Hujuma TRC, Mbarawa atoa tamko

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa

Tabora. Baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) wanadaiwa kulihujumu shirika hilo, ikiwemo kuiba mafuta huku mwingine akiyanyonya kisha kuweka maji katika injini ya kichwa cha treni.

Ingawa idadi yao haijawekwa hadharani, lakini inadaiwa kuwa watumishi hao wanafanya vitendo vya kuijumu TRC kwa manufaa yao binafsi na kusababisha hasara kubwa kwa shirika hilo.

Katika ripoti ya miaka miwili ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya utendaji ilionyesha TRC lilipata hasara ya Sh 22.8 bilioni mwaka 2020/21 na mwaka 2021/22 lilipata hasara ya Sh 31.2 bilioni.

Madai ya vitendo vya kulihujumu shirika hilo yalitolewa na jana Mkurugenzi Rasilimali watu na Utawala wa TRC, Amina Lumuli wakati akijibu hoja mbalimbali za watumishi mbele ya Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, katika stesheni ya Tabora

Lumuli alisema kulikuwa kuna tatizo kubwa la wizi hasa wa mafuta na kusababisha hasara kubwa huku kanda ya Tabora ikiongoza.

Kwa mujibu wa Lumuli TRC limekuwa likitumia Sh 1.2bilioni kwa mwezi kwa ajili kwa mwezi akisema ni gharama kubwa kutokana na hujuma za vitendo vya wizi vinavyofanywa na baadhi ya wafanyakazi wasiowaaminifu.

“Tunatumia kiasi hicho ambacho inaelekea sio halisi kutokana na hujuma zinazofanywa na baadhi ya watumishi.

“Kuna mfanyakazi alinyonya mafuta yote ya kwenye injini na kuweka maji na kusababisha kuharibika.Mwenzake aliyekwenda kuliendesha hakufahamu kama yamewekwa maj, lakini alyefanya kitendo hiki alifukuzwa kazi,” alisema Lumuli.

Katika hatua nyingine, Lumuli alisema matukio ya ajali yanarudisha TRC kupoteza mali za watu na kusababisha vifo, akisema kuna eneo walifanya uchunguzi na kubaini madereva walisababisha ajali.

Alisema walifanya jaribio la kuwasindikiza ndipo walipogundua mbinu hiyo, hata hivyo, hivi sasa matukio ya ajali yamepungua. Mbali na hilo, Lumuli alisema baadhi ya watumishi wamekuwa wakitengeneza ‘freepass’ bandia na kulisababishia hasara shirika.

“Kulikuwa na watumishi waliotengeneza za bandia na kuwa wanazigawa kwa watu na kusababisha hasara kwa shirika,” alisema.

Akizungumza na wafanyakazi hao, Profesa Mbarawa aliwataka kubadilika na kutambua kuwa shirika hilo ni lao, sio la watu fulani.

Katika mkutano huo huo, Profesa Mbarawa aliagiza kufungwa kwa kamera za usalama kwenye karakana. Pia katika treni aliagiza kufungwa kwa mfumo maalumu wa kufuatilia mwenendo wa chombo.

“Muda wa kubembelezana umekwisha, lazima tubadilike tukitambua kuwa shirika hili ni letu na sio la mtu mwingine.

“Serikali imewekeza Sh 10bilioni katika sekta ya reli ambayo inapaswa kuendelezwa na kutoa huduma bora kwa wateja wake,” alisema Profesa Mbarawa.

Waziri Mbarawa alisema wafanyakazi wanapaswa kuthaminiwa na kupewa moyo ili kufanya kazi yao vizur, ndio maana amefunga safari kwenda kusikiliza na kujifunza kutoka kwao.

Alibainisha Mkoa wa Tabora na Stesheni yake ni muhimu kwa sababu kuna njia tatu zinazounganisha reli kutoka Dar es Salaam na Mwanza kwenda mikoa ya Kigoma na Katavi.