Jaji Mkuu asema mahakama si chombo cha kuibeba serikali kushinda kesi

Muktasari:

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, amewataka wanasheria wa serikali walioko kwenye taasisi mbalimbali za umma, kuhakikisha wanajiandaa vyema kushinda kesi na kuwataka kutambua kuwa mahakama haipo kwa ajili ya kuipendelea serikali au kuikandamiza katika utoaji wa haki.


“Imewahi kusemwa kuwa nyuma ya kila Serikali, ipo timu madhubuti ya wanasheria wa Serikali, ambao wanafanya kazi kimya kimya nyuma ya pazia, na matunda ya juhudi zao ni amani, utulivu na utawala wa sheria unaowawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kisiasa, kijamii na kiuchumi”.

Hii ni kauli ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma alipokuwa akifungua mkutano wa pili wa Mawakili wa Serikali walio katika utumishi wa umma uliofanyika hivi karibuni jijini Dodoma.

Jaji Mkuu anasema, kila nchi inahitaji Serikali na kila shughuli ya maendeleo kiuchumi, kisiasa, na hata ulinzi, usalama na amani, hufanywa na Serikali kwa kuwezeshwa na Katiba na Sheria.

Kwa sababu hiyo, anasema wajibu aliopewa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi kusimamia na kuratibu utoaji wa huduma za sheria kupitia wizara, idara, vitengo na taasisi mbalimbali za umma utakuwa na mafanikio  kama au pale tu, taasisi husika na viongozi wao watakubali ushauri wa kisheria unaotolewa na kuheshimu kazi ngumu zinazofanywa na mawakili wa serikali.

Mkutano huo uliwakutanisha mawakili wa serikali wapatao  900 walioko katika utumishi wa umma kupitia wizara,  idara na taasisi zinazojitegemea, wakala na mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Profesa Juma katika kutilia mkazo nafasi, wajibu na majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anatoa ujumbe kwa viongozi mbalimbali wa Serikali kwa kusema;

 “Ujumbe wangu kwa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, madiwani na wakuu wa mashirika ya umma, mkubali ushauri wa kisheria kutoka kwa wanasheria wa serikali wanaofanya kazi katika maeneo yenu. Endapo mtaona ushauri wao hauwaridhishi zipo nganzi za kufuata hadi kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakili Mkuu wa Serikali”.

Anasisitiza Jaji Mkuu kwa kuwataka mawakili hao kuwasaidia viongozi kwa kuwashauri kabla hawajatoa amri na maagizo mbalimbali ambayo huzidisha migongano ya kisheria kwa serikali.

Anasema ni matumaini yake Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakubaliana naye kuwa wajibu aliopewa wa kusimamia na kuratibu utoaji wa huduma za kisheria kupitia wanasheria hao walio katika utumishi wa umma na ambao sasa kwa mujibu wa muundo mpya wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wanakuwa chini yake, utakuwa na  mafanikio, kama taasisi za umma na viongozi wao  watakubali ushauri wa kisheria unaotolewa.

Mawakili wa serikali waliopo nje ya ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali, kwa mujibu wa Jaji Mkuu Juma, wanafanya kazi katika mazingira yanayohitaji kuwekewa mizani yenye uwezeshaji mkubwa ili kuwawezesha kutoa ushauri wa kisheria kwa mujibu wa taaluma yao, na kwa uhuru.

Hata hivyo, anasema ili ushauri wao (wanasheria) uweze kuwa na tija na kukubalika katika taasisi wanazozitumikia, hawana budi kuepuka kujiingiza kwenye majukumu au kazi zenye migongano ya kimaslahi kwa serikali.

Jaji Mkuu anasema; “Uwakili wa serikali ni utumishi unaohitaji kuaminiwa na kuaminika, msitumie fursa ya kuaminiwa na kuaminika kwenu kwa maslahi binafsi dhidi ya manufaa ya umma. Nyie ni washauri wa kisheria wa viongozi kwenye maeneo yenu ya kazi, tumieni ujuzi, weledi na uadilifu mkubwa kufanya hivyo kwa maslahi ya taifa letu”.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu Profesa Juma, mawakili hao wakishindwa kutumia ujuzi, weledi na uadilifu mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yao, watasababisha mkanganyiko mkubwa miongoni mwa jamii ya Watanzania.

 

Maboresho ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Kuhusu maboresho yaliyofanywa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yakiwamo ya kuwaweka wanasheria wote walio katika utumishi wa umma kuwa mawakikli wa serikali kwa mujibu wa Hati Idhini ya Rais kupitia  Tangazo la Seriklai Na. 48 na Sheria mbalimbali ikiwamo ile ya Utekelezaji wa Majukumui ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Jaji Mkuu anasema maboresho hayo yamelenga kuleta tija na ufanisi kwenye kazi zinazofanywa na wanasheria walio katika utumishi wa umma juu ya utekelezaji wa majukumu yao.

Anasema ni matarajio ya watu wote hususani kwa Mahakama kuona kazi  za kisheria zinazofanywa za kuishauri serikali au kuendesha mashauri ya jinai, madai au  uandaaji miswada ya sheria kwa niaba ya serikali, yanatekelezwa kwa ufanisi.

“Mkiwa maafisa wa mahakama tunawatazamia kufanya kazi zenu katika misingi ya taaluma iliyowekwa kwa kuzingatia maadili, weledi, uwazi, uzalendo na usiri katika kutekeleza majukumu yenu,”anasisitiza Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu aliwakumbusha kwamba, wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na kupitia Katiba ya Tanzania, Serikali, Bunge na Mahakama, zinapata mamlaka zao kutoka kwa wananchi.

Alisema wanasheria katika sekta ya umma wahakikishe sheria zinalenga ustawi wa wananchi wa kawaida.

Anasisitiza kwamba, sheria wanazosimamia ni lazima zikidhi matarajio ya kimaendeleo, na ni muhimu sheria hizo zikawasaidia wananchi masikini kunufaika na Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025

 

Taasisi za umma kushitakiana mahakamani

Kupitia mkutano huo, Jaji Mkuu aliishauri Wizara ya Katiba na Sheria kuangalia namna ya kutatua changamoto ya taasisi moja ya umma kufungua mahakamani shauri dhidi ya taasisi nyingine ya umma.

Profesa  Juma alisema,  wakati  taasisi moja ya umma inapofungua shauri dhidi ya taasisi nyingine ya umma,  mara nyingi pande zote mbili zinawakilishwa na wanasheria wa serikali au pande zote mbili  zina ajiri  mawakili wa kujitegemea.

Athari ya taasisi ya umma kufungua shauri dhidi ya taasisi nyingine ya umma, licha ya kutumia kiasi kikubwa cha fedha za umma, Jaji Mkuu Juma anabainisha kwamba, mashauri yanayohusisha wizara, idara,  serikali za mitaa na taasisi zingine za umma, huchukua muda mrefu na kupunguza kasi ya maendeleo na matumizi ya rasilimali inayogombaniwa mahakamani.

Jaji Mkuu anatoa ushauri na kupendekeza kwamba,  ipo haja  ya kutumia njia ya usuluhishi badala ya  kupeleka mashauri  mahakamani pale taasisi za umma zinapokuwa na mgogoro wa kisheria.

“Wanasheria wa serikali, katika kesi zingine za madai, pale inapobidi mjaribu sana kulenga kufikia usuluhishi nje ya mahakama badala ya kuendesha kesi kwa miaka hata 10, kuanzia kesi inapoanza ngazi za chini hadi kufikia  Mahakama ya Rufaa,”anasema.

Kama hiyo haitoshi, Jaji Mkuu  anasema “Kuna wakati wanasheria wa serikali wanakiri  kwa pembeni, kuwa kesi wanayoendesha haina nafasi ya kushinda au hata wakishinda gharama hadi kupata  ushindi ni kubwa na kwamba, wanapambana tu kwa sababu mkuu wa idara au kitengo anasema hiyvo. Hapa ndipo haja ya kujenga imani ya mawakili hawa na kuwaruhusu wapate usuluhishi nje ya mahakama”.

Mawakili kujiandaa vema

Pamoja na kusisitiza haja na umuhimu wa taasisi za umma kutumia njia za usuluhishi badala ya mahakama pale inapobidi. Jaji Mkuu anawakumbusha tena mawakili wa serikali kujiandaa vema wanapoiwakilisha serikali mahakamani.

 “Vilevile nitumie fursa hii kuwataka wanasheria wote kutumia weledi na kujiandaa vizuri mnapoiwakilisha serikali mahakamani. Mara nyingi kumekuwapo na malalamiko kutoka upande wa Mahakama kwamba, baadhi ya wanasheria hawajiandai vizuri, hivyo kushindwa kwenye mashauri ambayo serikali ilipaswa kushinda,”anasema.

Jaji Mkuu anasema; “Wakati mwingine unaona wazi kuwa mawakili wa kujitegemea wanaonekana wamejitayarisha vyema zaidi. Hali hii haitoi picha nzuri kwa serikali mnayoiwakilisha mahakamani. Serikali ni chombo chenye nguvu kubwa, mawakili wa serikali walio bora ni kielelezo kizuri cha nguvu ya serikali katika kutekeleza sheria kwa maslahi ya wananchi”.

Jaji Mkuu anawataka wanasheria wa Serikali kutambua kuwa  mahakama ipo si kwa ajili ya kuipendelea serikali au kuikandamiza katika utoaji wa haki.

Anasema “Katika kutoa mizani sawa ya haki kwa kufuata misingi iliyowekwa na Ibara ya 107A (2) (a) ya Katiba, Mahakama inatakiwa kutenda haki kwa wote bila ya kujali hali ya mtu kijamii na kiuchumi”.

Kwa sababu hiyo, wito wa Jaji Mkuu kwa mawakili wa serikali wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kama maafisa mahakama katika kuisaidia Mahakama kufikia uamuzi wa haki.

Anasema, Huduma zinazotolewa na Mawakili wa Serikali ni lazima ziwe zenye ubora na shindani zaidi ya huduma zinazotolewa na mawakili wa kujitegemea au pia ziwe bora zaidi ya huduma za mawakili kutoka nje.

Jaji Mkuu anamshukuru Rais Dk John Magufuli kwa kufanya mabadiliko makubwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikiwa ni pamoja na kutambua umuhimu wa mawakili wa serikali.

Anasema “Mabadiliko ya kimuundo yaende sambamba na kuboreshwa kwa maslahi  na hali za maisha ya mawakili wa serikali, ikiwa ni pamoja na  kuongezwa kwa posho na stahili mbalimbali kwa wanasheria hao wanaofanya kazi katika utumishi wa umma, hasa kwa kuzingatia kwamba wanasheria hao hawawezi kujiingiza katika migongano  ya kimaslahi.