Jaji Mkuu ataka Tehama kuziba pengo watumishi mahakamani

Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amewataka Watumishi wa Mahakama kuchochea matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili sekta ya Mahakama iwe sehemu ya mabadiliko na yatakayoendana na Tanzania ya kidijitali.

Dodoma. Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amewataka Watumishi wa Mahakama kuchochea matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili sekta ya Mahakama iwe sehemu ya mabadiliko na yatakayoendana na Tanzania ya kidijitali.

Jaji Juma ameyasema hayo Mei 18, 2023 wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama jijini hapa, huku akisistiza matumizi yanasaidia kuziba pengo la upungufu wa watumishi wa Mahakama nchini.

Mapema mwaka huu, wakati wa uzinduzi wa wiki ya sheria, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Phillip Mpango alisistiza umuhimu wa matumizi ya Tehama mahakamani kwani inaongeza ufanisi na kusogeza huduma karibu na wananchi.

Vilevile Jaji Mkuu huyo, amewataka viongozi hao kuwa na utaratibu wa kukutana na watumishi mara kwa mara na kujenga tabia ya kujitafutia elimu kupitia mifumo ya kidijitali badala ya kusubiri kuwezeshwa kusoma na Serikali.

Kwa upande mwingine, Profesa Juma amewasihi Wakuu wa Kanda, Divisheni na Mikoa ya Uongozi wa Mahakama, kuacha ubinafsi wa kubana taarifa na maazimio yanayotolewa kwenye vikao na Mabaraza ya Mahakama.

“Viongozi wa Makao Makuu, Kanda, Divisheni na Wilaya, mjenge tabia ya kuwapa mrejesho watumishi katika maeneo yenu, hii tabia tunaenda kwenye mikutano tunarudi tu hatufanyi mrejesho siyo nzuri kwani shauku ya watu wetu waotutuma haijibiwi,” amesema Kiongozi huyo.

Kwa upande wake Kamishna wa kazi msaidizi, Andrew Mwawisi amesema ili Baraza liwe bora linatakiwa liwe na Chama cha Wafanyakazi chenye tija na kushawishi namna ya kufanya kazi kwa nidhamu.

Mwawisi amesema Baraza linatakiwa kufanya tathmini ya vikao vya Mabaraza ya Wafanyakazi kama yana mchango katika ukuaji wa maendeleo na kufanya vikao mara kwa mara kwa mujibu wa sheria.

“Pia Baraza linatakiwa kuwa na wajumbe watakaoweza kuishauri Kamati ya Baraza, kujenga hoja mbalimbali, kusimamia utekelezaji wa maazimio, kutunza siri na maadili makubwa yanayotolewa na Baraza,” amesema Mwawisi.