Jaji aeleza sababu ya hukumu kesi za ujangili kuenguliwa na mahakama za juu

Thursday October 14 2021
jaji pc
By Beldina Nyakeke

Musoma. Imeelezwa kuwa watuhumiwa wengi wa kesi zinazohusu masuala ya wanyamapori na nyara za Serikali wanaohukumiwa vifungo mbalimbali na mahakama za ngazi za chini mkoani Mara,   huachiwa huru na mahakama za juu kutokana na ukiukwaji wa sheria.

Kati ya kesi 10 zinazokatiwa rufaa mahakama kuu kesi sita hufutwa hivyo watuhumiwa kuachiwa huru huku kesi nne pekee ndizo huonekana kukidhi matwaka ya sheria za hifadhi na maliasili.

Akizungumza mjini hapa leo Oktoba 14 kwenye kikao cha mafunzo kilichowajumuisha wapelelezi, waendesha mashataka na mahakimu wa ngazi za mahakama ya mwanzo hadi mkoa wa mkoa wa Mara, Jaji Mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Musoma, John Kahyoza amesema kuwa hali hiyo inasababishwa na maandalizi duni ya kesi hizo.

Amesema kuwa kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wapelelezi, waendesha mashtaka pamoja na mhakimu kufanyakazi kwa mazoea hivyo kupelekea rufaa nyingi kushinda na hivyo watuhumiwa wengi wa ujangili kuachiwa huru.

"Rufaa nyingi zinashinda kwa sababu ya kukosewa kwa nyaraka.

“Kwa mfano unakuta hati ya mashtaka, hati ya kukamatwa mtuhumiwa amekamatwa katika eneo la Simiti, halafu hati ya mashtaka inasema mtuhumiwa alikamatwa katika eneo la Simitu na kwenye ushahidi unakuta mtuhumiwa alikamatwa katika eneo la Simatu sasa unabaki unajiuliza hivi mpelelezi, mwendesha mashtaka na hakimu kweli wamefanya kazi yao ipasavyo?” amesema.

Advertisement

Ameongeza kuwa rufaa nyingi pia zinashinda kutokana na wahusika kutokuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yao, huku akitoa mfano mkanganyiko ambao hutokea mara kwa mara kuhusiana na mnyama aliyeuwawa.


"Mnasema Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani zinawatetea majangili hili sio kweli, jiulize wewe umetimiza wajibu wako kama itatokea hiyo. Hakuna Jaji anayempa ushindi mtuhumiwa endapo kesi yako imendeshwa vema kwa kuzingatia misingi yote ya kisheria.

“Timizeni wajibu wenu na sio kutuarushia lawama. Kwa mfano umemfunga mtu miaka 30 kwa kukutwa na nyara za Serikali, je mwenendo wa kesi ulizingatia mahitaji yote ya kisheria au tunafanya kwa mazoea?” amehoji.

Naye mwendesha mashtaka wa Serikali mkoani Mara, Venance Mayenga amesema kuwa kesi nyingi zinashindwa katika ngazi ya rufani kutokana na baadhi ya waendesha mashtaka kushindwa kutimiza wajibu wao na kufanya kazi kwa mazoea.

Advertisement