Jaji Mutungi: Wanawake ni mtaji kwa vyama vya siasa

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema wanawake ni mtaji mkubwa kwa vyama vya siasa, hivyo vinatakiwa kuwapa nafasi katika nafasi za uamuzi.

Jaji Mutungi amebainisha hayo leo Aprili 25, 2023 wakati wa warsha ya kupitia ripoti ya uchambuzi wa mapengo ya kijinsia katika nyaraka za kisheria za vyama vya siasa.

Amesema vyama vya siasa lazima viwe na mikakati ya makusudi kuhakikisha kwamba vinaongeza idadi ya wanawake wanaoshiriki katika nafasi za uamuzi.

"Wanawake ni mtaji mkubwa kwa vyama vya siasa, kwa wingi wao na hamasa yao katika kusimamia shughuli za vyama vyao vya siasa wakati wote hasa wakati wa uchaguzi.

"Lakini kiwango cha ushiriki wao katika vyombo vya uamuzi bado ni mdogo ukilinganisha na kiwango kilichopo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Vyama vya Siasa," amesema Jaji Mutungi.

Amesisitiza kwamba vyama vya siasa ni taasisi zenye fursa ya kutoa viongozi wa kisiasa, hivyo ni muhimu vikawa na misingi inayozingatia makundi mbalimbali ya jamii katika uongozi.

"Demokrasia ya kweli ni ile inayotoa fursa sawa za ushiriki wa makundi yote katika jamii," amesema Jaji Mutungi wakati wa warsha hiyo iliyowahusisha wanawake na wadau wengine kutoka kwenye vyama vya siasa na asasi za kiraia.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba amesema wanahitaji ushiriki wa wanawake uongezeke ndani ya mfumo wa demokrasia, na siyo kuulikaiweka kando demokrasia."

"Wanawake wanapogombea, hamasa wanayoileta ni kubwa sana. Tatizo ni ule mfumo, akigombea akapigiwa kura, atapata hizo kura na kutangazwa mshindi?" - Profesa Lipumba.

Akiwasilisha uchambuzi huo, mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Victoria Lihiru amesema vyama vingi vya siasa vimeandika dibaji nzuri sana kwenye Katiba zao inayohusisha ushiriki wa wanawake, lakini ukiingia ndani huoni tena,"

"Hakuna jitihada zozote za makusudi za vyama vya siasa kushirikisha wanawake.

"Kuna masuala lazima yaangaliwe kwa unyeti wake, kama ilivyo masuala ya Muungano, vivyo hivyo kwa masuala ya kijinsia," amesema Dk Lihiru.