Jaji mkuu Tanzania aeleza mchakato hukumu kuandikwa kwa Kiswahili

Jaji mkuu Tanzania aeleza mchakato hukumu kuandikwa kwa Kiswahili

Muktasari:

  • Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amemueleza Rais John Magufuli kuwa mahakama imeanza mchakato wa hukumu kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili badala ya Kiingereza.



Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amemueleza Rais John Magufuli kuwa mahakama imeanza mchakato wa hukumu kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili badala ya Kiingereza.

Profesa Juma amesema ingawa utaratibu huo hauwezi  kwenda haraka kwa sababu baadhi ya nyaraka zipo kwa lugha ya Kiingereza lakini kwa mamlaka aliokuwa nayo ameshaanza kugawa kanuni kwa majaji  kuhusu mchakato huo.

“Baada ya miezi miwili au mitatu tutakuja na kanuni zaidi ya 50 zilizokuwa lugha ya Kiingereza na kuwekwa kwa Kiswahili. Lengo ni kesi ikija mahakamani ubishi usiwe kwenye tafsiri ya lugha, tubishane haki na siyo lugha,” amesema.

Ameeleza hayo leo Jumanne Februari 2, 2021 katika hafla ya kumuapisha Jaji Zephrine Galeba kuwa Jaji wa mahakama ya rufani iliyofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Kabla ya kupandishwa cheo na rais Magufuli baada ya kuandika hukumu kwa lugha ya Kiswahili, Jaji Galeba alikuwa Jaji wa mahakama kuu Kanda ya Musoma mkoani Mara.

Profesa Juma amemshukuru rais kwa kumteua Jaji Galeba  akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza mzigo kwenye mahakama ya rufani.

“Mahakama  ya rufani haina sifa nzuri kuna mrundikano wa mashauri unaotokana na uchache wa majopo wa kuamua kesi zinazosajiliwa kila siku. Tunashukuru huyu mmoja uliyetupa bado kuna wengine,” amesema.

Rais Magufuli amesema amemteua Jaji Galeba kutokana na ushujaa wake wa kuandika hukumu kwa Kiswahili licha ya utaratibu uliopo katika  mahakama mbalimbali hukumu kuandikwa kwa Kiingereza.

Jaji huyo alimshukuru Magufuli na kuahidi kutenda haki katika utekelezaji wa majukumu yake.