Huu ndiyo ujumbe wa Chadema kupitia mabango

Mwanza. Kila mtu ana namna yake ya kufikisha ujumbe pale anapoandama, leo kwenye maandamano ya amani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yaliyoongozwa na Tundu Lissu, mabango yenye ujumbe mbalimbali yametawala.

Lissu apigilia msumari

Maandamano hayo yanafanyika leo Alhamisi Februari 15, 2024, kuanzia Buhongwa hadi Furahisha jijini Mwanza, yatakakohitimishwa kwa mkutano wa hadhara.

Katika bango lililobebwa na Lissu pamoja na mwanaharakati, Boniface Mwabukusi limesomeka 'miswada ya uchaguzi ni kifo cha demokrasia.'

Mabango mengine yaliyoonekana katika maandamano hayo yamesomeka: 'Tozo, kodi, rushwa ni chanzo cha umasikini kwa wavuvi.’

Yapo pia yanayosomeka, 'Katiba mpya italinda rasilimali za nchi’, 'tunataka Tume huru ya uchaguzi itupatie demokrasia ya kweli nchini.’

Lipo linalosomeka: 'Ugumu wa maisha siyo mpango wa Mungu ni mpango wa CCM, huduma mbovu za afya, tatizo la umeme, tatizo la maji, migogoro ya ardhi, miundombinu mibovu yote sababu ya CCM.’

Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), amesema mwitikio mkubwa wa wananchi katika maandamano hayo ni ishara kwamba wamechoshwa na ugumu wa maisha.

Amesema watatumia maandamano hayo kuishinikiza Serikali kutatua matatizo yanayowatesa wananchi, ikiwamo gharama za maisha kuwa juu.

Lissu, Mwabukusi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Azavel Lwaitama, John Heche, Benson Kigaila na Twaha Mwaipaya ni miongoni mwa viongozi wanaoongoza maandamano hayo yaliyoanzia Buhongwa saa 4.40 asubuhi ya leo Februari 15, 2024 kuelekea uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.

Maandamano yalipofika Nyegezi Stendi (kilomita mbili kutoka Buhongwa) msaidizi wa kiongozi huyo alionekana akimdokeza Lissu kupanda kwenye gari baada ya kutembea kwa muda mrefu, hata hivyo Lissu aligoma na kuendelea kutembea.

Tangu aliposhambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017, Lissu amekuwa akitembea kwa kuchechemea.

Mwanasiasa huyo akiwa na viongozi wenzake wametembea kwa miguu hadi eneo la Makalai walikosimama kusalimiana na wakazi wa eneo hilo.

Mkazi wa Tema, Kata ya Nyegezi, Esther Moja ameeleza kufurahishwa na maandamano hayo, akisema mabango yaliyobebwa na waandamaji ni ishara ya kupaza sauti kuhusu matatizo yanayoitesa jamii.

"Nimefurahi kumuona Lissu akiongoza maandamano, kwa mara ya kwanza tumeshuhudia maandamano ya aina hii kwa lengo la kupaza sauti zetu wananchi," amesema Esther.