Jalada kesi ya Chavda lapelekwa kwa DPP

Mshtakiwa Pravinchandra Chavda akitoka nje ya chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kusomewa shtaka linalomkabili. Picha na Pamela Chilongola

Muktasari:

  • Kesi ya Chavda iliyotarajiwa kuanza kusikilizwa leo katika hatua ya awali, imeahirishwa baada ya jalada la kesi hiyo kupelekwa Ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na sasa imepangwa kuendelea na hatua hiyo Desemba 14, 2023

Dar es Salaam. Jalada la kesi inayomkabili mfanyabiashara Pravinchandra Chavda (73), anayekabiliwa na kesi ya kudai amepoteza hati za umiliki wa viwanja vitano na makosa mengine limepelekwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya mapitio zaidi.

Jalada hilo limerejeshwa ofisi za DPP, wakati kesi hiyo imeshapangwa kuanza usikilizwaji wa awali, baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi umekamilika.

Chavda anayetetewa na Wakili Majura Magafu, alipandishwa kizimbani Oktoba 23, 2023 akikabiliwa na mashtaka mawili ya kujipatia mali kwa udanganyifu na kutoa taarifa za uwongo kwa askari polisi.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga, mshtakiwa huyo aliyakana na Wakili Mwanga aliieleza upelelezi wa kesi umekamilika, hivyo kuomba Mahakama hiyo ipange tarehe kwa ajili ya kumsomea hoja za awali mshtakiwa huyo.

Hakimu Mfawidhi Aaron Mathias anayesikiliza kesi hiyo alipanga kuanza usikilizwaji wa awali, leo Alhamisi, Novemba 23, 2023.

Hata hivyo, kesi hiyo ilipoitwa leo, Wakili wa Serikali, Frenk Michael akaieleza Mahakama kuwa jalada la polisi limeitishwa ofisi ya DPP kwa ajili ya mapitio, hivyo wanasubiri maelekezo.

"Jalada la polisi limeitishwa ofisi ya DPP kwa ajili ya mapitio, wameshindwa kuandaa hoja za awali hivyo wameiomba Mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya usikilizwaji wa awali," amedai Michael.

Kutokama na hali hiyo, Hakimu Mathias ameahirisha kesi hadi Desemba 14, 2023.

Katika shtaka la kwanza,  inadaiwa Januari 10, 2002, Chavda, mkazi wa Mtaa wa Nyang'oro, Upanga-Dar es Salaam, alijipatia kiwanja kitalu namba 1814 kilichopo Msasani Peninsula, jijini Dar es Salaam, baada ya kuwasilisha kwa msajili wa hati nyaraka za uwongo kinyume cha vifungu 301 na 302 vya sheria ya kanuni za adhabu.

Inadaiwa mshtakiwa huyo aliwasilisha nyaraka za uhamisho akijifanya ni mkurugenzi mtendaji pekee wa Kampuni ya Central Point Investment Limited, inayomiliki kiwanja hicho, wakati akijua sio kweli.

Katika shtaka la pili, Chavda anadaiwa Oktoba 7, 2019, katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa Jeshi la Polisi, kinyume cha kifungu cha 122(a) cha PC.

Inadaiwa siku hiyo mshtakiwa huyo alidai kupota hati miliki tano kwa nia ya kujipatia taarifa ya upotevu wa nyaraka hizo, akijua kuwa si kweli.

Mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.