Italia kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ruaha kwenye fani ya utabibu

Muktasari:
- Balozi wa Italia nchini Tanzania, Marco Lambard ameahidi kuwaunganisha Rucu na vyuo vikuu vilivyopo Italia ili wanafunzi na chuo hicho waweze kupata fursa ya kujitanua kielimu. Pia, amesema wataendelea kudumisha umoja na mshikamano ulipo kati yao.
Iringa. Balozi wa Italia nchini Tanzania, Marco Lambard amesema nchi yake iko tayari kushirikiana na Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu) katika kupanua mafunzo ya afya yatakayosaidia kupunguza uhaba wa watumishi wa sekta hiyo nchini.
Balozi Lambard ameeleza hayo leo Alhamisi Machi 10, 2022 baada ya kutembelea chuo hicho na kujionea maendeleo ya ujenzi wa jengo la sayansi litakalo husisha maabara, famasia na hospitali ya chuo kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwa wanachuo.
“Nimekuja chuoni hapa nimejionea ujenzi wa jengo la sanyansi, ni zuri na litakapokamilika, chuo kitamudu kuongeza mitaala mipya ya afya lakini pia tutawaunganisha na vyuo vikuu vilivyopo Italia ili wanafunzi na chuo waweze kupata fursa ya kujitanua kielimu. Tutaendelea kudumisha umoja na mshikamano ulipo kati ya chuo na umoja katika Taifa la Tanzania,” amesema Lambard.
Katika taarifa yake kwa Balozi huyo, Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha anayeshughulikia fedha na utawala, Profesa Dominicus Kasilo amesema chuo hicho kinatarajia kuongeza mitaala mipya ya afya ili kupunguza uhaba wa watumishi wa afya nchini.
Profesa Kasilo amesema chuo hicho kina mradi wa sayansi ambapo wana jengo la gorofa nne na ndani ya jengo hilo wamekusudia likikamilika liwe na hospitali ambayo watu watakuwa wanatibiwa hapo na huduma zote za kihospitali zipatikane.
“Tutakuwa na mitaala ya mambo ya uuguzi, degree ya kwanza kwa watu wa maabara na famasia, sasa hilo ndio lengo kubwa kwa sababu sekta ya afya bado ina upungufu wa wataalam wengi na sisi kama chuo tumejikita kusaidia kuongeza idadi ya wataalamu wa afya.
“Tuna uhusiano na vyuo kadhaa vya kule Italia lakini tumeanza mazungumzo na hatujafikia mahali pazuri kwamba tunaanza kufanya kazi kwa pamoja, kwa hiyo sisi tumemleta balozi ili tumweleze hayo na kwamba kwa kuwa kule ni nyumbani kwake aweze kutuunganisha na vile vyuo vikuu vya nchini Italia,” amesema.
Kwa upande wake, Rais wa serikali ya wanafunzi katika chuo hicho, Eliubu Gondola amekiomba chuo hicho kukamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa wakati ili kuwezesha wanafunzi wa masomo ya afya kuanza kufanya masomo kwa vitendo.
Naye, Sista Anna Banda, mwanafunzi wa fakati ya afya, famasi amesema katika ugeni huo, Balozi amewaahidi kwamba watakuwa na ushirikiano kati ya chuo cha Ruaha pamoja na vyuo vilivyopo Italia.