Huduma za benki zapiga hodi kwa Mrombo
Muktasari:
- Benki ya NMB imeendelea kuongeza mtandao wake kwa fungua tawi la 229 Kwa Mrombo jijini Arusha.
Arusha. Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeipongeza Benki ya NMB kwa kuwa kinara miongoni mwa benki 44 nchini kwa kutanua mtandao wa matawi, hivyo kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za benki na hivyo kukuza kiwango cha amana za wateja.
Pongezi hizo zimetolewa leo Jumatano Mei 3 na Mkurugenzi wa BoT Kanda ya Arusha, Ibrahim Malogoi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, wakati wa uzinduzi wa tawi la Benki ya NMB Kwa Mrombo jijini Arusha.
Tawi hilo linakuwa tawi la 229 kwa benki hiyo nchini, hafla iliyohudhuriwa na Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi.
Uzinduzi wa tawi la Kwa Mrombo linalokuwa la sita la benki hiyo jijini Arusha, umefanyika, sambamba na makabidhiano ya msaada wa madawati 100 kwa shule ya msingi Msasani iliyopo jirani na tawi hilo, kupitia programu ya uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Malogoi amesema sekta ya fedha inakua kwa kasi na wao kama wasimamizi wakuu wa sekta hiyo wanafarijika kwa ongezeko la matawi ya benki nchini.
"Sekta ya Fedha inakua kwa kasi bila kupingwa, Tanzania tunazo benki 44, kati ya hizo Kanda ya Kaskazini zipo 28, huku mkoa wa Arusha pekee zikiwepo 26 zinazotoa huduma.
“Tawi hili ambalo limekuja kwa wakati sahihi, ni ushahidi wa kukua kwa sekta hii, kwani linakuwa ni tawi la 988 ya matawi ya mabenki yote nchini,” amesema.
Amesema kati ya matawi hayo, 196 yapo katika Kanda ya Kaskazini (Arusha, Tanga, Manyara na Kilimanjaro), huku tawi hili la NMB Kwa Mrombo likiwa la 65 mkoani Arusha.
“Sisi BoT tunafarijika kwa ongezeko hilo ambalo litaongeza kiwango cha amana kwa Mkoa na Kanda yetu, lakini pia kwa Taifa.
"Kwa rekodi zilizopo, hadi Desemba 2022, kiwango cha amana za wateja ni Sh3.3 trilioni, kati ya hizo Sh1.4 trilioni ni amana za wateja waliopo mkoani Arusha pekee, ndio maana tunaamini kwa ujio wa tawi hili, NMB itaharakisha kukua kwa amana hizo," amefafanua Malogoi.
Kwa upande wake, RC Mongella amesema anaamini kuwa tawi hilo ni kichocheo cha ukuaji kiuchumi kwa wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi wa Arusha, na kuwa uwingi wa matawi mkoani mwake, pamoja na uwekezaji mkubwa kidijitali uliofanywa na benki hiyo.
"Tawi hili, sambamba na mengineyo mkoani Arusha, litakuwa kichocheo cha ukuaji wa haraka kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja, mkoa na Taifa kwa ujumla, hasa ukizingatia uwekezaji mkubwa wa kidijitali uliofanywa na benki hii, ambao utachagiza upatikanaji wa huduma.
Awali, Mponzi alimshukuru RC Mongella kwa kutenga muda wa kushiriki uzinduzi wa tawi hilo ambalo linaenda kuwa chachu ya maendeleo na mkombozi wa wateja wao, wakiwemo mawakala wa NMB waliotapakaa katika mji wa Arusha na mikoa mikoa jirani ya Kanda ya Kaskazini.
"Tunajivunia kukua kwa mtandao wetu wa matawi, sambamba na uwekezaji mkubwa kidijitali, ambao unampa fursa mteja kufungua akaunti kwa simu na hata kupata huduma, zikiwemo za Mikopo midogo isiyo na dhamana ya Mshiko Fasta," amebainisha Mponzi mbele ya Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Matawi ya NMB, Donatus Richard na Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Dismas Prosper.
Sherehe zinazoenda sambamba na kampeni endelevu ya upandaji miti milioni moja kwa mwaka huu, iliyozinduliwa Machi mjini Dodoma na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.