IMF yaipa Tanzania mkopo wa Sh2.4 trilioni

Muktasari:

Ili kuongeza matumizi ya jamii, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeridhia mkopo huo kuongeza mzunguko wa fedha na kupunguza hatari ya kifedha kutoka kwa mashirika ya serikali, kibinafsi na Serikali za Mitaa.

Dar es Salaam. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeidhinisha mkopo wa dola za Marekani 1.046 bilioni (zaidi ya Sh2.4 trilioni) kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kurejesha uchumi ulioathiriwa na vita vya Russia na Ukraine na janga la Uviko-19.

Hii ni awamu ya pili Tanzania inapokea mkopo kutoka shirika hilo, tangu ilipofanya hivyo Septemba mwaka jana, ambapo mkopo wa Sh1.3 trilioni ulitolewa kukabili changamoto za kiuchumi zilizotokana na Uviko-19.

Katika taarifa yake iliyoitoa leo Julai 19, IMF ilisema “Uchumi wa Tanzania unashindwa kuimarika kutokana na vita hivyo, huku Uviko-19 ikizidisha changamoto katika maendeleo.”

Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani, imeshuhudia kupanda kwa bei ya bidhaa mbalimbali, zikiwemo mafuta ya dizeli na petroli, ngano, mbolea na mafuta ya kupikia.

Hali hiyo imeilazimu Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuchukua hatua kadhaa kupunguza gharama za maisha, kuendeleza miradi mikubwa na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi.

Mbali na kutoa ruzuku ya Sh100 bilioni kila mwezi kupunguza bei ya mafuta, hatua nyingine zilizochukuliwa ni kuongeza bajeti ya kilimo kutoka Sh294 bilioni hadi Sh954 bilioni ikiwa ni jitihada za kuinua uzalishaji wa ndani na kuzalisha ajira.

Akiwasilisha bajeti ya Sh41.48 trilioni kwa mwaka wa fedha 2022/23 bungeni mwezi uliopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, alisema Serikali itapunguza kiwango cha mafuta ghafi ya mawese kuanzia Julai 1, mwaka huu katika jitihada za makusudi za kupunguza mzigo wa mafuta.

Kabla ya hatua hiyo, mafuta ghafi yalitumika kuvutia ushuru wa asilimia 25 wa uagizaji ambao ulianzishwa mnamo 2018.

Kutokana na hatua hizo, IMF ilionyesha kuunga mkono mpango wa uimarishaji uchumi wa Tanzania, huku wataalam wake wakisema kunahitajika msaada ili kufanya mageuzi ya kiuchumi.

Katika mkopo huo, Tanzania itapokea dola za Marekani 151.7 milioni (zaidi ya Sh349 bilioni).

Mradi huo uliotangazwa na IMF ni sehemu ya Mpango wa Kuongeza Mikopo (ECF) unaolenga kusaidia kifedha na kuboresha utulivu wa kiuchumi kwa Tanzania, kufanya uwekezaji wa umma na kusaidia sekta binafsi.

"Kwa kutambua rekodi thabiti ya Tanzania katika utekelezaji wa mageuzi, wakurugenzi waliunga mkono maombi ya mamlaka ya kupanga utaratibu wa ECF ili kukidhi mahitaji ya dharura ya kifedha," amesema Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IMF na Kaimu Mwenyekiti wa bodi ya utendaji, Bo Li.