Hofu ya viongozi na huduma za jamii kijijini Gambosi

Kigango cha Kanisa Katoliki katika Kijiji cha Gambosi. Simulizi nyingi zimekuwa zikieleza kuwa kijiji hicho hakina makanisa na kwamba, wananchi wake wanaishi kwa kufuata imani za jadi na ushirikina. Picha na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

Tangu Taifa lipate Uhuru mwaka 1961, kiongozi pekee wa kitaifa aliyekanyaga ardhi ya Gambosi ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Maisha ya wananchi katika Kijiji cha Gambosi ni sawa na maeneo nchini licha ya kwamba zimekuwepo taarifa nyingi kukihusu. Hata hivyo, simulizi zingine zimeendelea kubeba ukweli wa kijiji hicho maarufu mkoani Simiyu. Sasa endelea...

Tangu Taifa lipate Uhuru mwaka 1961, kiongozi pekee wa kitaifa aliyekanyaga ardhi ya Gambosi ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Viongozi wengine waliokanyaga ardhi ya kijiji hicho ambao kwa sasa wanahesabika kama wenyeji wa Gambosi, kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Gambosi, Kaliwa Bahame ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga.

Tangu walipoteuliwa kushika nyadhifa zao, viongozi hao wawili wa wilaya na mkoa wamefika kijijini hapo mara kadhaa kuhimiza shughuli na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Viongozi wengi wanakwepa kijiji chetu. Pengine ni kutokana na historia mbaya ya ushirikina tunaohusishwa nayo. Ninyi sasa muwe mabalozi wetu kuwa ushirikina Gambosi ni hadithi za matukio ya kale,” anasema diwani Bahame.

Viongozi na fursa kupitia Gambosi

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkuu wa Mkoa, Mtaka na Katibu Tawala wa mkoa huo, Jumanne Sagini wanasema uongozi wa mkoa umekubaliana kutumia historia ya kijiji hicho kama mojawapo wa vivutio vya utalii na kiuchumi mkoani humo.

“Kwa mfano idara ya utamaduni na mambo ya kale katika taasisi zetu za elimu ya juu inaweza kukifanya Kijiji cha Gambosi kuwa miongoni mwa maeneo ya kufanyia utafiti wa utamaduni na imani za kale,” anasema Mtaka.

Sagini anaahidi kuwa, ofisi yake iko tayari kusaidia taasisi au mtu binafsi mwenye nia ya kutumia historia ya kijiji hicho kama fursa yenye mchango chanya wa maendeleo na maisha ya wenyeji wa eneo hilo.

“Gambosi ni eneo potential kwa utafiti wa utamaduni na tiba asili kwa kitengo cha dawa na tiba asilia pale Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili,” anasema Sagini.

Katibu tawala huyo anaelezea kufurahishwa na uamuzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd wa kufuatilia na kuandika makala maalumu kuhusu historia ya kijiji hicho anayosema imepotoshwa kwa muda mrefu.

“Sisi viongozi wa Mkoa wa Simiyu, Gambosi ni sawa na vijiji vingine na tunafika mara kwa mara kuhamasisha maendeleo. Tunataka kila mmoja aelewe na kuamini hivyo, badala ya kukalia historia inayopotosha ukweli,” anasisitiza Sagini.

Huduma jamii

Huduma ya umeme kupitia mradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), imefika kijijini hapo, huku ujenzi wa shule ya sekondari ukiendelea.

Miongoni mwa shughuli za kiuchumi zinazofanyika kijijini hapo kupitia huduma ya nishati ya umeme ni ufundi wa kuchomelea na miradi ya mashine za kukoboa na kusaga nafaka.

Kijiji cha Gambosi pia kina zahanati inayotoa huduma za afya ambayo hata hivyo hutumiwa zaidi na wageni, watendaji na watumishi wa umma wakiwamo walimu, maofisa ugani na watumishi wa kada zingine kutokana na idadi kubwa ya wenyeji wa eneo hilo kutumia zaidi tiba asili.

Tofauti na vijiji vingine jirani, Mtendaji wa Kijiji cha Gambosi, Chalo Charles anasema wananchi wa eneo hilo wanapata huduma ya uhakika ya majisafi na salama kutoka kwenye visima virefu na vifupi vilivyochimbwa kijijini hapo.

Ingawa kuna shule ya msingi, huku ujenzi wa sekondari ukiendelea, Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Msingi Gambosi, Mathias Sumuni anataja suala la utoro kuwa changamoto inayokwamisha maendeleo ya elimu kwa watoto wa wenyeji.

Shule ya Msingi Gambosi ina zaidi ya wanafunzi 1,100 na walimu 20, kati yao wakiwamo wa kike wanane.

“Mwaka huu tumeandikisha watoto 220 walioanza darasa la awali. Badala ya kuchunga mifugo, wazazi sasa waelimishwe umuhimu wa kuwapeleka shule watoto wao,” anashauri mwalimu Sumuni.

Akijibu swali iwapo amewahi kukumbana na mauzauza tangu alipohamishiwa Gambosi, mwalimu huyo anasema, “Wanaoeneza habari za ushirikina Gambosi ni watu wasiojua historia sahihi ya kijiji hiki na ambao hawajafika hapa. Tunaoishi hapa tunapaona pa kawaida kama maeneo mengine tulikotoka.”

Changamoto ya barabara

Changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa kijiji hicho kinachoweza kutumika kama moja ya vivutio vya kitalii na kielimu kwa wanafunzi wa masomo ya mila, desturi na utamaduni za Kiafrika ni miundombinu ya barabara.

“Wageni wanaokuja kijijini kwetu hutumia njia na mapito ya ng’ombe. Hakuna barabara rasmi baada ya kutoka kijiji jirani cha Nyamuswa. Viongozi lazima warekebishe kasoro hii kwa kutuchongea barabara,” anasema mkazi wa kijiji hicho, Maduhu Nsangi.

Akionyesha hisia ya kutengwa kimaendeleo, mwananchi huyo anahoji, “Au kwa sababu kijiji chetu kinadaiwa kuwa cha kichawi ndiyo maana halmashauri ya wilaya inachonga barabara na kuishia Nyamswa?”

Makanisa na huduma za kiroho

Pengine msomaji utashangaa, lakini pamoja na historia na simulizi zinazokihusisha Kijiji cha Gambosi na imani za kishirikina, wakazi wake hawapo nyuma kwenye masuala ya kiroho.

Kuna makanisa matano yanayoeneza neno la Mungu kwa wakazi wa kijiji hicho. Lipo Kanisa Katoliki; la Adventista (Wasabato); la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT); African Inland Church of Tanzania (AICT) na Living Water.

“Haikuwa jambo rahisi tulipoanza kueneza injili hapa (Gambosi). Hii ni kwa sababu wenyeji wengi waliamini na kushikilia dini za jadi, lakini tunamshukuru Mungu anatenda kuna zaidi ya watu 1,000 wamemgeukia Mungu na kubatizwa,” anasimulia Mwinjilisti wa Kanisa la Living Water, Emmanuel Kalwari

Ni nyumbani mkuu wa kanisa

Miongoni mwa masuala ya kihistoria kwa Kijiji cha Gambosi ni pamoja na kuwa nyumbani kwao na Askofu Mkuu wa Kanisa la Wasabato, Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania, Mark Malekana.

Diwani Bahama anasema kiongozi huyo wa kiroho amekuwa chachu ya maendeleo ya sekta mbalimbali kijijini hapo ikiwamo elimu baada ya kusaidiana na wadau na viongozi wengine akiwamo Mkuu wa mkoa huo, Mtaka kufanikisha ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara kwenye Shule ya Sekondari Gambosi.

Ujenzi wa shule hiyo ya sekondari ambao kukamilika kwake kutaondoa dhana potofu kuwa wananchi waishio Gambosi ya ushirikina na badala yake wametakiwa wajenge mpya yenye watu wasomi na weledi.

Licha ya kijiji hicho kuwa na miradi ya maendeleo, Mtendaji wa Kata ya Gambosi, Mathew Shini anabainisha kuwa vitendo vya ushirikina vilikuwa vikifanyika kipindi cha nyuma ambacho kila mtu aliyetembelea kijiji hapo alijionea miujiza mingi hasa usiku.

“Watu wengi walijionea maaajabu mengi katika kijiji hicho ambacho ulikuwapo mti maarufu kwa jina la Nkune, ambao ulikuwa ukienda ukapumzika unaweza ukastukia unatengewa chakula bila kuona mtu na usipokula tu unaweza kupoteza maisha,” anasema Shini.

Anasema kuenea kwa taarifa kulitokana na watu waliowahi kufika kijijini hapo ambao unaweza kuamka usiku ukajikuta upo nje ya nyumba na hayo walikuwa wanafanyiwa wageni na muda mwingine unaweza kuona mji mkubwa kama Dar es Saalam unawaka taa za umeme.

Shini anasema hivi sasa vitu hivyo havipo tena kutokana na kuwapo kwa utandawazi na wengi waliokuwa wakifanya uchawi kufariki dunia, hivyo huwezi kuona au kutokewa miujiza mpaka nawe uwe unatumia dawa za kichawi ndipo unaweza kuuona.