Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ni bajeti ya kujitegemea, Sh62.3 trilioni zaombwa

Muktasari:

  • Katika bajeti hiyo, Serikali imeweka mkazo katika kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kurasimisha sekta isiyo rasmi na kuharakisha matumizi ya mifumo ya kidijitali kama sehemu ya mkakati wa kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo kutoka nje.



Dar es Salaam. Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27 imejielekeza katika kujitegemea zaidi ikiwamo kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kulinda uzalishaji wa ndani.

Hatua hiyo imeelezwa bungeni jana na Balozi Khamis Mussa Omar alipowasilisha hotuba ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27, akiliomba Bunge liidhinishe Sh62.3 trilioni zitakazotumika kwa shughuli za maendelezo.

Waziri amelieleza Bunge kuwa bajeti ya mwaka huu wa fedha imelenga kuongeza mapato ya ndani zaidi kutokana na misaada ya washirika wa maendeleo kutarajiwa kupungua kwa asilimia 39.1 kwa mwaka 2026/27 ikilinganishwa na fedha zilizoahidiwa mwaka 2025/26.

“Hali hii inatokana na kubadilika kwa sera za baadhi ya washirika wa 155 maendeleo. Tunawashukuru washirika wetu wa maendeleo kwa msaada wao pale walipoweza,” amesema.

Hata hivyo, Balozi Omar amesema Tanzania ni Taifa na wananchi wake ndiyo wenye wajibu wa kulijenga.

 Amesema ni wajibu wa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, kulipa kodi kwa hiari na kushikamana na Serikali katika kuleta maendeleo.

Balozi Omar amesema mwaka 2026/27 Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh 62.33 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.3 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2025/26 ya Sh56.49 trilioni.

 Amelieleza Bunge kuwa mapato katika mwaka mpya wa fedha yanatarajiwa kuwa Sh46.79 trilioni na mapato ya kodi ni Sh 36.99 trilioni, mapato mengine ni Sh9.24 trilioni (ikijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Sh1.97 trilioni na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo Sh 563.1bilioni.

“Ili kuendana na dhamira yetu ya kujitegemea katika uendeshaji wa Serikali na maendeleo, takribani robo tatu ya bajeti yote ya mwaka 2026/27, sawa na asilimia 74.2 inatarajiwa kugharamiwa na mapato ya ndani,”amesema.

Miongoni mwa mikakati ya Serikali katika kujitegemea, imeongeza tozo na kodi katika bidhaa mbalimbali za nje ikiwamo kodi kwenye magari yaliyotumika; kwa magari yaliyodizi miaka 20 na kuendelea kodi yake ni asilimia 50.

Pia, Serikali imeweka mkakati wa kupata fedha kwa ajili ya Bima ya Afya kwa Wote kwa kuongeza kodi ya Sh20 kwa kila sigara 1000 na Sh10 kwa kila kilo moja ya sukari.

Mbali na hiyo, katika kuongeza uwekezaji kwenye sekta ya madini na kuhakikisha Serikali inanufaika na sekta hiyo, imependekezwa kuanzishwa mfuko wa utafiti wa madini nchini utakaokuwa ukipata asilimia 10 kutokana na mauzo ya madini.

Pia, katika kuwezesha wananchi Serikali imependekeza kuongeza asilimia ya mikopo wa wanawake, vijana na wenye ulemavu kutoa asilimia 10 hadi asilimia 15, kiwango ambacho huwa kinatengwa kwenye halmashauri.

Tozo zingine ambazo Serikali imependekeza ni tozo ya usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi kwa kiwango cha asilimia 30 ya thamani ya mzigo (FOB) au Sh200 kwa kila kilo moja kutegemea na kiwango kitakachokuwa kikubwa kwenye taka za karatasi (waste paper) zinazotambulika kwa HS Code 4707.00.00.

Lengo la hatua hiyo ni kuchochea uongezaji wa thamani nchini na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi hiyo kwa wazalishaji wa karatasi na maboksi nchini.

 Hatua hiyo inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh415 milioni.

Mapendekezo ya bajeti hayakuwaacha wacheza Kamari; Serikali imependekezwa kutozwa kwa ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia tano kwenye thamani ya dau la kamari inayochezwa kwa njia ya michezo ya kubashiri ya ardhini au mtandaoni.

Hatua hiyo itajumuisha michezo ya kasino ya ardhini au mtandaoni, mashine za sloti arobaini (forty machine) pamoja na michezo ya vikaragosi (virtual games operations).


Bima ya Afya kwa Wote

Katika suala la kujitegemea, Serikali baada ya kupitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote mwaka 2023 na kuanza kufanya kazi, imekuja na pendekezo la uanzishaji wa vyanzo vya ziada vya mapato kwa ajili ya kugharamia Bima ya Afya kwa Wote kwa kuongeza ushuru kwenye sigara na sukari.

Hatua hiyo ya Serikali itafikiwa kufuatia mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 ya kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwa Sh20 kwa kila sigara 1,000  zinazotambulika kwa HS Heading 24.02 na 24.03.

Mwaka 2025/26 Serikali ilianzisha vyanzo vya mapato kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya Ukimwi na kugharamia Bima ya Afya kwa Wote ikilenga kuongeza mapato ya Serikali kwa kipindi hicho kwa Sh586.4 milioni.

Tozo hii itakusanywa na Bodi ya Sukari Tanzania na kuwasilisha kwenye Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote, hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh7.5 bilioni.

Awamu ya kwanza, jumla ya wananchi 1,457,602 sawa na kaya 276,004; wazee 229 na watoto 267; wizara ilisema watasajiliwa na kugharamiwa na Serikali.

Ili kugharamia kaya zisizo na uwezo mahitaji yaliyotajwa wakati huo na Serikali ni Sh587.6 bilioni na bajeti ya mwaka 2025/26 ni Sh201 bilioni na kiasi kilichotolewa ilikuwa Sh48.8 bilioni.


Uchumi wa kidijitali wapewa msukumo

Sambamba na kuongeza mapato ya ndani, Serikali imeweka mkazo katika kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kuhamia kwenye mifumo ya malipo ya kidijitali.

Amesema kuanzia mwaka wa fedha 2026/27 malipo katika sekta mbalimbali yatafanyika kwa njia za kidijitali.

Maeneo hayo ni nauli za mabasi ya mwendokasi, vivuko, madaraja, mabasi ya masafa marefu, teksi mtandao, reli, usafiri wa anga na maegesho ya magari.

Pia, biashara katika shopping malls, vituo vya mafuta, sinema, gym, kumbi za mikutano, viwanja vya michezo pamoja na maonesho ya Sabasaba na Nanenane zitalazimika kutumia mifumo ya malipo ya kidijitali.

Katika sekta ya elimu, ada na michango yote kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu, italipwa kwa njia za kielektroniki.

Huduma za hoteli, migahawa, utalii, biashara ya ardhi, majengo, mashamba pamoja na shughuli za mazao ya kimkakati kupitia AMCOS nazo zitahusika katika mfumo huo.


Serikali kubana matumizi

Mbali na kuongeza mapato, bajeti hiyo imeweka mkazo katika kubana matumizi yasiyo na tija.

Balozi Omar amesema Serikali itaendelea kudhibiti safari za ndani na nje ya nchi pamoja na kupunguza semina, warsha na makongamano yenye gharama kubwa bila matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi.

Amesema mifumo ya ukaguzi wa ndani, udhibiti wa matumizi na usimamizi wa fedha za umma, itaendelea kuimarishwa ili kuzuia upotevu wa rasilimali za Taifa.

Serikali pia itaunganisha mifumo yote ya fedha za umma ikiwamo ya mapato, matumizi, mali na madeni ili kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Amesema mapendekezo ya Serikali mashirika ya umma yameelekezwa kujiendesha kwa ufanisi zaidi, huku yale yanayofanya biashara yakitakiwa kuandaa mikakati ya kujiondoa kwenye utegemezi wa ruzuku za Serikali.

Mashirika yenye faida pia yatahamasishwa kujiorodhesha katika Dar es Salaam Stock Exchange ili kuongeza mtaji na kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali.

Katika hatua ya kuendana na matumizi ya nishati safi, taasisi zote za umma zimeelekezwa kuanza kuzingatia ununuzi wa magari yanayotumia umeme na gesi katika mipango na bajeti zao.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali pamoja na utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje.

“Tunataka taasisi za umma ziwe sehemu ya mageuzi ya matumizi ya nishati safi kwa kuanza kutumia magari ya umeme na gesi, jambo ambalo litapunguza gharama na kuongeza ufanisi,” amesema.


Bidhaa za urembo zaguswa kodi mpya

Pia, Serikali imesema itaendelea kuweka vivutio vya kikodi ili kuhamasisha kilimo cha mazao ya mafuta, kuongeza matumizi ya mbegu zinazozalishwa nchini na kuimarisha viwanda vya ndani vinavyochakata na kuzalisha mafuta ya kupikia.

Amesema katika sekta ya pamba, Serikali imependekeza hatua za kuendelea kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha vitambaa na bidhaa zinazotokana na pamba inayozalishwa nchini.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)kwenye nguo na mavazi yanayozalishwa kwa kutumia pamba ya ndani.

Waziri Omar amesema hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya malighafi za ndani, kuimarisha ushindani wa viwanda vya ndani na kuongeza thamani ya zao la pamba.

“Hatua hii inatarajiwa kuokoa mapato ya Serikali yanayotokana na marejesho ya VAT kwa walipakodi yenye thamani ya Sh6.3 bilioni,” amesema.


Magari ya umeme kupewa nafuu

Katika jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi, Serikali imependekeza kusamehe VAT kwenye vifaa vinavyotumika katika vituo vya kuchaji magari ya umeme vinavyoingizwa nchini.

Pia, imependekeza kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa baadhi ya magari yanayotumia umeme.

Waziri Omar amesema hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya nishati mbadala, kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli na kulinda mazingira.

Kwa mujibu wa makadirio ya Serikali, utekelezaji wa hatua hizo utapunguza mapato ya Serikali kwa takribani Sh5.97 bilioni.

Amesema Serikali inaendelea na mazungumzo na viwanda vya kuunganisha magari vilivyopo nchini ili kuweka utaratibu wa kutoa vivutio maalumu vya kikodi kwa wawekezaji watakaojihusisha na uunganishaji wa magari ya umeme hapa nchini.


Mita janja za gesi zaguswa

Katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Serikali imependekeza pia kusamehe VAT kwenye mita janja za gesi ya kupikia (LPG Smart Meters) zinazoingizwa nchini.

Msamaha huo utatolewa kwa kampuni na taasisi zinazojihusisha na usambazaji wa gesi ya kupikia.

Waziri Omar amesema hatua hiyo inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa Sh16.8 milioni, lakini itachangia kuongeza matumizi ya gesi safi ya kupikia na kupunguza utegemezi wa nishati zinazoharibu mazingira.

Kwa upande mwingine, Serikali imependekeza kuongeza ushuru wa bidhaa kwa magari yaliyotumika yanayoingizwa nchini.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, magari yenye umri wa miaka minane hadi 10 yatatozwa ushuru wa asilimia 20 badala ya asilimia 15 ya sasa.

Magari yenye umri wa zaidi ya miaka 10 lakini yasiyozidi miaka 20, yatatozwa ushuru wa asilimia 40 badala ya asilimia 30, huku yale yenye umri wa zaidi ya miaka 20 yakitozwa ushuru wa asilimia 50.

Waziri Omar amesema hatua hiyo inalenga kuongeza mapato ya Serikali na kudhibiti uingizaji wa magari chakavu ambayo huongeza changamoto za mazingira na gharama za usimamizi wa taka ngumu.


TRA kutumia akili unde kuongeza mapato

Mbali na hatua za kikodi, Serikali imetangaza mikakati mipya ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutumia teknolojia.

Waziri Omar amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaongeza matumizi ya Akili Unde (AI), mifumo ya kidijitali na teknolojia ya msimbo pau (barcode) katika kufuatilia bidhaa zinazoingizwa na kuuzwa nchini.

Amesema matumizi ya teknolojia hizo yatasaidia kupunguza ukwepaji kodi, kuongeza uwazi na kuimarisha usimamizi wa mapato ya Serikali.


Matumizi ya fedha taslimu kuounguzwa

Katika hatua nyingine pia, Serikali imesema inadhamira ya kuendelea kupunguza matumizi ya fedha taslimu kwa kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali.

Waziri Omar amesema hatua hiyo inalenga kupunguza ubadhirifu wa fedha, kuongeza uwazi na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Sambamba na hilo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeelekezwa kuanza kuondoa matumizi ya vocha za simu za kukwangua kwa mkono na kuhamia mfumo wa kidijitali.

Amesema utekelezaji wake utaanza katika maeneo ya mijini kabla ya kusambazwa nchi nzima kulingana na matokeo ya tathmini ya awali.


Bidhaa za urembo, viatu vya plastiki

Katika mapendekezo mengine ya kodi, Serikali imependekeza kuongeza ushuru wa bidhaa za urembo zinazoingizwa nchini kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15.

Aidha, viatu vya plastiki vitatozwa ushuru wa asilimia 10, huku ushuru wa kamba za nyuzi za plastiki ukiongezwa kutoka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 25.

Pia, imependekeza kutoza ushuru wa asilimia tano kwa magari yenye ujazo wa injini usiozidi CC 1,000 yanayoingizwa nchini.