Jaji Kihwelo awaonya madalali wa Mahakama

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Dk Paul Kihwelo

Muktasari:

Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama nchini wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kanuni ili kuondoa malalamiko yanayoelekezwa kwa Mahakama kutokana na ukiukwaji wa taratibu na kanuni za utendaji kazi wao.

Dar es Salaam. Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama nchini wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kanuni ili kuondoa malalamiko yanayoelekezwa kwa Mahakama kutokana na ukiukwaji wa taratibu na kanuni za utendaji kazi wao.

Kauli hiyo imetolewa Jumatatu ya Agosti 15, 2022 na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Dk Paul Kihwelo wakati akifungu mafunzo ya wiki mbili kwa wenye nia ya kufanya kazi ya Udalali na Usambaza Nyaraka za Mahakama.

Dk Kihwelo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani amesema baadhi ya maafisa hao wamekuwa wakikiuka taratibu za kazi hali inayosababisha tuhuma kurudishwa kwa Mahakama wakati mhimili huo unakuwa umeshatekeleza kazi yake ya kutoa uamuzi/amri za mashauri mbalimbali.

“Tunajua madalali na wasambaza nyaraka wa Mahakama ndio wanaotekeleza amri za Mahakama, baada ya Mahakama kutoa amri wao ndio wana wajibu wa kuitekeleza hiyo amri kama ni kubomoa nyuma, kukamata mali na kuuza na kadhalika, hivyo ni muhimu waelewe na kuzingatia sheria na taratibu za utendaji kazi wao ili Mahakama iondokane na malalamiko mbalimbali yanayotolewa,” amesem Dk Kihwelo na kuongeza

“Haya ni mafunzo ya awamu ya tisa tangu chuo hiki kianze kutoa mafunzo mwaka 2018, mafunzo haya yameondoa malalamiko mengi yaliyokuwepo kutoka kwa wananchi ambapo kwa kufanya hivi inawawezesha madalali na wasambaza nyaraka za Mahakama kufanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu zilizopo,” ameongeza.

Amebainisha kuanzishwa kwa mafunzo hayo ni moja kati ya sehemu ya uboreshaji wa huduma unaoendelea katika mhimili wa Mahakama lengo likiwa ni kuleta taswira chanya ya Mhimili huo kwa wananchi.

“Lengo kuu la mafunzo haya ni kuboresha utoaji huduma kwa jamii kwa weledi na kuhakikisha kuwa Mahakama inakuwa na Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wenye weledi, mbinu bora na nyenzo za kufanyia kazi,” anasisitiza

Amesema tangu kuanzishwa kwa mafunzo hayo mwaka 2018 hadi sasa Chuo kimeweza kuwajengea uwezo Madalali wa Mahakama 240 na Wasambaza Nyaraka za Mahakama 131.

Tumaini Mwamkonja ni dalali wa Mahakama kutoka Mkoa wa Rukwa, anasema mafunzo hayo yatamuwezesha kufanya kazi zake kwa weledi.

“Ninapotoka hapa nitakuwa nimeiva sana na nitaendaa kufanya kazi kwa maadili na kuleta tija kwa mahakama,” anasema Tumaini.

Kwa upande wake, Samuel Lusenga ambaye ni dalali wa mahakama kutoka mkoa wa Simiyu, anasema amekuja kuongeza ujuzi zaidi wa namna bora ya utekelezaji wa kazi za mahakama na usambazji wa nyaraka za Serikali, kwani miaka mitatu nyuma alishawahi kupata mafunzo kama hayo.

“Moja ya changamoto inayowakabili baadhi ya madalali ni uelewa mdogo wa namna bora ya utekelezaji wa kazi zao, hivyo kwa kulitambua hilo ndio maana mahakama imekuja na njia hii ya kutujengea uwezo sisi tunaotekeleza amri za mahakama” aansema

Katika awamu hiyo ya tisa ya mafunzo hayo, jumla ya watu 26 wameshiriki mafunzo hayo kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

Kwa mujibu wa Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama, za mwaka 2017, mwombaji wa kazi za Udalali na Usambaza Nyaraka za Mahakama anapaswa kuwa na cheti cha Umahiri cha mafunzo ya Udalali na Usambaza Nyaraka za Mahakama kinachotolewa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Aidha, ili kupata nafasi ya kusoma mafunzo haya mwombaji ni lazima pamoja na sifa nyingine awe angalau na cheti halali cha kumaliza elimu ya kidato cha nne.

Hata hivyo, baada ya kukamilika kwa utoaji wa mafunzo hayo, washiriki watafanya mitihani ya kupima umahiri wao na wakifaulu wanapatiwa cheti cha umahiri ambacho ni moja ya kigezo cha kuomba kazi ya udalali pamoja na usambaza nyaraka za Mahakama