Hospitali ya Bugando yapeleka huduma stendi Nyegezi

Wataalam wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando wakitoa huduma kwa baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza wakati wa huduma ya vipimo, ushauri na matibabu bila malipo katika kambi ya matibabu eneo la Stendi Kuu ya Nyegezi. Picha na Damian Masyenene

Muktasari:

Ofisa Mfiziotherapia kutoka Hospitali ya Bugando, Dk Samson Apolinary amesema idara hiyo hupokea na kuhudumia wastani wa wagonjwa 100 kila siku.

Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando inapokea na kuhudumia wastani wa wagonjwa 36, 000 wenye matatizo ya mgongo, shingo na shinikizo la damu kila mwaka.

Pamoja na sababu zingine za kiafya, tabia ya kutofanya mazoezi na shughuli za kila siku za kiuchumi zinazosababisha wengi kukosa muda wa kupumzika zinatajwa kuchangia matatizo hayo, huku kundi la waendesha pikipiki na bajaji wakielezwa kuwa hatarini zaidi.

Akizungumza jijini Mwanza leo Mei 18, 2023 wakati wa kambi ya kutoa huduma ya vipimo, ushauri na matibabu bila malipo kwa wakazi wa jiji la Mwanza, Ofisa Mfiziotherapia kutoka Hospitali ya Bugando, Dk Samson Apolinary amesema idara hiyo hupokea na kuhudumia wastani wa wagonjwa 100 kila siku.

Kambi hiyo ya vipimo, ushauri na matibabu bila malipo zimetolewa katika eneo la Kituo Kikuu cha Mabasi Nyegezi ikilenga kuwafikia madereva wa magari, pikipiki na bajaji.

“Watu wengi tunaowafanyia vipimo leo wamebainika kuwa na matatizo ya mgongo, maumivu ya shingo, kisukari, uzito na unene uliopitiliza kutokana na kutofanya mazoezi na aina ya shughuli zao za kiuchumi,’’ amesema Dk Apolinary

Ameongeza; “Baadhi ya madereva wamebainika kuwa na tabia ya kutoenda hospitali kupata matibabu sahihi baada ya ajali, hali inayowaweka katika hatari ya kupata kiharusi au ulemavu wa kudumua unaoweza kupunguza uwezo wao kiutendaji na kuwafanya tegemezi,”

Samuel Daud, mmoja wa madereva waliopata huduma ameushukuru uongozi wa Hospitali ya Bugando kwa kuwasogezea huduma ya vipimo, ushauri na matibabu bila malipo.

‘’Nimepata vipimo, ushauri na matibabu. Nimefanikiwa kufahamu chanzo cha tatizo langu la muda mrefu la maumivu ya mgongo kuwa ni kukaa na kuendesha gari muda mrefu. Nawashauri madereva wenzangu kujenga tabia ya kufanya mazoezi, kupima afya na kupata muda wa kupumzika,’’ amesema Samuel

Wito wa madereva kufanya mazoezi, kupima afya na kupata muda wa kupumzika pia umetolewa na Amani Masashua huku akiuomba uongozi wa Hospitali ya Bugando kuongeza siku za kambi ya matibabu eneo la Stendi ya Nyegezi ili kufikia wahitaji wengi zaidi.

Ofisa Mfiziotherapia Hospitali ya Bugando, Gilbert Mrosso amewashauri Watanzania kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kufanya mazoezi na kuepuka mitindo ya maisha yenye madhara kiafya ikiwemo ulaji usiofaa.