Kesi ya kina Mwakabibi yafikisha siku 724 bila upelelezi kukamilika
File Photo
Muktasari:
- Kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Lusubilo na mwenzake upelelezi haujakamilika kwa siku 724.
Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Lusubilo Mwakabibi na Mratibu wa Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Edward Haule haujakamilika kwa siku 724 sasa.
Agosti 20, 2021 washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka wakiwa watumishi wa Serikali na kesi ya Uhujumu Uchumi namba 63/2021.
Tangu Agosti 20, 2021 hadi leo Agosti 15, 2023 washtakiwa hao wamefikisha siku 724 ambapo upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Awali Wakili wa Serikali Monica Ndakidemi alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini bado wanaendelea na upelelezi.
"Naiomba mahakama hii ipange tarehe nyingine ya kutajwa Kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika,"alidai Ndakidemi.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Septemba 20, 2023 Kwa ajili ya kutajwa huku washtakiwa hao wakiwa nje kwa dhamana.
Katika kesi ya msingi kati ya Machi 2020 na Machi 2021 katika eneo la Manispaa ya Temeke washtakiwa hao wakiwa waajiriwa wa manispaa hiyo, wanadaiwa kuelekeza ujenzi wa stendi ya mabasi eneo la Buza, kiwanja ambacho kinamilikiwa na Dayosisi ya Kanisa la Anglikana bila kuwa na ruhusa.
Nyongeza na Shangwe Meshack