IGM yafanyia kazi malalamiko ukiukwaji haki za binadamu mgodini Mwadui

Mtaalamu wa Baraza hilo  ambaye ni mwanasheria katika Baraza  hilo Natujwa Mvungi, akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga. Picha na Suzy Butondo

Muktasari:

  • Baraza huru  la usuluhishi lafanyia kazi malalamiko 5,573 ya wananchi wa vijiji 12 vinavyozunguka mgodi wa almas Mwadui.

Shinyanga. Jumla ya malalamiko 5,573 yahusuyo ukiukwaji wa haki za binadamu katika mgodi wa Almasi Mwadui, mkoani Shinyanga, yameshughulikiwa na Baraza Huru la Usuluhishi (IGM), lililoanza kazi Novemba mwaka jana.

Malalamiko hayo ni yale yanatokana na wananchi katika vijiji 12 vinavyozunguka mgodi huo, kwa mujibu wa mwanasheria katika baraza hilo, Natujwa Mvungi.

Amesema baraza hilo ni chombo huru kisicho cha kimahakama, kilianzishwa kushughulikia ukiukwaji haki za binadamu unaodaiwa kufanyika katika mgodi huo.

Mvungi amesema hayo leo Novemba 23, 2023; katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari ili wafahamu majukumu ya baraza hilo.

“Malalamiko yanayoshughulikiwa ni pamoja na yanayohusu watu kupigwa, kuumwa na mbwa, kubakwa, vifo, watu kupotea, na uharibifu wa mali. Baraza lilianza Novemba 2022 kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya kampuni ya Petra Diamond Limited inayomiliki mgodi wa Mwadui na kampuni ya uwakili ya Leigh Day,” amesema na kuongeza;

“...pamoja na mambo mengine, makubaliano hayo yalihusu kuanzishwa na kutekelezwa kwa mfumo huru usio wa kimahakama kushughulikia malalamiko yanayohusu uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu ambao unahusishwa na utendaji kazi wa kampuni za ulinzi katika mgodi wa Mwadui.”

Kwa mujibu wa Mvungi, IGM imeundwa kufuatia miongozo ya Umoja wa Mataifa juu ya biashara na haki za binadamu, kwa kuzingatia vigezo na ufanisi, na kuhakikisha linatekeleza majukumu yake kikamilifu bila ya kuathiriwa na mgodi.

Aidha, amesema  malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu ambayo wanayashughulikia ni kuanzia kipindi cha mwaka 2009 hadi 2021 na kwamba baraza hilo litafanya kazi kwa miezi 24 tangu kuanzishwa kwake mwaka jana na baada ya hapo litavunjwa.

Katika hatua nyingine, ametaja changamoto wanakumbana nazo kuwa ni uelewa hafifu wa walalamikaji, ukosefu wa ushahidi na ukweli kwa malalamiko yaliyowasilishwa na udanganyifu wa taarifa sahihi ya malalamiko yanayoletwa kwenye baraza.

Paul Mikongoti, kutoka baraza hilo amesema wamefanya mafunzo kwa waandishi wa habari ili wapate uelewa wa shughuli za baraza hasa wanapotimiza wajibu wao wa kuuhabarisha umma.

Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga wamesema walikuwa wakisikia tu kuhusu baraza hilo bila ya kuwa na taarifa za kina.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Shinyanga, Greyson Kakuru ameshukuru wanahabari kupata ufahamu kuhusu majukumu ya baraza hilo, huku akisema wataandika kwa kile kinachoendelea barazani humo.