Jalada kesi ya Mwakabibi, wenzake larudishwa Takukuru
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Lusubilo Mwakabibi
Muktasari:
- Upande wa mashtaka umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa jalada katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Lusubilo Mwakibibi na mwenzake limerudishwa Takukuru kwa ajili ya upelelezi zaidi.
Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Lusubilo Mwakibibi na Mratibu wa Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Edward Haule umedai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ametoa maelekezo jalada lirudishwe Takukuru kwa ajili ya upelelezi zaidi.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka wakiwa watumishi wa Serikali katika kesi ya Uhujumu Uchumi namba 63/2021.
Wakili wa Serikali, Winiwa Samson alidai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa hivyo kuna maelekezo kutoka kwa DPP jarada lirudishwe Takukuru kwa ajili ya upelelezi zaidi.
"Upelelezi bado haujakamilika hata hivyo jarada limerudishwa Takukuru kwa ajili ya upelelezi zaidi naiomba mahakama hii ipange tarehe nyingine," amedai Samson.
Katika kesi ya msingi kati ya Machi 2020 na Machi 2021 katika eneo la Manispaa ya Temeke washtakiwa hao wakiwa waajiriwa wa manispaa hiyo, katika utekelezaji wa ardhi walielekeza ujenzi wa stendi ya mabasi eneo la Buza, kiwanja ambacho kinamilikiwa na Dayosisi ya Kanisa la Anglikana bila kuwa na ruhusa.
Pia inadaiwa tarehe hiyo na maeneo hayo washtakiwa hao kwa makusudi wakitumia madaraka yao vibaya na kinyume na Kifungu cha 3(1) cha Sheria ya Ardhi na kifungu cha 3,4,5,7 na 11 cha Sheria ya Ardhi ya mwaka 2019.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 19, 2023 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa hao wapo nje kwa dhamana.