Idara ya magonjwa ya moyo kujengwa KCMC
Muktasari:
- Serikali ya Tanzania imesema mwaka wa fedha 2021/22 imekusudia kujenga idara ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kaskazini (KCMC) utakaogharimu Sh6 bilioni.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema mwaka wa fedha 2021/22 imekusudia kujenga idara ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kaskazini (KCMC) utakaogharimu Sh6 bilioni.
Akizungumza bungeni Jumanne Mei 11, 2021 wakati akiwasilisha bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2021/22 ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri Dk Dorothy Gwajima amesema ujenzi huo utakuwa wa awamu.
“Hospitali imepanga kujenga wa idara ya magonjwa ya moyo utakaogharimu Sh6 bilioni. Ujenzi huo utafanyika kwa awamu, hivyo unategemewa kukamilika mwaka 2024,” amesema.
Amesema katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021, hospitali ilifanya ununuzi wa mashine ya ECHO (GE) inayotumika kwenye kliniki ya magonjwa ya moyo.
Ametaja gharama za mashine hiyo ni Sh118 milioni fedha ambazo ni mapato ya ndani, “Ununuzi wa Ventilators 2 katika Idara ya ICU, ununuzi huu umegharimu Sh175.9 milioni na ununuzi wa Patient’s monitor 15 katika idara ya ICU ambazo zimegharimu Sh426.8 milioni.”
Amesema kwa mwaka huo wa fedha, hospitali itaendelea kuboresha idara ya saratani kwa kujenga na kuanzisha huduma ya tiba kwa mionzi, kwamba ujenzi huo utagharimu Sh7 bilioni.
Amesema pia itakamilisha ujenzi wa vyumba vinne vya upasuaji ambapo kwa sasa ujenzi huo umefikia asilimia 70 ya utekelezaji. Ujenzi huo utagharimu Sh490 milioni.