Idd el Fitri kuswaliwa Moshi kitaifa

Muktasari:

Ofisa Habari wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Juma Holela alisema jana kwamba Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir atashiriki ibada hiyo.

Mikoani/Dar. Swala ya Idd el Fitri itaswaliwa kitaifa mjini Moshi mwishoni mwa wiki kulingana na mwandamo wa mwezi.

Ofisa Habari wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Juma Holela alisema jana kwamba Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir atashiriki ibada hiyo.

Kuhusu ibada hiyo, Katibu wa Bakwata Wilaya ya Moshi, Awadhi Lema alisema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Lema alisema kwa muda mrefu walikuwa wakiomba baraza la Idi lifanyike Moshi na safari hii maombi yao yamekubaliwa.

“Sala ya Idd itafanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Muungano asubuhi na baraza la Idd litafanyika saa 10:00 alasiri pale CCP (Chuo cha Polisi),” alisema.

Mkoani Dar es Salaam, Rais mstaafu Alhaji Ali Hassan Mwinyi atakuwa miongoni mwa Waislamu watakaoshiriki swala ya Idd katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum aliwataka Waislamu kujitokeza kwa wingi katika swala hiyo itakayoanza saa moja asubuhi.

Aliwasihi Waislamu kuitumia siku hiyo kuwasaidia wenye mahitaji ili kuhakikisha watu wote wanapata chakula na kusherehekea.

“Siku ya Idd ni furaha kwa wote. Waislamu watoe zaka kwa yatima, wajane, rafiki na maskini. Wagonjwa watembelewe hospitalini na kufarijiwa, familia zitembeleane na waliogombana wapatane,” alisema.

“Tumefunga mwezi mzima tukijiweka karibu na Mungu basi isije ikawa hii siku moja tukafanya mambo ya ajabu ambayo yataharibu maana yote ya kufunga siku 30. Tusherehekee ndani ya mipaka ya kisheria kwa usalama na amani bila ya maasi ya namna yoyote,” alisema.

Maandalizi ya sikukuu

Bei za bidhaa zimepanda kuelekea sikukuu hiyo. Mchuuzi wa mbuzi eneo la Vingunguti, Shadrack Waziri alisema tangu wiki hii ya mwisho ya mfungo wa Ramadhani, bei ya kitoweo hicho imepanda kutoka Sh80,000 hadi kati ya Sh100,000 na Sh130,000.

Katika mitaa ya Kariakoo, kilio kikubwa pia kilikuwa gharama.

“Hali zimezidi kuwa mbaya mwaka huu, nguo hazishikiki wenye watoto wengi tuna changamoto kubwa nguo zinaanzia Sh30,000,” alisema Halima Senkinda.

Wafanyabiashara kwa upande wao wamelalamikia ugumu wa biashara wakidai wateja wengi hawanunui nguo dukani na badala yake wanakimbilia kwa wachuuzi wa mtaani wanaopanga bidhaa chini.

Hali ilikuwa hiyo hiyo jijini Mwanza. Zulfa Mustapha, mkazi wa Kirumba alisema nguo aliyonunua Sh35,000 mwezi mmoja uliopita juzi aliuziwa kwa Sh45,000 katika duka hilohilo.

Akizungumzia ongezeko la bei, mfanyabiashara wa nguo mtaa wa Makoroboi, Andrew Mushi alisema wamelazimika kupandisha bei baada ya wauzaji wa maduka ya jumla kuongeza.

Katibu wa Bakwata Mkoa wa Mwanza, Sheikh Mohamed Balla aliiomba Serikali kudhibiti tabia na mazoea ya kila mwaka ya wafanyabiashara kutumia mfungo wa Ramadhani na sikukuu ya Idd kujinufaisha kwa kupandisha bei ya bidhaa kuanzia chakula hadi nguo.