muumini anatakiwa kutumia vizuri nafasi hii kwa kufanya toba ya kweli na kuongeza matendo mema,” amesema Sheikh Salum.
Ameongeza kuwa baadhi ya watu hujihusisha zaidi na maandalizi ya Sikukuu ya Eid Al-Adha huku wakisahau kiini cha masiku haya ambacho ni ibada na utiifu kwa Allah.
“Eid ni sehemu ya furaha, lakini kabla yake kuna safari ya ibada. Watu wasikimbilie mavazi na maandalizi ya nyama huku wakisahau kuswali, kufunga na kufanya dua,” amesema.
Kwa upande wake, Sheikh Ali Kibwana amesema masiku haya yanapaswa pia kuwa kipindi cha kuimarisha mshikamano wa kijamii na kusaidia wenye mahitaji.
Amesema Uislamu umeweka mkazo mkubwa katika kuwajali maskini, mayatima na watu wenye changamoto za maisha, hasa katika vipindi vya ibada.
“Tunapokaribia Eid Al-Adha ni muhimu wenye uwezo kuwasaidia wasiojiweza ili kila mmoja afurahie siku hizi kwa amani na upendo,” amesema Sheikh Kibwana.
Amesema changamoto za kiuchumi zinazoikabili jamii kwa sasa zinahitaji watu kuwa na moyo wa kusaidiana badala ya kuishi kwa ubinafsi.
Katika masiku haya, siku ya tisa ya Dhul Hijja maarufu kama Siku ya Arafah imepewa nafasi ya kipekee katika Uislamu.
Mtume Muhammad (Rehema na amani zimshukie) amesema:“Hakuna siku ambayo Allah Huwaokoa watu wengi zaidi kutoka motoni kuliko siku ya Arafah.” (Imepokewa na Sahih Muslim)
Kwa wasiokuwa katika ibada ya Hijja, kufunga siku hiyo kunaelezwa kuwa na malipo makubwa mbele ya Allah.
Mtume amesema:“Ninatarajia kwa Allah kuwa Saumu ya siku ya Arafah inafuta madhambi ya mwaka uliopita na mwaka unaofuata.”
Wanazuoni wengi wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kufunga siku hiyo kwa wale wenye uwezo ili kupata fadhila hizo kubwa.
Kuacha maovu
Naye, Sheikh Kwega Mfaume amesema vijana wanapaswa kutumia kipindi hiki kujitenga na maovu na kurejea katika maadili mema.
Amesema changamoto nyingi zinazoshuhudiwa katika jamii hivi sasa, ikiwamo matumizi ya dawa za kulevya, ukosefu wa maadili na ongezeko la vitendo vya uhalifu, vinaweza kupungua ikiwa watu watarejea katika misingi ya dini.
“Masiku haya si ya anasa pekee, ni wakati wa kutafakari maisha yetu, kufanya toba na kuimarisha ibada. Vijana wanapaswa kutumia muda wao katika mambo yenye manufaa,” amesema Sheikh Mfaume.
Ameongeza kuwa baadhi ya watu huingia katika kipindi cha Eid kwa matumizi makubwa kupita uwezo wao jambo ambalo baadaye huwasababishia matatizo ya kifedha.
Mbali na saumu na dua, wanazuoni wamewahimiza Waislamu kuongeza dhikri katika siku hizi kwa kumtaja Allah mara kwa mara kupitia takbira, tahmid na tasbih.
Aidha, kwa wale wenye uwezo wa kifedha, kuchinja katika siku ya Eid Al-Adha ni sunnah kubwa inayofufua utiifu wa Nabii Ibrahim.
Allah amesema:“Basi swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje.” (Surat Al-Kawthar: 2)
Yapi ya kuzingatia katika siku hizi
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata Sheikh Khamis Mataka amesema hizi ni siku tukufu sana katika Uislamu, siku ambazo ndani yake kuna fadhila kubwa, rehema nyingi na fursa adhimu ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.
Katika kipindi hiki, Sheikh Mataka amewataka waislamu kuzingatia mambo muhimu matano ikiwemo kuuimarishe ibada na uchamungu, kuwakumbuka wenye uhitaji, kudumisha umoja, upendo na mshikamano.
Mambo mengine ni kujiepusha na maasi ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya, ulevi, Kamari, uasherati na tabia zote zinazoharibu maadili ya Kiislamu.
Pia amesisitiza kuendelea kuombea amani, utulivu na mshikamano kwa Taifa na wawe mstari wa mbele kujenga Taifa lenye maadili.
“Vilevile, ninawakumbusha Waislamu kuwa ibada ya kuchinja ni alama ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu, si mashindano ya kujionyesha wala fahari mbele za watu. Mwenyezi Mungu haziifikii nyama wala damu zake, bali humfikia uchamungu wetu.
“Nawaomba Waislamu wote wazitumie siku hizi kwa kufanya tathmini ya maisha yao, kuongeza matendo mema na kurekebisha pale walipokosea. Huenda hii ikawa Dhul Hijja yetu ya mwisho, hivyo tujitahidi kuvuna kheri nyingi kabla ya kurejea kwa Mola wetu,” amesema.