Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jaji Chande alivyofafanua tena ripoti yake, wapokea ‘sms’ za matusi 300

Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Jaji Mohamed Chande akizungumza katika mkutano wao na wahariri na waandishi wa habari.

Muktasari:

  • Aprili 23, 2026, Jaji Othman Chande ambaye ni Jaji Mkuu mstaafu, alikabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa na mapendekezo mbalimbali ikiwemo Serikali iunde Tume ya Uchunguzi wa Kijinai kufuatia matukio hayo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Jaji Mohamed Chande amesema tume hiyo kazi yake ilikuwa kubaini hoja kutokana na ushahidi uliowasilishwa.

Pia, Mjumbe wa Tume hiyo, Profesa Ibrahim Juma amesema baada ya kuwasilisha ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Aprili 23, 2026, baadhi ya wajumbe wa tume hiyo wamepokea ujumbe zaidi ya 300 za matusi.

Wameyasema hayo leo Jumanne, Aprili 28, 2026 jijini Dar es Salaam katika mkutano wao na wahariri na waandishi wa habari wakifafanua masuala mbalimbali na kujibu maswali waliyoulizwa.

"Tume kazi yake ya msingi ilikuwa ni kubaini hoja na kubaini hoja ni 'fact finding' kutokana na ushahidi uliowasilishwa mbele ya tume. Kujibu zile hadidu za rejea tulizopewa," amesema.

Amesema hadidu hizo za rejea ziliwataka kubaini chanzo, lengo la wahusika, nani wahusika, madhara ya kibinadamu kiuchumi, kijamii yaliyotokana na ghasia hizo na kubaini, kuzuia na kudhibiti kilichotokea.

Ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Aprili 23, 2026 ikionesha watu 518 walipoteza maisha wakati na baada ya uchaguzi kutokana na vurugu hizo.

Jaji Chande amesema ndani ya siku 153 ilizopewa kufanya kazi, kila siku ilikutana ana kwa ana na mashahidi 40.

Idadi hiyo ya watu iliyokutana nao kwa siku, amesema imefanya tume hiyo kwa siku zote 153 ilizofanya kazi, iwe imekutana na jumla ya watu 6,205 ana kwa ana.

Jaji Chande, ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo, Jumanne Aprili 28, 2026 alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari.

"Tume hii, imekutana ana kwa ana na watu 6,205. Sasa jiulize ni tume gani kwa siku 153 imekutana ana kwa ana na watu 6,205, hakuna duniani. Sisi tumesikiliza mashahidi na kuhojiana na watu 40 kwa siku moja," amesema.

Jaji Chande amesema tume hiyo ilijikita zaidi katika ushahidi uliotolewa na wananchi badala ya ule wa vyombo vya dola, hususan polisi.

Amesema katika mchakato wa uchunguzi wao, walipokea ushahidi mwingi uliowasilishwa kwa njia ya viapo, ambapo jumla ya vielelezo 953 vilitoka kwa raia, huku polisi wakitoa vielelezo 26 pekee.

Amesema ushahidi huo uliowasilishwa ulikuwa chini ya kiapo, ama kwa maandishi au kwa watu kufika mbele ya tume na kuapa, hatua ambayo ilisaidia kuongeza uzito wa taarifa zilizokusanywa.

Mbali na ushahidi wa viapo, Jaji Chande amesema tume hiyo pia ilitumia madodoso yaliyosambazwa kwa njia ya mtandao na kwa njia ya ana kwa ana, ambapo jumla ya madodoso 4,891 yalijazwa na kurejeshwa yakiwa na majibu ya maswali maalumu yaliyolenga kukusanya taarifa za kina kuhusu matukio ya uvunjifu wa amani.

Aidha, amesema tume ilifanya mikutano ya hadhara katika mikoa 11 tofauti nchini, pamoja na kuendesha majadiliano na makundi maalumu 201 yaliyohusisha jumla ya watu 3,565.

Kuhusu uwajibikaji, Jaji Chande amesema: “Wote tunakubaliana kuwe na uwajibikaji. Hakuna aliyesema hapa na hakuna aliyesema uahirishwe. Lakini nachosema uwe uwajibikaji wa haki na tulishauriwa na viongozi wakuu wa nchi tuliowaona kwamba anayestahili kuwajibika awajibishwe kwa mujibu wa sheria na asiyestahili kuwajibishwa asiwajibishwe.”

"Wengine wakaenda mbali zaidi kwamba asitolewe mtu kafara kwenye kuwajibishana. Ushauri huo tulipokea na ilibidi tusikilize pia maoni ya watu."

Pia, Jaji Chande, amesema wamebaini kuwa suala la kutekwa na kupotea kwa watu linahitaji kupewa kipaumbele katika uchunguzi.

Amesema ingawa Jeshi la Polisi lina kazi nyingi, ni muhimu kuwepo mkakati maalumu wa utatuzi wa changamoto za kutekwa na kupotea kwa watu na hilo lifanywe kwa kuanzia kwenye mizizi yake.

"Tumeona kwamba, katika upelelezi unaoendelea wa kesi za kutekwa na kupotea kwa watu, pamoja na mafanikio ya kuwapata wenzetu waliopotea, walijipoteza au waliotekwa, kuna umuhimu wa kuwa na mkakati maalumu wa kutatua," amesema.


Jumbe 300 za matusi

Mjumbe wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Profesa Ibrahim Juma amesema baada ya kuwasilisha ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Aprili 23, 2026, baadhi ya wajumbe wa tume hiyo wamepokea ujumbe zaidi ya 300 za matusi.

Profesa Juma ambaye ni Jaji Mkuu mstaafu amesema kitendo hicho, kinaashiria Tanzania kwa sasa kumezuka tabia aliyoiita hatari ya watu kuzima maoni ya wengine, huku wakitaka ya kwao pekee ndio yasikilizwe.

Amesema tabia hiyo imedhihirika hata baada ya kuwasilishwa ripoti ya tume hiyo, baadhi ya wajumbe wamepokea ujumbe zaidi ya 300 wa matusi katika simu zao, kutoka kwa watu hao ili kuzima maoni yaliyowasilishwa kupitia ripoti.

"Baada ya taarifa kutoka, tumepokea matusi zaidi ya 300 kwa sababu kuna mtu hataki maoni yetu yaliyopatikana kwa njia ya methodolojia ya kusikiliza watu yasiwafikie watu," amesema.

Aprili 23, 2026, Chande ambaye ni Jaji Mkuu mstaafu, alikabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam ikiwa na mapendekezo mbalimbali ikiwemo Serikali iunde Tume ya Uchunguzi wa Kijinai kufuatia matukio hayo. Tume hiyo itakuwa na jukumu la kupeleleza na kufuatilia masuala mahususi yanayohitaji upelelezi zaidi ili kushughulikia tuhuma zilizobainishwa katika taarifa ya Tume.

Masuala hayo ni pamoja na kubaini wahusika wakuu wa ghasia, matukio tatanishi ya vifo na majeruhi, maiti ambazo hazijapatikana na kupendekeza hatua za uwajibikaji.