Jaji Makaramba: Vyombo vya habari ni msingi wa  usalama wa Taifa lolote

Jaji mstaafu, Robert Makaramba

Muktasari:

Imeelezwa kuwa Taifa lolote linalojali usalama wake huwaacha wanahabari wafanye kazi zao kwa uhuru, kwani wao ndiyo wanajua wapi pako vizuri na wapi pana shida.

Dar es Salaam. Jaji mstaafu, Robert Makaramba amesema kuheshimu na kulinda uhuru wa wanahabari ndiyo msingi wa usalama wa Taifa lolote duniani.

Amesema kuminya  uhuru wa wanahabari na kutunga sheria lukuki dhidi yao, sawa na kutumia rungu kuuwa mbu.

Kilichoelezwa na Jaji Makaramba kinarejea maisha magumu iliyopita tasnia ya habari nchini katika kipindi cha miaka saba iliyopita.

Ndani ya kipindi hicho, malalamiko ya wanataaluma hiyo yalielekezwa kwa mamlaka za Serikali kuminya uhuru wa kupata taarifa na kutekeleza majukumu yao.

Hayo yanathibitishwa na matukio kadhaa ya kuvamiwa kwa vyombo vya habari, kutekwa, kuuawa na wengine kutishwa yaliyotokea katika vipindi tofauti ndani ya miaka hiyo.

Jaji Makaramba ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, alipohutubia hafla ya kumuaga Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) anayemaliza muda wake, Kajubi Mukajanga na kumkaribisha mpya, Ernest Sungura.

Amesema katika miaka ya hivi karibuni, taaluma ya habari ilitungiwa sheria kadhaa kukandamiza utendaji wake, akisema hayo ni matumizi makubwa ya nguvu yasiyo na sababu.

"Kama Taifa lolote linataka usalama wa hali ya juu, utapatikana kwa kuheshimu uhuru wa waandishi wa habari.”

"Serikali makini itaona waandishi wa habari ndiyo walinzi wa utendaji wa Serikali maana wao ndiyo wataona wapi inaharibikiwa  au inaenda vema," amesema.

Jaji Makaramba ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya MCT, amefananisha waandishi wa habari na kile alichokiita neno, lililotajwa katika Kitabu kitakatifu cha biblia.

Amesema ni wanahabari pekee ndiyo wenye uwezo wa kuongeza au kupunguza neno wakaathiri amani ya Taifa, hivyo ni vema waachwe huru kutekeleza majukumu yao.

"Serikali makini itawaacha waandishi wa habari ili waendeleze hilo neno, ni vibaya sana kumuona mtu  ana mwelekeo fulani mkaamua kumbadilisha eti kwa sababu akiachwa atasema," ameeleza.

Akizungumza katika hafla hiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema pamoja na umuhimu wa uhuru kwa wanataaluma ya habari ni vema watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya maadili ya kitaaluma.

Ameisisitiza kauli hiyo kwa hoja kuwa, "katika dunia ya sasa yenye maendeleo ambayo hata mtu asiyestahili anaweza kuandika habari, ni muhimu kuwepo chombo kama MCT ili kusimamia msingi ya taaluma ya habari," amesema.

Hata hivyo, Matinyi ameeleza matarajio yake kwa uongozi mpya wa MCT utakuwa chanzo cha kuimarika kwa taaluma ya habari kama ilivyokuwa kwa uongozi unaomaliza muda wake.

Katibu Mtendaji anayemaliza muda wake, Kajubi Mukajanga amesema utendaji wake wa miaka 15 ndani ya MCT uligubikwa na milima na mabonde mengi.

Amesema matarajio yake ni kuona asasi hiyo inaendelea kukua na kutoa mchango mkubwa kwa wanataaluma.

"Nafahamu Katibu Mtendaji mpya (Ernest Sungura) na nafahamu utendaji wake tulikuwa pamoja The Guardian, nina imani kwamba hapo nilipoachia mliodhani mmeona, mtaona zaidi," amesema.

Kwa upande wa Sungura, ameeleza mchakato wa kupatikana kwake ulianza tangu mwaka 2022 na rasmi alitangazwa mwaka 2023.

Hata hivyo, ameahidi kuendeleza yaliyofanywa na watangulizi wake, huku akibainisha tayari wameshaanza kufikiria maboresho ya maeneo mbalimbali ikiwemo Tuzo za Umahiri wa Waandishi wa Habari (EJAT).