Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Homera ataja sababu kutotekelezwa maamuzi ya mahakama

Waziri wa Katiba na Sheria Dk Juma Homera akiwa katika chumba cha kupokea kero na malalamiko ya wananchi ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Amesema malalamiko mengi wanayopata ofisini kwake, yanaonyesha haki zilishapatikana mahakamani lakini kwenye kutekeleza wa uamuzi huo unakuwa na ugumu, hivyo kufanya haki ichelewe kuwafikia waliostahili.

Dodoma. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera amekiri kuwa utekelezaji wa sheria kwa watu walioshinda kesi mahakamani bado una changamoto huku akibainisha kuwa uzembe uko kwa baadhi ya watendaji wa ngazi ya chini.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kuzitumia ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya kwani wana vyombo vya kusimamia utekelezaji wa sheria ikiwemo Polisi.

Dk Homera ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 14, 2026 wakati akitoa ufafanuzi kwenye kipindi cha ‘Sema na Waziri’ ambacho hutumika kupokea kero na malalamiko.

Amesema malalamiko mengi wanayopata ofisini kwake, yanaonyesha haki zilishapatikana mahakamani lakini kwenye kutekeleza wa uamuzi huo unakuwa na ugumu, hivyo kufanya haki ichelewe kuwafikia waliostahili.

“Si mmeona hata simu nyingi tulizopokea leo, inaonyesha watu walishinda mahakamani lakini kuna kauzembe mahali ambako lazima kashughulikiwe ili mwananchi anaposhinda apate haki yake mapema bila kuchelewa,” amesema Dk Homera.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameagiza kesi ya Salum Namtuka, mkazi wa Dar es Salaam, ishughulikiwe kwa haki, akisema ni aibu Wakili wa Serikali kushauri kesi ya jinai ikamalizwe kwa madai hata kabla ya kufikishwa mahakamani, hivyo kuna haja ya kumfuatilia mtumishi huyo.

Waziri wa Katiba na Sheria Dk Juma Homera akiwa katika chumba cha kupokea kero na malalamiko ya wananchi ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma.

Namtuka amepiga simu kuelezea namna alivyozungushwa Polisi huku Wakili wa Serikali akimtaka afungue kesi ya madai kufuatia shambulio la kupigwa risasi ambapo hadi sasa anaishi na kipande cha chuma shingoni, jambo alilosema limekuwa la muda mrefu.

Mwananchi huyo amesema alipewa maelekezo hayo na Wakili wa Serikali licha ya ushahidi kuwa wazi lakini alikataa kupeleka kesi mahakamani badala yake akaelekeza muhusika aombe madai kwani waliompiga risasi hawakukusudia kuumia.

“Haya ni mambo ya ajabu sana, Wakili wa Serikali unaamua mambo yako kichwani hii si sawa, Polisi naomba kesi hiyo muanze upya ili tuweze kumsaidia mwananchi huyu,” amesema Dk Homera wakati akizungumza na Polisi wa Dar es Salaam.

Dk Homera amesema bila sheria madhubuti na utekelezaji wa haki, hakutakuwa na Taifa lenye haki, hivyo akaomba kila mmoja kuwajibika kwa nafasi yake katika kuitafuta haki.

Akizungumzia lugha za hukumu ambazo hutolewa kwa Kiingereza, amesema agizo lililotolewa jana na Rais Samia Suluhu Hassan jijini Arusha, kuanzia sasa mawakili watazunguka nchi nzima kufafanua sheria zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.

Amefafanua kuwa hadi sasa sheria 446 zimetafsiriwa na nyingine karibu 1,000 ziko mbioni kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, akisisitiza majaji kuongeza nguvu ya uandishi wa hukumu.